Jipange: Pep bado anasubiri kwa Jose Mourinho

Muktasari:

Pambano la kesho linatazamiwa kuwa la kisasi kwa Guardiola na kikosi chake ambacho April mwaka huu walizuiwa kutangaza ubingwa wa England mbele ya Manchester United kwenye Uwanja wa Etihad katika mechi iliyokuwa ya kusisimua

LONDON, ENGLAND. PEP Guardiola mkali, lakini Jose Mourinho bado mkali zaidi na Pep ana safari ndefu ya kumfikia Jose Mourinho. unaweza kushangaa lakini hayo ndio maoni ya mtu mmoja muhimu alipoulizwa kuhusu nani zaidi kati ya wababe hao katika soka la England.

Manchester City na Manchester United zinakutana kesho katika dimba la Etihad katika pambano la kwanza la msimu huu baina yao na tayari joto baina ya pambano hilo limepanda huku vita baina ya makocha wa timu hizo waliowahi kuburuzana nchini Hispania ikiwa imehamia England kwa sasa.

Paul Merson, kiungo wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya England ambaye kwa sasa ameibuka kuwa mchambuzi mtata England amedai kwamba mpaka sasa Mourinho ni kinara kwa Pep hata kama kocha huyo Mhispaniola anafundisha soka la kuvutia.

Mourinho na Guardiola wamekutana mara tano katika soka la England michuano mbalimbali na kila timu imeshinda mechi mbili huku wakitoka sare moja. Hata hivyo Guardiola ameiwezesha City kuchukua ubingwa wa England msimu uliopita na kufikisha pointi 100 kwa mara ya kwanza katika historia ya England.

Wakati huo huo United imekuwa na wakati mgumu tangu Guardiola atue England na Mourinho anaonekana kuchemsha kutoa upinzani katika misimu yake miwili Old Trafford licha ya kuiwezesha United kushika nafasi ya pili msimu uliopita.

Lakini Merson alipoulizwa ni kocha gani ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika soka la England alidai kwamba bado anaamini kuwa Mourinho ana mchango mkubwa zaidi ukizingatia kazi aliyowahi kuifanya akiwa na Chelsea.

Mourinho aliwasiuli England mwaka 2004 akitokea Porto ya Ureno na kuanzia hapo alitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya England katika vipindi tofauti na Merson anaamini mpaka Pep Guardiola atwae kwanza mataji matatu ndipo wanaweza kuzungumza lugha moja.

“Pep ndio kwanza ameanza Ligi hii. Ametumia pesa nyingi na amekuwa mkali kwa wengine. Hata hivyo msimu wake wa kwanza hakufanya lolote. Alitumia pesa nyingi kwa walinzi wa pembeni na ameitengeneza timu yake kw namna anavyotaka icheze. Kwa sasa hawakamatiki.” Alisema Merson.

“Lakini alichofanya Mourinho kwa Chelsea ni kitu kikubwa. Lakini hapo hapo jiulize, Pep angeweza kutwaa ubingwa wa Ulaya na Porto kisha Inter Milan? Sina uhakika. Wote ni makocha wazuri sana lakini mpaka Pep atwae mataji matatu ya Ligi Kuu England ndipo tunapoweza kumuweka kando ya Mourinho.” alisema Merson.

Pambano la kesho linatazamiwa kuwa la kisasi kwa Guardiola na kikosi chake ambacho April mwaka huu walizuiwa kutangaza ubingwa wa England mbele ya wapinzani wao katika dimba la Etihad katika mechi iliyokuwa ya kusisimua.

Katika pambano hilo, hadi mapumziko United walikuwa wamechapwa mabao 2-0 na City kupitia kwa mabao ya mlinzi, Vincent Kompany na kiungo, Ilkay Gundogan. Hata hivyo United walisawazisha mabao hayo mawili katika kipindi cha pili kupitia kwa kiungo wao wa kimataifa wa Ufaransa, Paul Pogba aliyefunga mabao mawili ndani ya sekunde 97.

Baadaye mlinzi, Chris Smalling alifunga bao la ushindi la tatu na kuwaacha City wakisubiri mechi nyingine kutangaza ubingwa wao.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa City kupoteza mechi baada ya kuongoza kwa mabao mawili tangu walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho Oktoba 2008. Kwa upande wa Guardiola mwenyewe hiyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kwa timu yake kufungwa baada ya kuongoza kwa mabao mawili. mara yake ya mwisho ilikuwa Desemba 2013 akiwa na Bayern Munich wakati walipoongoza mabao 2-0 dhidi ya timu yake ya sasa Manchester City lakini wakaishia kuchapwa mabao  3-2