JULIO: Morrison? Mbona ningemnyoosha

Nyota wa zamani wa kimataifa ambaye kwa sasa ni kocha, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amefunguka namna maisha yake ya soka alivyoanza ikiwemo kuibukia Simba ambao baadaye walimtosa kwa madai ya usaliti. Pia, amekumbushia tukio lake la kummdhibiti straika wa zamani wa SC Villa ya Uganda, Majid Musisi kiasi cha kubatizwa jina la Mrema.

Julio pia alieleza namna kifo cha Hussein Tindwa uwanjani kwenye mechi ya kimataifa dhidi ya Rocca Rover ys Nigeria mwaka 1978, kilivyoshindwa kumtoka mpaka leo, likiwa ndio tukio linalomhuzunisha, huku akifichua usajili wake wa Pilsner ulivyobadilisha maisha yake.

Leo Julio, mwenye maneno mengi anafichua namna alivyojipeleka Taifa Stars na kuweka bayana kama angekuwa Kocha wa Bernard Morrison, asingemchekea na utukutu wake anaouonyesha ndani ya Yanga. Kivipi? Endelea naye kuhitimisha mahojiano maalum na Mwanaspoti.

AJIPELEKA MWENYEWE STARS

Ni nadra kwa mchezaji kujipeleka timu ya taifa, lakini Julio aliwahi kufanya kwa kupata ujasiri wa kwenda kwenye kambi ya Taifa Stars bila kujali atachukuliwaje na kocha wa timu hiyo.

Julio anafichua hakuwa ameitwa kwenye kikosi cha Stars ya Kocha Abdallah Kibadeni na Hafidh Badru, lakini akaamua kwenda mwenyewe kwa kuamini huenda hawakumuona vizuri kwenye mechi za klabu yake.

“Nilibeba viatu vyangu nikajipeleka kambi ya Stars, sikuona aibu nilipofika nikaulizwa hujui hii ni timu gani na ina mipaka yake? Nilichokifanya nikawajibu mlinisahau. Huwezi amini makocha hao waliniunganisha kwenye mazoezi hayo na nilifanya kitu cha tofauti kilichonibeba,” anasema Julio.

“Nilifanya mazoezi na kuwaongoza wenzangu kwenye kupasha mwili joto, kitendo kilichomkuna aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka (FAT) Yunus Abdallah na kuuliza kwani mi ni nani? Akajibiwa ni Julio akafurahia na huwezi amini niliteuliwa kuwa nahodha wa kuongoza wenzangu kupitia mazoezi yale,” anaongeza Julio huku akicheka.

AMTAJA MOGELLA TU

Julio anakiri wakati anacheza soka kulikuwa na mastraika wakali waliokuwa wasumbufu ukiachana na Musisi, lakini anadai aliyekuwa akimnyima raha ni Zamoyoni Mogella, huku akitamba kuwa ngome alizokuwa nazo kipindi hicho ilikuwa matata na ilimrahisishia kazi kuwazuia mastraika.

Anasema kuanzia Pilsner, alikuwa akicheza kama beki wa mwisho na kuwaachia msala wenzake aliokuwa anacheza nao eneo hilo akiwemo Rajabu Rashid na James Washokera.

Kwa Simba Julio alicheza sambamba na Frank Kasanga na Method Mogella na kuwepo kwa wenzake mbele kulimrahisishia kazi kusafisha hatari zote.

“Nilikuwa na kazi nyepesi sana wakati ule kwanza kipa ilikuwa ukimrudishia mpira kwa mguu anaudaka tofauti na sasa ni kwa kichwa tu na kucheza nyuma ya mabeki wawili ilinipunguzia kazi ndio maana hakuna straika aliyenitisha, ingawa kwa kweli Mogella alikuwa balaa kipindi hicho.”

FAMILIA YA SIMBA NA YANGA

Julio ni kati ya wachezaji wachache wanaotoka familia ya wanasoka kwani kuanzia baba yao mpaka ndugu zake waligawana Simba na Yanga na kucheza soka kwa mafanikio kitu anachojivunia.

Katika familia yote kuanzia baba na mama hadi wao walitofautiana mapenzi ya kuzipenda Simba na Yanga, Mwanamtwa Kiwhelo ‘Dally Kimoko’ na baba yao walikuwa Yanga wakati yeye, Mussa, Mhesa na mama yao ni Simba lialia.

Kuhusu mechi za Simba dhidi ya Yanga zilipokuwa zinachezwa na ilipotokea timu mojawapo kushinda au kufungwa, Julio anafichua ilikuwa hakuna ugomvi badala yake ilikuwa ni kununiana na wanaotamba ndani ya nyumba ni walioshinda na kula chakula kwa mbwembwe.

