Jeshi lamzuia kipa Yanga

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Prisons, Havintishi Abdalah, amekiri kukwama kwa dili hilo akisema kwamba, Kalambo amekataa kuihama klabu hiyo kwa sasa kutokana na kuwa kwenye kipindi kigumu huku ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

MABOSI wa Yanga wamekuwa wakienda resi kwa ajili ya kuhakikisha siku chache zilizosalia kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Jumamosi wanafanikiwa kuingiza mashine kadhaa mpya klabuni kwao, lakini juzi kati wamekutana na kigingi cha jeshi.

Ndio. Yanga ilikuwa ikipiga hesabu za kumnasa kipa Aaron Kalambo kutoka Prisons Mbeya ili atue Jangwani kuchukua nafasi ya Beno Kakolanya anayewadengulia kwa muda sasa, akiwa pia ameiandikia klabu hiyo barua ya kutaka kuachwa asepe zake.

Lakini, katika harakati zao hizo ghafla walijikuta wakiwekewa kigingi kwa jeshi hilo la Magereza kumzuia kipa huyo kutimka klabu kwao kwenda Yanga kwa madai wana hali mbaya na Kalambo ndiye anayeonekana kama roho yao kwa sasa.

Prisons imegoma kabisa kumruhusu kipa huyo kutua Jangwani na taarifa zinasema sababu kubwa ya Prisons kuchomoa kumuuza Kalambo ni umuhimu wa mchezaji husika ambaye amekuwa akiwasaidia kuondoka katika mkia wa msimamo wa ligi.

Wanajeshi hao wanataka Kalambo abaki kuipigania klabu yao kurudi katika nafasi nzuri ambapo endapo watamuuza sasa wanaweza kuyumba zaidi katika eneo hilo.

“Walikuja Yanga wanamtaka Kalambo nafikiri wanahitaji mtu wa kuchukua nafasi ya Beno (Kakolanya) ila tumeshindwa kukubaliana,” alisema mmoja wa viongozi wa timu hiyo ya jeshi la Magereza, ambayo msimu huu imekuwa ikichechemea katika ligi.

“Hatuwezi kukaa mezani kwa sasa na Yanga kumuuza Aron unajua shida tupo katika nafasi mbaya katika ligi na kipa huyu ndiye roho ya timu yetu kwasasa tukimuuza ina maana tunazidi kujichimbia shimo.”

Katibu Mkuu wa Prisons, Havintishi Abdalah, amekiri kukwama kwa dili hilo akisema kwamba, Kalambo amekataa kuihama klabu hiyo kwa sasa kutokana na kuwa kwenye kipindi kigumu huku ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

“Aaron (Kalambo) amefanya uungwana kwa kutoondoka sasa kwa sababu timu haipo kwenye nafasi nzuri na bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Prisons,” alisema Abdalah.

SHIKALO MBIONI

Lakini hali ikiwa hivyo, mabosi wa Yanga wameamua kutesti zali kwingine kwa kutaka kumleta Mkenya, Farouk Shikalo ili achukue nafasi hiyo ya Kakalonya.

Yanga iliyocheza mechi 15 na kushinda 13 ikikusanya alama 41 ikiwa kileleni inahaha kusaka kipa wa kumsaidia Ramadhani Kabwili aliyefungwa mabao matatu, akizidiwa moja na Nkinzi Kindoki aliyefungwa manne, huku Kakolanya akifungwa mawili tu. Katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawa iliamua kutua Bandari Kenya kutaka kumsajili Shikalo ambapo habari kutoka Kamati ya Usajili ya Yanga iliyopo chini ya Mwenyekiti wake Hussein Nyika zinasema Jangwani wameshamalizana na kipa huyo. Kigogo mmoja wa Yanga aliliambia Mwanaspoti wameshamaliza mazungumzo na kipa huyo na kinachosubiriwa ni kumpelekea mkataba na kusaini kabla ya dirisha dogo kufungwa Jumamosi wiki hii.

“Anachosubiri ni mkataba tu kutoka kwetu na tutaamua asaini hapa au tumfate kule kule kwao Kenya na kabla ya usajili kufungwa tutashusha vifaa vingine viwili vya maana,” alisema.

STRAIKA MWADUI

Mwanaspoti lilijikita zaidi katika kamati hiyo ya usajili ya Yanga na kupenyezewa jina lingine la mchezaji ambaye Kocha Mwinyi Zahera anamtaka, ni straika matata aliyeitesa Simba na Azam, Charles Ilanfya anayekipiga Mwadui.

Kocha Mwinyi Zahera alifichua kuwa mapema wiki hii hana mpango tena na Kakolanya kwa vile ameshindwa kumheshimu kama kocha wake, lakini kuhusu ujio wa kipa mpya alisema;

“Kama kocha, ndio nitakuwa na maamuzi ya mwisho katika nafasi yake kama nitaleta kipa mwingine au kuwatumia waliokuwepo.”

Naye Meneja wa Ilanfya, Majisafi Sharifu alisema amepokea ofa za timu tano zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zote zikihitaji huduma za mchezaji huyo na kuweka wazi kuwa makubaliano baina yao na klabu hizo ndio yataamua nani mwenye kisu kikali. Alisema ofa hizo ni za Yanga, JKT Tanzania, Coastal Union, Singida na KMC na kusisitiza;

“Ilanfya ni mchezaji mdogo ana miaka 21, hivyo maslahi hayaangaliwi sana kikubwa ni uhuru wa kumruhusu aweze kuendeleza kipaji chake.” alisema.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Mwadui, Ramadhan Kilao alisema hawana taarifa kutoka Yanga zikihusiana na kumtaka mchezaji huyo.

Imeandikwa na Charity  James na Thobias  Sebastian