Jamani! JKT hawalali kisa huyu Kagere

Muktasari:

Kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Bares’ alizungumzia maandalizi ya kikosi chake kwa msimu mpya, amesema alizitumia siku nane kuwanoa wachezaji wake na kuwapa pumzi.

KAMA ratiba ya Ligi Kuu Bara itabaki kama ilivyo basi, straika wa Simba Meddie Kagere, ajipange kwelikweli kuwakabili mabeki wa JKT Tanzania.

Simba na JKT ndio zitafungua dimba la msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na Kagere, ambaye yuko kwenye kasi kubwa ametamba kuanza msimu huu kwa kushindo.

Kipute cha ligi kitaanza rasmi Agosti 23, huku mechi za kimataifa za marudiano za Simba, Yanga, Azam FC na KMC zikiwa hazijapangiwa tarehe maalumu zikitajwa kupigwa kati ya Agosti 20 na 23, hilo linaweza kuwa sababu kwa baadhi ya mechi kusogezwa mbele.

Kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Bares’ alizungumzia maandalizi ya kikosi chake kwa msimu mpya, amesema alizitumia siku nane kuwanoa wachezaji wake na kuwapa pumzi.

Pia, alisema wakati akiendelea na maandalizi yake, aliwachungulia mastaa wa Simba wakati wa mechi yao ya kirafiki dhidi ya Power Dynamos kwenye Tamasha la Simba Day.

Bares alisema Kagere ni mchezaji hatari anayejua kutumia faulo, mbinu, nguvu, kasi na akilikufunga na hilo limewafanya mabeki wake kumfuatilia zaidi.

“Kikosi chote cha Simba ni kizuri, ila timu zinahitaji matokeo na ili tushinde lazima washambuliaji wetu wawe na kasi na makini uwanjani. Pia, lazima tuwazuie watu kama Kagere ili wasilete madhara katika lanmgo letu,” alisema.