SOKA ARABUNI

Julio anafunguka maisha yake ya soka yaliishia Arabuni alipokwenda kucheza soka la kulipwa kabla ya kurejea tena Msimbazi na kuichezea 1994 sambamba na Taifa Stars kabla ya kustaafu rasmi na kugeukia ukocha.

Anasema alianzia ukocha akiwa Mafunzo ya Zanzibar na kupata hamu ya kuwa kocha mkubwa zaidi kwa kwenda kusomea Brazil mwaka 1999 akiwa na klabu ya Kajumulo World Soccer kwa ngazi ya Diploma na baadaye kumalizia Uholanzi 2002-2003 chini ya ufadhili wa bosi wake, Alex Kajumulo.

“Nilipomaliza ndipo rasmi nikajiingiza kufundisha timu mbalimbali nchini ikiwemo ingia toka, ingia toka ndani ya Simba ambayo ikiwa na shida ndipo ilinikabidhi timu au kuwa kocha msaidizi kwa muda mrefu.”

KWANINI KIBADENI?

Ulishawahi kujiuliza swali, kila alipokuwa Simba basi ilikuwa kawaida kuwa na Abdallah Kibadeni? Julio alipoulizwa sababu ya uswahiba wake na Kibadeni anakiri, imechangiwa na mambo mengi lakini kubwa ni kule kumheshimu mno kocha huyo, lakini pia ni mtu anayeendana naye kiufundishaji.

Akifafanua zaidi, Julio anadai sababu kubwa za kuwa pamoja na Kibaden kama makocha akiwa msaidizi wake ilitokana na kukubaliana sera zao za ufundishaji kila mmoja akijulia ya mwenzake hivyo, kuwafanya wadumu bila kukwazana katika utekelezaji wa jukumu yao.

“Mimi na King tulikuwa tunajuliana na kuendana sera zetu za ufundishaji, sikuwa mbishi kwake kwenye maelekezo aliyonipatia wakati wote, kuendana huko ndipo kulipelekea tuwe pamoja na hata kukabidhiwa Simba kwa nyakati tofauti.”

Anasema kutaka kuthibitisha kuwa yeye na Kibadeni wanajuliana, anakumbushia ile mechi ya sare ya maajabu ya 3-3 dhidi ya Yanga waliotangulia kufunga mabao yao kwenye kipindi cha kwanza na wao kusawazisha walipotoka mapumziko.

“Katika maisha yangu yote ya ukocha ukiachana na mengi niliyoyafanya, hakuna linalozidi mchezo wetu dhidi ya Yanga mwaka 2013 tulipotoka nyuma kwa mabao matatu na kulazimisha sare ya 3-3. Mimi na Kibadeni tuliwatuliza vijana wakati wa mapumziko na kurudi uwanjani na nguvu kubwa.”

AJIVUNIA KINA NDEMLA

Julio ni kama amehusika katika kuwaendeleza vijana wengi wanaofanya vema kwa sasa ndani na nje ya Tanzania na kuwataja Farid Mussa, Mbwana Samatta, Miraji Adam, Abdalah Seseme, Jonas Mkude, Ibrahim Ajib, Said Ndemla, Bakary Mwamnyeto, Himid Mao, Mudathir Yahya na Simon Msuva aliyefichua alivyofanikisha hati yake ya kusafiria kwenda kucheza mechi za timu ya vijana dhidi ya Cameroon na Nigeria.

Mbali na kufanya kazi na Kibaden, Julio anajivunia pia kuifundisha timu hiyo kama kocha msaidizi chini ya makocha wa kigeni wengi walioifundisha timu hiyo kwa nyakati tofauti jambo ambalo kwake anaamini ni sababu nyingine iliyomuongezea ujuzi.

Makocha ambao waliifundisha timu hiyo huku benchi wakisaidiwa na Julio ni pamoja na Trott Moloto, Milovan Cirkovic, Zdravko Logarusic na Patrick Liewig aliofanya nao Simba.

NUSURA AWE KOCHA YANGA

Julio, ambaye anakiri anaipenda Simba kikwelikweli na licha ya madhira ya kuitwa na kutimuliwa bado hana kinyongo na kama watamuita atakwenda kuliamsha goma kama kawaida, lakini usichokijua ni kwamba alikaribia kuajiriwa kuinoa Yanga mwaka 2001.

Anasema Tarimba Abbas aliyekuwa bosi wa Yanga alishaandaa mkataba kabisa wa kazi, lakini Imani Madega na viongozi wengine walimkataa wakati klabu hiyo ikinolewa na Mmalawi Jack Chamangwana, ambaye kwa sasa ni marehemu.

