JWTZ Mwenge Jazz yaja na video mbili, Bella kusindikiza uzinduzi

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi Digital, mratibu wa tamasha hilo, Selemani Semunyu amesema, Jumamosi ya wiki hii ni wakati wa kuzindua video zao mbili mpya ziitwazo Usiende Kombo na Heshima Yangu ,huku wakisindikizwa na mwanamuziki Christian Bella akiwa na Malaika Bendi pamoja na Bendi ya JKT Kimbunga.

Video ya 'Usiende Kombo' na 'Heshima Yangu' ya Bendi Kongwe ya Muziki wa dansi JWTZ Mwenge Jazz zinatarajiwa kuzinduliwa Jumamosi ya Machi 23,2019 katika Ukumbi wa Club 361 Mwenge jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MCL Digital, mratibu wa tamasha hilo, Selemani Semunyu amesema, Jumamosi ya wiki hii ni wakati wa kuzindua video zao mbili mpya ziitwazo Usiende Kombo na Heshima Yangu ,huku wakisindikizwa na mwanamuziki Christian Bella akiwa na Malaika Bendi pamoja na Bendi ya JKT Kimbunga.
Aidha Semunyu alisema kufuatia uzinduzi huo wamejipanga vizuri kwa kuanza na kazi hizo ambazo zimeshakamilika chini ya waimbaji wote wa JWTZ Mwenge Jazz na  amewataka wapenzi wa muziki nchini wazipokee kazi zao mpya za video zitakazozinduliwa siku hiyo.
Alisema  Semunyu kuna baadhi ya watu walisema bendi hiyo imepotea wao wakiwa hawajui nini kinachoendelea hivyo wamewaletea vitu vipya na vitamu na  video hizo zitaanza kuonekana kwenye vituo mbalimbali vya televisheni nchini kote, wakati wowote kuanzia siku hiyo.
"Sisi tumekuja kazini nia yetu ni kuleta burudani japo kuna baadhi ya watu walikuwa wanasema kama JWTZ Mwenge Jazz imepotea na wengine kusema imepoteza muelekeo kwa kile hatuonekani nje ya jukwaa,wajue tu bendi ipo na inaendelea kutumbuiza ndani jeshi na sio kwenye kumbi nje ya jeshi.
Wanamuziki baadhi wa JWTZ Mwenge Jazz ni Shukuru Majaliwa, Hussein Mtamile, Salum Dialo   Profesa  Ibrahimu Kandaya, Shabani Dimoso, Charles Chitopela, Leah Lyeme, Nica Luchele, Emmanuel Mahuwile hawa ni waimbaji wakongwe.

Semunyu amesema lengo la bendi kuanzishwa ni kuwaburudisha maafisa wa jeshi na maaskari na sio kupiga shoo kwenye kumbi za nje ya jeshi  kama zamani.
Bendi wameamua kuwa na wamamuziki vijana ambao watatambulishwa siku hiyo.

Hivyo kila mara wanaleta kizazi kipya na wanafanya hivyo kuendana na soko la sasa la vijana kwenye muziki wa dansi, pia wale wazee wanakuwepo katika bendi kwani wanamashabiki zao pia.