Jangwani ishu ni posho tu

Muktasari:

Yanga haina fedha na imekuwa ikibezwa na mashabiki wa Simba kuwa ombaomba, lakini ni moja ya klabu yenye matokeo mazuri kuliko Simba inayotambia mkwanja wa bilionea, Mohammed 'MO' Dewji.

SIMBA imepata sare ambayo hawakuitegemea juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kiasi kila shabiki wa klabu hityo ameshindwa kuelewa jinsi mabao yalivyokoswa, lakini Jangwani imefichuka siri ya mafanikio ya klabu ya Yanga.
Yanga haina fedha na imekuwa ikibezwa na mashabiki wa Simba kuwa ombaomba, lakini ni moja ya klabu yenye matokeo mazuri kuliko Simba inayotambia mkwanja wa bilionea, Mohammed 'MO' Dewji.
Beki kiongozi wa klabu hiyo, Andrew Vincent 'Dante' amefichua siri ya klabu yao kutopbagua uwanja wa kuzinyoosha timu pinzani katika lindi hilo la ukata mkali.
Dante aliliambia Mwanaspoti kuwa hesabu zao kubwa ni kukimbizana na Simba na wengine wanaowatishia kuchukua taji, lakini wao kama wachezaji pia wana akili tofauti kabisa na wanavyofikiria mashabiki wa soka nchini.
Alisema katika timu yao wanajua kwamba hali ya fedha sio nzuri na wanadai mishahara kwa muda mrefu, lakini hilo haliwezi kuwafanya kupoteza mechi zao.
Beki huyo mbishi alisema katika vikao vyao kama wachezaji walichokubaliana ni kwamba kama wakipambana na kushinda watakuwa wamevuna mambo mawili kwa wakati mmoja kwa kupata ushindi lakini pia kupata fedha.
Alisema fedha ambazo wanazivuna ni kupitia posho zao za ushindi kila mechi ambazo zinawasaidia kupunguza makali ya maisha yao huku pia ushindi ukipatikana na kujiimarisha katika ligi.
"Tukiwa kama wachezaji tunajua kwamba kila tunaposhinda tunapata pointi tatu, lakioni pia ndani ya pointi hizo pia tunajihakikishia posho za ushindi ambazo zinatusaidia sasa," alisema.
Aliongeza kuwa, wanajua kwamba uongozi wao hauwezi kuwadhulumu haki yao ya mishahara yao na kwamba hali ikikaa sawa watalipwa lakini wakipoteza ushindi hawataweza kuzipata pointi zilizopotea.
"Hali ya fedha katika klabu yetu hilo linajulikana haiko sawa lakini sio kwamba eti hela hakuna kwa maana ya mishahara alafu huku nyuma timu ifungwe," alisema.
"Tukifungwa hatupati posho lakini pia tunapoteza pointi ndiyo maana mnaona tunaweka nguvu kubwa katika kila mchezo,unaweza kuja kulipwa mishahara lakini kama ulipoteza pointi haziwezi kurudi tena.
"Uongozi unajua kuwa tunadai na hatujawahi kudhulumiwa mambo yakikaa sawa tutalipwa tu hakuna namna muhimu tupate mafanikio kwa timu kupata mafanikio lakini pia sisi kama wachezaji tukionekana uwanjani ndiyo tunajiweka sokoni."