JKT Stars yakosa mshindani RBA, mechi kurudiwa

MAMBO yanazidi kuwa magumu kwa timu za mpira wa kikapu za Kurasini Heat na ABC pamoja na kwamba Heat imeifunga ABC pointi 76-68  katika mchezo wa nne wa nusu fainali ya ligi ya RBA uliochezwa jana Alhamisi Uwanja wa Bandari, Kurasini.

Kwa matokeo hayo imefanya timu  hizo ziwe  zimefungana pointi 2-2 hali iliyofanya ikosekane timu itakayocheza na JKT Stars  kwenye fainali, hivyo timu hizo zinatarajia kurudiana kesho Jumamosi ili kupata mshindi.

Fainali za ligi hiyo ya RBA inatarajiwa kuchezwa keshokutwa Jumapili, kwenye Uwanja wa Bandari.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nahodha wa Kurasini Heat, Erick Lugola amesema licha ya kushinda mchezo huo lakini mechi ilikuwa ngumu na yenye ushindani.

“Kwa kweli mchezo ulikuwa ni mgumu sana, upande wa timu yangu kazi ilifanyika baada ya kushinda muda wa nyongeza," amesema Lugola.

Enrico Augustino ambaye ni mchezaji tegemeo wa ABC, amesema timu yake ingeweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo endapo ingetumia nafasi  vizuri walizopata za kufunga katika robo ya pili na ya tatu.  

Katika michezo minne ya timu hizo ilianza kwa  ABC  kuifunga Kurasini Heat pointi 72-65, Kurasini Heat ikashinda 75-72, ABC ikashinda  86-78 na mchezo wa jana Kurasini Heat  ilishinda pointi 76-68.

Mchezo wa jana uliopambwa na vikundi vya ngoma za uhamasishaji kutoka kwa timu hizo, iliyofanya mchezo  uonekane  mzuri na wenye ushindani mkubwa. 

Katika mchezo huo, ABC ilianza kuongoza robo ya kwanza pointi 15-10, 13-23, 20-14, 19-18 na mpaka mchezo unamalizika timu zilikuwa zimefungana pointi 66-66 ambapo muda wa nyongeza Kurasini Heat ilishinda pointi 76- 68.

Kwa upande wa ufungaji, Lugola wa Kurasini Heat aliongoza kwa kufunga pointi 25, akifuatiwa na Mwalimu Heri aliyefunga pointi 18  wakati upande wa ABC alikuwa Augustino aliyefunga pointi 19.