Jeuri ya pesa Simba yamleta pacha wa Kagere

Muktasari:

Kisinda mwenye urefu wa Sentimeta 188, alikuja alikuwa kwenye kikosi ambacho Simba ilifumuliwa mabao 5-0 mjini Kinshasa, DR Congo pia katika mechi ya marudiano iliyochezwa Dar na Simba kushinda mabao 2-1 na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na Aussems.

MABOSI wa Simba wamempotezea Kocha Patrick Aussems kwa kauli zake wakati akitimka kurudi kwao, lakini wakaifanyia kazi ripoti aliyoiacha kocha huyo juu ya kutaka kuongeza straika mmoja wa kumsaidia Meddie Kagere na mezani mwao kuna majina mawili akiwamo winga wa AS Vita.

Winga huyo anayemudu pia kucheza kama straika ni Mkongomani Rossein Tuisila Kisinda ambaye ndiye anayepigiwa hesabu zaidi na mabosi wao ili kumvuta Msimbazi, jina lingine likiwa la straika mmoja matata kutoka KCCA ya Uganda.

Habari kutoka ndani ya Simba, zimedokeza kulingana na timu yao ilivyo wamekubaliana kuongeza mshambuliaji mmoja tu dirisha dogo ili kuiongezea nguvu timu na kati ya wanaompigia hesabu ni winga huyo aliyezaliwa Desemba 20, 1999 akijiandaa kutimiza miaka 20.

‘’Hao ndio majina ya washambuliaji wawili waliopo mezani kwetu kwa sasa, tunaendelea kuwatathmini, lakini Tuisila ndiye tunayemtaka zaidi, ikishindikana kuna mwingine kutoka KCCA, ila inategemea jinsi kocha mkuu mpya atakavyotaka, kama atawakataa basi tutaangalia wengine.”

Kisinda mwenye urefu wa Sentimeta 188, alikuja alikuwa kwenye kikosi ambacho Simba ilifumuliwa mabao 5-0 mjini Kinshasa, DR Congo pia katika mechi ya marudiano iliyochezwa Dar na Simba kushinda mabao 2-1 na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na Aussems.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema kwa sasa wanawaza zaidi kumpaka kocha mpya na baada ya hapo ndio watawekeza nguvu usajili wa dirisha dogo ingawa tayari wana majina ya wachezaji, japo hawezi kuyataja kwa sasa.

Senzo alisema kwa tathmini waliyoifanya timu yao inaweza kuongeza mshambuliaji mmoja tu ili kuongeza nguvu kwani kuumia kwa John Bocco na kutokuwa sawa kwa Wilker Da Silva kumeonekana kutokuwa na makali zaidi katika eneo hilo na kazi zote akibebeshwa Kagere pekee.

‘’Hili la usajili kuhusu Kisinda na huyo mshambuliaji wa KCCA ya Uganda nadhani mpaka hapo kocha mpya atakapofika ndio utakuwa wakati sahihi wa kulifanya hili kwani haiwezekani kusajili mchezaji katika timu bila ya mapendekezo ya kocha mkuu.”

‘’Kuhusu mchakato wa kumsaka kocha mkuu nadhani bado unaendelea ila baada ya muda nadhani ambao tumekubalina na Bodi ya Wakurugenzi Simba nadhani tutaliweka wazi n kutangaza ambaye atakuja kuchukua nafasi ya Aussems kwani tupo katika hatua za mwisho katika hilo,’’ alisema.

AMPOTEZEA AUSSEMS

Katika hatua nyingine Senzo, alipoulizwa kauli na maandishi ya Aussems juu ya uongozi wao, alisema hakufanya jambo sahihi lakini kwa kuwa wameachana naye si wakati wa kumzungumzia.

Alieleza Aussems kama alidai katika wachezaji aliowataka dirisha kubwa ni Francis Kahata hilo si sahihi kwani waliopo wana uwezo wa kuitumikia timu.

“Ukimwondoa Kahata, wote waliosajiliwa kama Benno Kakolanya, Ibrahim Ajibu, Miraji Athumani, Deo Kanda na wengineo wana uwezo ila hawajapata muda wa kuitumikia timu. Pia uhuru aliowapa baadhi yao uliwafanya washuke kiwango.”

“Tukipata kocha mpya tutamweleza hilo ili awabane wazembe, pia kutoa nafasi kwa wengine.”

Juu ya Wabrazil alisema Tairone Santos, Wilker Da Silva na Gerson Fraga ni wazuri na kuna mchezaji aliyecheza na Tairone, anayekipiga Mamelodi Sundowns alimweleza jamaa ni bonge la beki ila hajapata muda wa kutosha wa kucheza.

“Hata nilipozungumza na Tairone aliniambia alikuwa anakosa muda wa kucheza ndio maana anashindwa kuonyesha kiwango ila akipata muda wa kutosha ataonesha kiwango zaidi.”

“Nilipojaribu kuzungumza na Aussems alionekana kama kutowakubali wachezaji hawa jambo ambalo lilipelekea kutokuwa na maelewano kati yao lakini kwetu tunaamini ni wachezaji wazuri na bora ambao tunao katika timu,’’ alisisitiza.

Wakati huo huo Seleman Matola aliyetua rasmi Simba akitokea Polisi Tanzaia anatarajia kusaini kesho mkataba wa miaka mitatu. Senzo alisema Matola huenda akasaini mkataba huo, lakini kinachotakiwa ni muda mwafaka ili jambo hili liweze kutangazwa na kuanza kuitumikia Simba ambao wamepnga kuwa na benchi la ufundi imara.

“Jambo kama hili la heri wala halina wasi wasi kwani linaweza kukamilika muda wowote kutokana tumefikia katika hatua nzuri y kulikmilisha,” alisema Senzo.