MAKA EDWARD: Jiwe lililokataliwa na waashi limegeuka kuwa jiwe kuu

Monday August 26 2019

 

By THOMAS NG’ITU

KUFANYA vizuri kwa Simon Msuva kule Morocco katika klabu yake ya Al Jadida, bila shaka ilikuwa njia nyepesi kusajiliwa kwa beki, Nickson Kibabage.

Pia, mchangao wa Msuva bila shaka umechangia kwa kiungo Maka Edward kupata timu, kutokana na rekodi ambazo ameweka winga huyo kule Morocco.

Sasa ipo hivi, soka la Bongo limezidi kuchanua kwani nyota wa zamani wa Toto Africans na Yanga, Maka Edward wiki iliyopita naye alisaini mkataba wa miaka minne katika Klabu ya Athletico De Tetuan ya Ligi Daraja la Kwanza kule Morocco.

Maka kabla ya kwenda Morocco alitimkia Latvia lakini alirejea nchini kimyakimya na baadaye kuibukia Morocco.

Mwanaspoti lilifanya mazungumzo na Maka kutaka kufahamu hatua zote alizopitia hadi kutua Athletico De Tetuan ambayo ina uhusiano na Atletico Madrid inayoshiriki Ligi Kuu Hispania.

UGUMU WA MAISHA LATVIA

Advertisement

Wakati akiondoka nchini na kutimkia Latvia kufanya majaribio, wengi walikuwa wakishangazwa na mchezaji huyu kwenda sehemu ambayo haina ushindani mkali wa soka.

Hata hivyo, Maka Edward aliyewahi kusaini Simba na Yanga kwa wakati mmoja (kabla ya klabu hizo kuafikana) aliwahi kusema anaenda kupambana ili kucheza soka la kulipwa nje ya nchi lakini mambo yalikuwa tofauti alipoenda Latvia.

“Kule maisha yalikuwa magumu, nilikuwa nakula mlo mmoja kwa siku, wao walikuwa wanachukulia kawaida kwasababu walikuwa wamezoea,” alisema.

Kuhusu majaribo yake Latvia, Maka alisema: “Kitu kilichotokea kulikuwa na viungo wawili halafu niliambiwa kabisa sina kitu ambacho niliwazidi, kwahiyo kama kusajiliwa ni mpaka wamuuze mmoja ndipo hapo wakala wangu akaniambia nirudi wakati akihangaika sehemu nyingine ndio likaibuka dili la Morocco,” anafichua.

MOROCCO

KWEPESI TU

Baada ya kurejea nchini, Maka aliamua kukaa kimya tu na kutofanya lolote kwasababu hesabu zake zilikuwa hazipo tena Bongo.

“Unajua Yanga nilikuwa sipo kabisa katika mipango yao, kwahiyo na nilikuwa nimeshajiondoa katika Ligi ya Bongo, nikaambiwa nahitajika kwenda Morocco, basi nikaondoka,” alisema.

Aliongeza licha ya kwamba alikuwa hana mpango wa kucheza Ligi ya Bongo, alikuwa anajifua akijua lolote linaweza kutokea.

MECHI ZA ZAMPA ULAJI

Baada ya kufika Morocco, Maka alisema alikutana na mazingira tofauti kabisa katika upande wa soka. Lakini hilo halikumfanya akate tamaa ya kupambana kwani alikuwa anapiga tizi na wenzake na ndipo kukawa na mechi za kirafiki.

Maka alisema kama isingekuwa mechi za kirafiki, hana uhakika kama angeweza kupata shavu katika klabu hiyo, lakini mechi hizo zimempa ulaji baada ya kucheza soka safi.

“Tulicheza mechi nne za kirafiki, katika mechi hizo nilikuwa mchezaji bora wa mechi mara zote, ndipo nikajihakikishia nafasi na kweli ikawa hivyo, lakini mkataba wangu na Yanga ulitaka kunibana,” alisema.

YANGA KIROHO SAFI

Wakati kiungo huyu akihangaika kutafuta maisha kuchezwa soka la kulipwa nje ya nchi, bado alikuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Yanga.

Baada ya kufuzu majaribio Morocco, Maka alisema ilimchukua siku kadhaa kusaini mkataba kutokana na kubanwa na mkataba wa Yanga.

“Unajua nilikuwa na mkataba pale Yanga, kwahiyo ilibidi mazungumzo yafanyike na ndipo wakakubaliana, sijui ilikuaje lakini nilikuwa naamini nitabaki Morocco kwasababu sikuwa katika mipango ya Yanga,” alisema.

Maka aliongeza baada ya mazungumzo ya pande mbili, wakala wake alimuambia asaini kwa sababu walishakamilisha kila kitu.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alikiri uongozi wa Yanga kumuachia kwa moyo mmoja Maka kwenda kujaribu maisha yake sehemu nyingine.

“Hatujamuuza lakini tuliwapa barua ambayo imewaruhusu kumtumia, kwenye makubaliano mengine tutakuwa na asilimia 20 ambayo tunaipata pindi mchezaji huyu akiuzwa,” alisema.

LUGHA

CHANGAMOTO

Kama ambayo Msuva alivyopata tabu wakati akiingia Morocco, basi ndivyo ilivyo kwa Maka.

Kiungo huyo anasema kwa wiki kadhaa alizokaa Morocco, changamoto kubwa aliyokutana nayo ni lugha zinazotumika.

“Binafsi nazungumza Kiingereza na Kiswahili, huku jamaa wanazungumza Kiarabu, Kispeini na Kifaransa, ilinipa changamoto na itaendelea kunipa changamoto lakini sina budi kupambana,” alisema.


AWASIKILIZIA MSUVA NA KIBABAGE

Licha ya kukaa Morocco kwa takribani wiki tatu kabla ya kurejea Bongo kuweka sawa mipango ya hati yake ya kusafiria, Maka anafichua hajapata muda wa kuonana na Wabongo wenzake, Msuva na Kibabage wanaocheza katika Klabu ya Difaa Al Jadida, akisema atafurahi wakikutana.


Advertisement