Jeshi Stars, JKT Mbweni waanza kung'ara Muungano

Muktasari:

Mabingwa watetezi wa mashindano hayo, JKU ilianza vibaya kwa kulala kwa magoli 32-36 mbele ya Jeshi Stars huku jana Jumatatu ikiwa zamu ya JKT Mbweni kuonesha ubabe wake baada ya kuilaza JKT Makutupora kwa magoli 50-44.

Dar es Salaam. Timu ya Jeshi Stars na JKT Mbweni zimeanza vyema Mashindano ya Kombe la Muungano yaliyoanza Juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Gymkhana Unguja kwa kushirikisha timu 11 kutoka Bara na Visiwani.

Mabingwa watetezi wa mashindano hayo, JKU ilianza vibaya kwa kulala kwa magoli 32-36 mbele ya Jeshi Stars huku jana Jumatatu ikiwa zamu ya JKT Mbweni kuonesha ubabe wake baada ya kuilaza JKT Makutupora kwa magoli 50-44.

Kocha wa JKT Mbweni, Argentina Daudi alisema baada ya kuupoteza ubingwa msimu uliopita kwa kufungwa na JKU kwenye mchezo wa fainali, sasa wamerejea kwa kasi mpya kuhakikisha wanabeba ubingwa.

"Mchezo ulikuwa mgumu tangu mzunguko wa kwanza, lakini vijana wangu walijitahidi kupigana ili kulinda heshima yetu kwenye mchezo huu na mwisho tuliweza kufanikiwa kuibuka na ushindi, japo timu zinaonekana kujiandaa vizuri kutokana na timu kuongezeka na kila mmoja inahitaji kuonyesha uwezo wake," alisema kocha huyo.

Aliongeza moto huo wataendeleza kwenye michezo inayofuata na kuzidi kuwatahadharisha wapinzani wao wajiandae kupokea vichapo kwani baada ya ushindi huo, leo Jumanne JTK Mbweni itashuka uwanjani kuvaana na Zimamoto.

Kocha huyo alisema baada ya kutoka Zanzibar wachezaji wake watakuwa katika maandalizi makali ya kujiandaa na Mashindano ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Uganda mwezi wa tatu mwaka ujao.

JKT Mbweni ipo Kundi B' pamoja na Mafunzo, Zimamoto zote za Zanzibar, Tamisemi, Eagles na JKT Makutupora za Tanzania Bara, wakati Kundi A likiundwa na timu tano ambazo ni JKU, Afya, na KVZ za Zanzibar huku Jeshi Stars na Jiji Arusha iliyocheza jana Jumatatu jioni dhidi ya KVZ zikiwa zinatoka Tanzania Bara.

Meneja wa timu ya Arusha Jiji, Nicholaus Malima alisema kikosi chao kinaelea vizuri tangu kilipowasili visiwani humo wiki iliyopita ikiwa chini ya Kocha, Nurdin Hassan na wamejiandaa kwenda kufanya vizuri ili kubeba ubingwa huo.

Mbali na JKT Mbweni kucheza na Zimamoto leo, michezo mingine Jeshi Stars itacheza na Afya,  JKT Makutupora na Tamisemi, Mafunzo akivaana na Eagles,  huku Arusha Jiji akicheza na JKU.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Dk Devota John alisema wachezaji wanapaswa kucheza kwa malengo kwani mchezo wa netiboli kwa sasa unatoa wachezaji wengi wanaokwenda kucheza barani ulaya na kulipwa fedha nyingi.

"Mchezo wa Netiboli ndio mchezo pekee kwa sasa ambao unashirikisha pande mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo ukichezwa kwa upendo na mshikamano tutazidi kuudumisha Muungano wetu."