Jeshi la Ferguson, lililogeukia ukocha

Wednesday March 13 2019

 

By Fadhili Athumani

Februari 05, Feyenoord ya Uholanzi ilimtangaza mmoja ya wanafunzi wa aliyekuwa Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, beki wa zamani wa klabu hiyo, Jaap Stam kuwa kocha wake.

Huo ni mwendelezo tu wa orodha ya wanafunzi wengi wa Ferguson ambao baada ya kulielewa somo lake, wamejitoa na wao kupeleka ujuzi wa soka kwenye klabu kadhaa huku wengine wakiwa makocha kamili na wengine wakiwa wasaidizi.

Hii hapa orodha ya wanafunzi wa Ferguson, ambao waliibuka makocha.

OLE GUNNAR SOLSKJAER

Juzi tu ametoka kufanya makubwa na sasa mabosi wa Man United wanafikiria kumpa kazi ya kudumu kukinoa kikosi hicho.

Tangu achukue mikoba ya Jose Mourinho (Desemba 19, 2018), kama kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer, ameiongoza United kushinda mechi 14 kati ya 17 mpaka sasa na kupoteza miwili tu. Kutokana na hali ilivyo, pamoja na shinikizo la wachezaji, mashabiki na wachezaji wa zamani wa United, pamoja na Fergie mwenyewe, ambaye ameonyesha kufurahishwa na mafanikio ya Ole, huenda Mnorway huyo, akatangazwa kuwa kocha wa kudumu.

BRYAN ROBSON

Ni mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kunolewa na Ferguson. Hata hivyo, hajafanya vizuri sana kwenye kazi ya ukocha kama alivyokuwa enzi zake za uchezaji.

Alianzia Middlesbrough, kabla ya kutimuliwa na kuibukia Bradford City, West Brom na Sheffield United na huko alifanya kazi nzuri si haba.

Aliisaidia West Brom kuepuka kushuka daraja, msimu wa 2005-06. Pia aliwahi kuifundisha Thailand kati ya mwaka 2009 na 2011.

PAUL INCE

Baada ya kuhudumu kama Kocha-mchezaji wa Swindon Town, Mwaka 2006, Ince alifanya maajabu ya kuiokoa Macclesfield Town na adha ya kushuka daraja. Kitendo hicho, kiliwavutia MK Dons, ambao walimpa kazi ya kuongoza jahazi lao.

Akawasaidia kutwaa ubingwa wa Kombe la ligi (Football League Trophy) na ubingwa ligi daraja la pili, England. Baadae alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Blackburn Rovers, aliyoifundisha kwa miezi sita tu. Pia amezifundisha Notts County na Blackpool.

STEVE BRUCE

Amejijengea heshima huko Ligi Daraja la Kwanza. Kila timu anayopewa anapata mafanikio. Hivi sasa anaiongoza Sheffield Wednesday na mpaka sasa amecheza mechi saba bila kufungwa na kikosi hicho. Rekodi yake inaonyesha alizipandisha daraja, Birmingham City na Hull City. Kama hiyo haitoshi, akiwa Wigan Athletic na Sunderland, Bruce alifanya kazi nzuri, japo hakuwa na mafanikio ya kuridhisha Aston Villa.

MARK HUGHES

Kocha wa zamani wa Wales, alihakikisha Blackburn Rovers, inapata nafasi ya kudumu, kwenye chati za juu ya jedwali la EPL, alipohudumu klabuni hapo, mwanzoni mwa miaka ya 2000. Akawapeleka kwenye UEFA. Fowadi huyo wa zamani wa Man United, Barcelona na Chelsea, aliteuliwa kuinoa Man City, mwaka 2008, lakini akatimuliwa mwezi Desemba, mwaka uliofuata. Alijiunga na Fulham, akaisaidia kumaliza katika nafasi ya nane, kabla ya kuachia ngazi mwaka 2011.

GARY NEVILLE

Nahodha wa zamani wa United, Gary Neville (43), aliacha kazi nzuri ya utangazaji, mapema mwezi Desemba 2015 na kuhamia katika kazi ya ukocha. Akakabidhiwa mikoba ya kuinoa Valencia lakini kilichomtokea huko, kila mtu anakifahamu. Alitimuliwa mwezi machi mwaka uliofuata, baada ya kuandikisha ushindi mara 10, katika mechi 28 za mashindano yote na kwa sasa amerejea kwenye kazi yake ya uchambuzi.

Gary, Lim, Phil Neville, Scholes, Ryan Giggs, Nicky Butt na David Beckham, wanahusishwa na Salford City.

ROY KEANE

Roy Keane, ambaye alikuwa nahodha wa United, wakashinda mataji 17, aliteuliwa kuinoa Sunderland, mara baada ya kutundika daruga mwaka 2006. Aliikuta ikiwa ya 23, kwenye jedwali la daraja la kwanza, akaipandisha daraja.

Akahamia Ipswich Town. Walikuwa hawajaonja ushindi katika mechi 14, za mwanzo za EPL (2009-10). Baadae akawa kocha msaidizi wa Jamhuri ya Ireland. Kwa sasa, ni msaidizi wa Martin O’Neill, pale Nottingham Forest.

RYAN GIGGS

Mwaka 2014, David Moyes alipofukuzwa kazi, wengi waliamini mtu sahihi wa kuchukua kijiti cha ukocha ni Ryan Giggs. Walimwona kama mrithi sahihi wa Ferguson. Aliteuliwa kuongoza jahazi kama kocha wa muda.

Akaiongoza United kushinda mechi mbili, sare moja na akafungwa mechi moja, kabla bodi ya United haijaona inafaa kazi hiyo, akapewa Mkongwe Louis van Gaal. Akasalia kama kocha msaidizi.

Baada ya Van Gaal, ikaaminika angepewa kazi, lakini Bodi iliamua tofauti na mikoba alikabidhiwa mbwatukaji, Jose Mourinho (2016). Giggs, alichosha kusubiri, akaamua kuondoka Old Trafford, ambapo kwa sasa ni Kocha wa timu ya taifa ya Wales.

PAUL SCHOLES

Ni chini ya mwezi mmoja, tangu Paul Scholes alipoteuliwa kuchukua mikoba ya ukocha pale Oldham Athletic. Lakini bila kupepesa, ashakum sio matusi, kazi hii ni kama inamlea Scholes, ambaye ni mmoja wa viungo hatari kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka.

Licha ya kushinda mechi ya kwanza nyumbani, dhidi ya Yeovil Town, wakitoa kichapo cha 4-1, Latics, wamefanikiw akupata pointi mbili tu, katika mechi nne za hivi karibuni na hivi sasa wako katika nafasi wa 13, kwenye msimamo.

Advertisement