Jella aipa mchongo Taifa Stars kuitikisa Afcon

Thursday May 23 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Nahodha wa Taifa Stars iliyoshiriki Fainali za Afrika (Afcon) mwaka 1980, Jellah Mtagwa amewataka nyota wa sasa wa Stars kujituma, kuwa na umoja na kujitoa kwa Taifa ili wafanye vizuri kwenye fainali za mwaka huu.

Jellah aliyekuwa nahodha wa Stars kwa miaka 10 tangu 1974 alibainisha hayo katika mahojiano ya hivi karibuni, nyumbani kwake Dar es Salaam.

Alisema nafasi ambayo Stars imeipata nafasi nyeti katika soka la Afrika, hivyo wachezaji wasifikirie watapata nini kwenye hayo mashindano, bali wafikirie Taifa litakuwa katika hali gani watakaposhinda.

"Wakati wetu tulijitoa sana, wachezaji kila mmoja alionyesha uchu wa kutaka mafanikio, hatukuwaza malipo, tulitaka heshima.

"Hata tulipofungwa kwenye Afcon, matokeo haya kutuumiza mno, sababu tulicheza na wenyeji Nigeria wakatufunga 3-1, Ivory Coast tukatoka nao sare na Misri wakatufunga, lakini mpira tulicheza," anasema.

Beki huyo tegemeo wa zamani wa Starsm Pan African na Yanga alisema mashindano ya Afrika ni mashindano magumu, ambayo yanahitaji umakini, uwezo na kujituma ili kufanya vizuri.

Advertisement

"Ni mashindano magumu na timu za kundi letu ni ngumu, Stars wanapaswa kugangamala haswa ili wasije kuishia hatua ya makundi au kuwa timu itakayofungwa mabao mengi," alisema Jella.

Alisema wasiwasi wake ni kuchelewa kuanza maandalizi kwa Stars mpaka sasa kwani kipindi hiki timu ilipaswa kuanza mazoezi ya pamoja.

"Wanahitaji kucheza mechi nyingi za kirafiki, lakini pia kufanya mazoezi ya pamoja kwa muda kidogo, kipindi hiki ilipaswa Ligi yetu iwe imekwisha na timu imeanza kujiandaa kwa Afcon," alisema Jella.

 

Advertisement