Javu, Bigirimana Blaise wampa kiburi kocha

Tuesday January 8 2019

 

By Masoud Masasi

Mwanza.HUKO Alliance FC kwa sasa ni raha kwa kwenda mbele, hadi Kocha Mkuu wao, Malale Hamsini kukiri ana kiburi cha kuamini atairejesha kwenye heshima timu hiyo kutokana na kasi waliyoanza nao nyota wake wawili wapya, Hussein Javu na Bigirimana Blaise.

Nyota hao wametengeneza pacha matata ya ushambuliaji ikiwa ni muda mfupi tu tangu watue, Javu akitokea Mtibwa Sugar na Bigirimana akitokea Stand United na kumfanya Hamsini kuzuga eti bado hajaridhika na moto wao, akidai wana vitu adimu.

Javu na mwenzake walisajiliwa dirisha dogo na muunganiko wao umeifanya timu hiyo kuonekana moto katika siku za karibuni tofauti na ilivyoanza msimu kwa kuburuza mkia kwa muda mrefu.

Tayari Javu amefunga mabao wawili, huku Bigirimana akitupia moja katika mechi mbili walizocheza na Kocha Hamsini alisema licha ya nyota hao kufanya vizuri lakini bado hajaridhishwa na kile wakifanyacho akitaka wawe makini zaidi katika kutupia nyavuni.

Kocha huyo alisema hakukurupuka kufanya usajili ndio maana aliwaleta washambuliaji hao baada ya kubaini wanafanana aina ya uchezaji wao ambao aliona watasaidia sana kwenye Ligi Kuu.

“Bado Sijaona kile kiwango ambacho mimi nakitaka pamoja na kufanya vizuri lakini nataka wawe bora sana unajua niliwasajili baada ya kugundua wanafanana aina ya uchezaji ambao niliona wakicheza kama pacha watanisaidia sana”alisema Hamsini.

Alisema ataendelea kuwanoa zaidi washambuliaji hao ambao amesema anataka kuwaona kila mechi wanafunga mabao ya kutosha ambayo yatawasaidia kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA.

Advertisement