Hata hivyo, anasema licha ya unazi wake wa Msimbazi, lakini yupo tayari kuifundisha Yanga endapo atatakiwa kufanya hivyo, kwani kazi ni kazi haina ushabiki.

Kocha huyo anayekumbukwa kuacha kazi Mwadui, timu aliyoipandisha Ligi Kuu anasema amefurahishwa na matokeo ya Simba kuitambia Yanga mabao 4-1 kwani kipigo cha 1-0 kwenye Ligi kiliwanyima raha, japo awali alipata ugumu kutabiri kutokana na mechi za watani zilivyo.

MORRISON MTATA

Julio anasema matukio anayofanya nyota wa Yanga, Morrison kama angekuwa yupo chini yake mbona angemkoma, kwani asingemchekea.

“Inashangaza sana, mchezaji aliyesajiliwa kutoka nje ya nchi kuja kucheza soka Tanzania akawa na kiburi na mambo ya hovyo kama anavyofanya huyu jamaa. Ningekuwa ndiye kocha wake na yale aliyofanya awali kabla ya Kariakoo Derby ya wiki iliyopita, ningemtosa kabisa kikosini,” anasema.

Morrison amekuwa akigomea safari na kufanya utukutu mwingi ikiwamo kususa kwenda kukaa benchi alipotolewa kwenye pambano la Kariakoo Derby la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na kutimka moja kwa moja mpaka leo akiwa hajaonekana kambini kwa madai mkataba wake na Yanga umemalizika.

KIKOSI BORA

Julio kama ilivyo baadhi ya wadau wanaofuatilia mechi za ligi msimu huu na amekuwa na chaguo la Kikosi Bora kwa msimu huu kwa kuwataja Aishi Manula, Shomary Kapombe, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Papy Tshishimbi, Francis Kahata, Claotus Chama, Kelvin Sabato na John Bocco.

Na kuhusu uteuzi wa sasa wa Taifa Stars, Julio alimpongeza kocha Etienne Ndayiragijie kwa juhudi zake za kufuatilia mechi za timu zote na kuchagua wachezaji wanaoonyesha viwango akidai ndivyo inavyotakiwa badala ya kuita kwa mazoea tu.

Julio anadai ushirikiano mzuri kutoka kwa uongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) chini ya Wallace Karia na Wilfred Kidao unamrahisishia kazi Ndayiragijie ndio sababu amefanikiwa kuipeleka Tanzania kwenye mashindano ya CHAN kwa mara ya pili baada ya awali kupelekwa na Marcio Maximo.

Juu ya makocha wazawa, Julio anasema lazima waheshimiwe kwani wana uwezo wa kufanya makubwa tu kama ilivyokuwa upande wa timu za vijana, huku upande wa klabu, akizitaka timu ziwaamini na sio kusubiri mambo yakiwa mabaya ndipo wanawakabidhi timu na inapotokea hali nzuri wanaachana nao.

WACHEZAJI WA KIGENI

Ukiachana na masuala mengine mengi ambayo ameyazungumzia Julio, kwenye upande wa wachezaji wa kigeni amekuwa kidogo na kusita kuhusu kupungua kwa idadi ya wachezaji 10 au kubaki ilivyo, lakini zaidi aliegemea upande wa kupungua angalau wachache huku akieleza kimkakati jinsi ya kuwapata wachezaji wa kuisaidia nchi kisoka.

“Nilishawashauri Karia na Kidau kuhusu kuendelea kwao na mipango endelevu waliyonayo ya kuvumbua zaidi vipaji vya vijana wadogo.

Nasisitiza zaidi kuwepo mikakati madhubuti ya kuwaandaa vijana wengi na kuwa na timu nzuri za vijana ambao kupata kwao nafasi na kucheza mashindano mbalimbali kutawainua na kutusaidia kama taifa siku zijazo” anafunguka Julio.

AIPA TANO DODOMA JIJI

Julio aliyewahi kuinoa Dodoma Mji kabla ya kuachana nao, anaimwagia sifa timu hiyo kwa kupanda Ligi Kuu Bara na pia kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza kwa kuifunga Gwambina.

Akiwa ameifundisha timu hiyo kwenye misimu miwili iliyopita, kabla ya kumalizana na mabosi wake na msimu huu ikachukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Julio anasema ni timu iliyostahili kupanda mapema kwa vile imejipanga, ila ndivyo hivyo tena soka la Bongo lilivyo.

Anasema kwa hamasa anayoiona kwa wapenzi na wana Dodoma kwa ujumla kuungana tofauti na misimu miwili iliyopita anaamini hata kwenye Ligi Kuu Bara itafanya maajabu mbele ya Simba, Yanga na Azam ambazo zimekuwa zikitawala soka la Bongo kwa muda mrefu.