TUJIKUMBUSHE: Jonas Mkude apata ajali, mmoja afariki dunia

MASHABIKI wa soka kwa sasa kiroho safi baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza kuanza kwa mazoezi kwa klabu za soka, ikiwa ni maandalizi ya kuanza upya kwa mechi za ligi mbalimbali nchini baada ya kusimamishwa kwa zaidi ya siku 70 ili kupambana na virusi vya corona.

Kama ada Mwanaspoti katika kuwapa burudani wasomaji wake tunaendelea kujikumbusha na leo ikiwa Mei 28 tunarudi hadi mwaka 2017 ikiwa ni siku moja tu, tangu Simba ilipotwaa ndoo ya FA pale Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa kuinyoa Mbao FC, kiungo wao Jonas Mkude alipata ajali ya gari maeneo ya Dumila mkoani Morogoro.

Mkude alipata ajali hiyo iliyosababisha kifo cha mmoja wa mashabiki wao Shose Fidelis huku chanzo cha ajali hiyo kikiwa ni tairi la nyuma kupasuka ambapo gari lilikosa mwelekeo.

Mkude aliondoka jijini Dodoma asubuhi na gari binafsi aina ya Toyota Land Cruiser V8 huku akiwaacha wenzake waliofuata na gari la timu wakifuata nyuma yao.

Baada ya ajali hiyo, Mkude alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kupatika matibabu ya awali na baadaye kuhamishiwa Dar es Salaam.

Simba ilitwaa ubingwa huo ikiwa ni baada ya kushindwa kushiriki michuano ya kimataifa kwa miaka minne mfululizo ambapo kwenye fainali hiyo Simba ilishinda bao 2-1, mabao ya Simba yalifungwa na Fredrick Blagnon na Shiza Kichuya wakati bao la Mbao lilifungwa na Robert Ndaki.