Jezi ya Kobe yatumika kuipa taji Lakers

Muktasari:

Fainali ya ligi ya kikapu Marekani-NBA inachezwa huko Disney World mjini Chicago, Florida, eneo maalum lililotumika kuchezwa kwa mechi zote za kumalizia msimu wa ligi hiyo.

 

BLACK Mamba. Ndilo jina lingine maarufu alilokuwa analitumia aliyekuwa nyota wa mpira wa kikapu Marekani kwenye ligi ya NBA, Kobe Bryant aliyecheza ligi hiyo kwa miaka 20 kuanzia mwaka 1996 hadi 2016.

Katika miaka yote hiyo, Kobe aliitumikia timu moja pekee ya Los Angeles Lakers, akifanikiwa kuchukua mataji matano ya NBA ambayo ni miaka ya 2000, 2001, 2002, 2009 na 2010 kabla ya kustaafu akiwa hapo mwaka 2016.

Ni bahati mbaya sana, wakati Los Angeles Lakers ikiwa inacheza fainali ya NBA msimu huu dhidi ya Miami Heat, Kobe hajabahatika kuiona timu hiyo ikichuana kwenye fainali hii kwani mapema mwaka huu alifariki dunia kwa ajali ya Helkopta akiwa na binti yake Gianna na watu wengine saba.

 Hata hivyo, Kobe au ‘Mamba’ hajasahaulika, kwani Los Angeles Lakers kwenye mchezo wa pili wa fainali kati ya mechi nne zilizochezwa, timu hiyo ilivaa jezi maalum zenye ‘stika’ za jina la Mamba ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuendelea kumuenzi na walishinda mchezo huo.

 Kizuri kuhusu jezi hizo, ni kwamba Lakers wanaaminika wakivaa jezi hizo huwa wanapata nguvu kubwa ya kushinda mchezo husika, kutokana na umuhimu wa mchezo unaofuata wa tano kati ya saba inayotakiwa, Lakers wameamua kuvaa tena jezi zenye stika ya Mamba.

 Awali jezi hizo zilipangwa kuvaliwa kwenye michezo miwili tu ya fainali hiyo inayoendelea, ambao ni ule wa pili na ule wa saba, lakini uamuzi mpya wa kushtua umefanywa na uongozi wa timu na watavalia jezi hiyo kwenye mchezo wa kesho Jumamosi alfajiri.

 Lakers inayoongozwa na LeBron James pamoja na Anthony Davis, kupitia imani ya jezi hizo, endapo watashinda mchezo wa tano kesho, watakuwa wamehalalisha kubeba taji la 17 la NBA ambalo mara ya mwisho walibeba mwaka 2010 wakiongozwa na Kobe.