Jamani Yanga majanga

Muktasari:

Yanga hadi sasa ina majeruhi sita wote ni wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao ni Juma Abdul, Juma Mahadh, Haji Mwinyi, Mohamed Issa ‘Banka’ na Andrew Vincent ‘Dante’ huku Abdallah Shaib ‘Ninja’ anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu mfululizo.

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila amesema wingi wa majeruhi kwenye kikosi chake unampa wakati mgumu hasa kipindi hiki wakijiandaa na mchezo muhimu wa kutafuta tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani. Yanga inayoendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo wa Kombe la FA utakaochezwa CCM Kirumba jijini Mwanza dhidi ya Alliance wiki ijayo.

Yanga hadi sasa ina majeruhi sita wote ni wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao ni Juma Abdul, Juma Mahadh, Haji Mwinyi, Mohamed Issa ‘Banka’ na Andrew Vincent ‘Dante’ huku Abdallah Shaib ‘Ninja’ anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu mfululizo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwandila alisema anatamani kuona nyota wake wote wanakuwa fiti kabla ya kukabiliana na Alliance na kuweka wazi kuwa hata Taifa Stars inamuharibia programu yake kwani anashindwa kukiandaa kikosi kamili huku akiombea nyota wake wasipate matatizo.

“Naamini baadhi ya nyota hao walio majeruhi wanaweza kuwahi mchezo lakini ni wazi Ninja tutaendelea kumkosa kutokana na kufungiwa michezo mitatu na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF). “Kwasasa programu yangu kubwa niliyonayo ni kuwafundisha mbinu za kucheza mpira tofauti, Alliance wao mpira wao ni wa pasi fupifupi na wana kasi hivyo kinachofanyika ni kukwepa hilo kwa kucheza mipira mirefu na kuwa na kasi kuzidi wao.

“Tumekutana na Alliance michezo miwili ya ligi yote wametuonyesha ushindani pamoja na kushinda lakini tulichezewa mpira mkubwa na kutupa ugumu kwani walitambua hilo, nimeanza mapema.”