JPM azishukia Simba, Yanga

Muktasari:

  • Dk Magufuli, ambaye jana alieleza furaha yake baada ya Taifa Stars kufuzu Fainali za Afcon, alisema tabia hizo zinachelewesha maendeleo ya soka nchini.

IMEFICHUKA kuwa Rais John Magufuli ni miongoni mwa wanaokerwa na ile zomeazomea na kusalitiana kwa mashabiki wa Simba na Yanga pindi mmoja anapocheza na timu za kigeni.

Jana wakati akizungumza na wachezaji na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), Dk Magufuli alisema anachukizwa na tabia hizo za mashabiki hao kushindwa kupeana sapoti pindi mmoja anapowakilisha Taifa.

Dk Magufuli, ambaye jana alieleza furaha yake baada ya Taifa Stars kufuzu Fainali za Afcon, alisema tabia hizo zinachelewesha maendeleo ya soka nchini.

“Inapocheza Simba inawakilisha taifa hivyo lazima wote tuishangilia kama Taifa, vivo hivyo inapocheza Yanga inawakilisha Taifa wote tunapaswa kuishangilia.

“Inawezekana haya nayo ndiyo mambo ambayo yanatuchelewesha na ndio sababu nilikuwa nawaza ni kwanini siku moja tusichukue timu moja ya jeshi ili tuondoe hii hali ya kila mmoja kusifia mchezaji wake anapoichezea Taifa Stars,” alisema Dk Magufuli, ambaye alitumia fursa hiyo kumkabidhi Makamu wa Rais, Samia Suluhu kuiangalia timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars ili ifanye vizuri.

Ampongeza Bondia Mwakinyo

Pia, Rais Magufuli alimpongea bondia, Hassan Mwakinyo baada ya kumchapa makonde Muagentina, Sergio Gonzalez wa Argentina kwenye pambano lililofanyika juzi jijini Nairobi, Kenya.

“Nampongeza Mwakinyo na sikutarajia kama ana mwili mdogo mdogo kama wangu, lakini kamtwanga yule jamaa hadi kainama chini. Kwa kweli inafurahisha sana,” alisema.