Jamani huyu Wawa hatanii!

Muktasari:

Wawa alisema mwanzoni wakati anakuja nchini alikuwa akionekana kama mchezaji wa kawaida, ambaye umri wake umekwenda lakini baada ya kuanza kukitumikia kikosi cha Simba maneno yote yamepotea.

BEKI kisiki wa Simba, Pascal Wawa amesema kama kuna straika wa timu ya Ligi Kuu Bara, ambaye anahisi anaweza kumtisha wanapokutana, basi humpangia mikakati mapema kabisa.

Wawa alisema mwanzoni wakati anakuja nchini alikuwa akionekana kama mchezaji wa kawaida, ambaye umri wake umekwenda lakini baada ya kuanza kukitumikia kikosi cha Simba maneno yote yamepotea.

“Nimecheza soka la ushindani zaidi ya miaka 10, wakati natua hapa kujiunga na Simba nilisikia maneno nimezeeka, lakini kazi yangu imefuta kabisa hayo maneno ambayo sikuwa nayasikiliza.

“Kabla ya kuanza kucheza soka nimekaa darasani na kufundishwa jinsi ya kukabiliana na changamoto uwanjani na hilo limenisaidia sidhani ni wachezaji wangapi ambao kabla ya kucheza soka walikwenda shule,” alisema.

“Huwa natenga muda kuwafuatilia washambuliaji wa timu pinzani kama hawa wa AS Vita ambao wanashambulia kwa haraka na nimewafanyia maandalizi na tutapambana nao na kuwadhibiti,” alisema Wawa.