JKT Tanzania yazipeleka Simba, Yanga Mkwakwani

Muktasari:

  • JKT Tanzania ilizindua Uwanja wake wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo mwaka jana na sasa unafanyiwa ukarabati ikiwemo kuweka majukwaa yenye uwezo wa  kuchukua mashabiki 5000.

Dar es Salaam. Bodi ya Ligi Kuu Bara imekubali ombi la JKT Tanzania kutumia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa mechi zake za nyumbani itakazocheza dhidi ya Simba na Yanga.
JKT Tanzania tayari ina uwanja wake wa nyumbani wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam ambao uko kwenye ukarabati wa mwisho wa kuweka majukwaa.
Mtendaji mkuu wa bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema kutokana na sababu za kiusalama, mechi JKT Tanzania dhidi ya Simba na Yanga hazitafanyika kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo na sasa zitafanyika Uwanja wa Mkwakani Tanga.
"Tumefanya mabadiliko kwa timu ya JKT Tanzania tunajua wanatumia uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo, lakini kwa sababu ya usalama na wingi wa mashabiki Simba na Yanga hawataweza kwenda kucheza pale.
"Tumekaa na uongozi wa JKT Tanzania na wao wameomba mechi zao za Simba na Yanga za nyumbani watakwenda kuchezea Uwanja wa Mkwakwani Tanga na tayari klabu husika zimefahamishwa, TFF na waamuzi wote wamefahamishwa," alisema Wambura.
Katibu Mkuu JKT Tanzania, Abdul Nyumba ameishukuru Bodi ya Ligi kwa kuwakubalia ombi lao na sasa mashabiki wa Tanga wajiandae kuona mechi hizo.
"Tunaishukuru Bodi ya Ligi kwa kutambua yale matakwa yetu kwa sababu ukingalia matakwa jinsi yalivyo na uwezo wa uwanja wetu ulivyo usingeweza kuhimili mechi hizo.
"Uwanja wetu uko katika matengenezo,bado hauwezi kuhimili mechi ya Simba na Yanga kulingana na umaarufu wa mechi yenyewe kwani timu hizo ni maarufu.
"Bado uwanja hauwezi kuhimili mashabiki ambao watakuja kwenye mechi hiyo hivyo tumeomba tupelekwe Mkwakwani kama wenyeji wa mechi hizo na tunashukuru ombi letu limekubaliwa na tumeruhusiwa kucheza kule," alisema Nyumba.
JKT itaanza kucheza na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakani Tanga katika mchezo utakaofanyika Novemba 3.