Jeshi la Mexime lavamia kambi

Tuesday May 14 2019

 

By Saddam Sadick

MWANZA.MECKY Mexime na Kagera Sugar yake buana siyo watu wazuri. Wakimkamata Simba, wao wanachinja, wanafanya mishikaki, wanajilia tu. Wiki iliyopita walimpa kipigo kwa mara ya tatu mfululizo.

Sasa baada ya kumgeuza Simba kuwa ndafu ya sherehe, Mexime na jeshi lake anasema ile ilikuwa ni trela tu. Picha kamili litakuwa leo Jumanne watakapowavaa Stand United ‘Chama la Wana’ kwenye dimba la Kaitaba mjini Bukoba.

Kamanda wa kikosi, Mexime anasema wamedhamiria kuchukua pointi tatu zote dhidi ya United leo, ili ziwe chachandu ya kusherehekea kuwa timu pekee iliyozoa zile pointi zote sita msimu huu kutoka kwa vinara na mabingwa watetezi, Simba.

Kagera Sugar imekusanya pointi 43 na kukaa nafasi ya 10, huku Stand United wakiwa na alama 41 kwenye nafasi ya 14 baada ya mechi 35 kila moja.

Maxime alisema kwa kuwa bado hawajajihakikishia kubaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao, watahakikisha wanalivuruga ‘Chama la Wana’ leo ili kujiweka pazuri.

“Matokeo ya mechi iliyopita hatuyakumbuki tena, kwa sasa tunafikiria zaidi mchezo unaofuata, tunajua ushindani utakuwa mkali lakini tutapambana kuendeleza ushindi,” alisema Maxime.

Kwa upande wake Straika wa Stand United, Jacob Masawe alisema wanaenda kupambana kusaka matokeo mazuri ambayo yatawaweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

“Mchezo utakuwa mgumu ukizingatia timu zote zinataka ushindi lakini tumetoka sare mbili mfululizo, kwahiyo tunakwenda ugenini kubadili matokeo ya mchezo ili kuweka mambo sawa,” alisema Nyota.

Advertisement