Jinamizi la Nyoni laitesa safu ya ulinzi Simba kwa Al Ahly

Muktasari:

  • Mabeki wa Simba wameshika hatima ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Pengo la Erasto Nyoni limeendelea kuigharimu safu ya ulinzi ya Simba na kuacha hofu kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly.

Nyoni alipata majeruhi katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi amekuwa akisaidia vilivyo safu ya ulinzi ya Simba kutokana na utulivu alionao pamoja na uwezo wake wa hali ya juu kuwapanga mabeki wenzake sambamba na kusawazisha makosa yao pale wanaposhambuliwa tofauti na sasa ambapo Simba inaonekana kukosa mtu wa namna hiyo.

Kwa kudhihirisha kuwa pengo la Nyoni limeitesa Simba, katika mechi 10 ambazo hajacheza, timu hiyo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Safu ya ulinzi ya Simba imeshikilia hatima ya timu hiyo kwenye mechi yake ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa kesho jioni.

Kufanya vibaya kwa safu hiyo ya ulinzi katika siku za hivi karibuni, kunaiweka kwenye wasiwasi mkubwa Simba kwenye mchezo huo ambao inalazimika kuibuka na ushindi ili kuweka hai matumaini yake ya kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Takwimu za mechi tano zilizopita ambazo Simba imecheza kwenye mashindano mbalimbali zinaonyesha kuwa safu yake ya ulinzi imeruhusu wastani wa mabao mawili katika kila mchezo jambo linaloiweka kwenye hatari mbele ya washambuliaji wa Ahly ambao wamekuwa hawana ajizi mbele ya lango la timu pinzani.

Katika mechi tano za mwisho ambazo imecheza kabla ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC, nyavu za Simba zimetikiswa mara 13 ikiwa ni sawa na wastani wa mabao 2.6 kwa kila mchezo.

Safu hiyo ya ulinzi Simba iliruhusu mabao 10 katika mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita na Al Ahly, na kwenye mashindano ya SportPesa ilifungwa mabao matatu kwenye mechi tatu dhidi ya timu za AFC Leopards, Bandari FC na Mbao FC.

Kocha wa Mbao FC, Ally Bushiri alisema Simba inaruhusu idadi kubwa ya mabao kutokana na kukosa umakini.

"Simba huwa hawako makini pindi wanapokuwa na mpira lakini pale wanapoupoteza hawapambani kuutafuta na kuupora kutoka kwa wapinzani sasa wanapokutana na timu zinazojua kuuchezea mpira, inajikuta ikifungwa mabao mara kwa mara," alisema Bushiri.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema safu ya ulinzi ya Simba imekuwa haina mawasiliano mazuri.

"Ukiangalia aina ya mabao wanayofungwa ni matokeo ya mabeki kukosa mawasiliano lakini pia wamekuwa wakifanya makosa binafsi sasa wanapokutana na timu za wachezaji wa daraja la juu, wanajikuta wanaadhibiwa kwa kila kosa wanalofanya," alisema Mayay.

Simba inaingia kwenye mchezo huo huku ikiwa haina presha kubwa kwa safu yake ya ushambuliaji ingawa haijapata bao katika mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya AS Vita na Ahly kutokana na rekodi nzuri ya kufumania nyavu waliyonayo pindi wanapocheza nyumbani hapa Tanzania.

Lakini kinyume na hilo, Simba haina presha kubwa na safu yake ya ushambuliaji ambayo pamoja na kutofanya vizuri ugenini, imekuwa na rekodi inayovutia pindi wanapocheza uwanja wa Taifa.

Katika mechi tano za mwisho za mashindano ya kimataifa ambayo imecheza jijini Dar es Salaam, safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga jumla ya mabao 16.

Hata hivyo idara ya ulinzi ya Simba imeonekana kuyumba na kuvurunda mara kwa mara pasipo kuonyesha kuimarika jambo linalowapa faida wapinzani wao kufunga mabao ambayo yamekuwa yakiwagharimu