JKT Queens wapewe tu ndoo yao

Muktasari:

Timu hiyo imefunika kwa kila kitu katika ligi ya msimu huu ambao imesaliwa na mechi za raundi tano tu kabla ya kufikia tamati, kwani imefunga mabao 96 na kuruhusu wavu wao kuguswa mara nne tu mpaka sasa.

HAKUNA namna tena, wapewe tu taji lao. Ndio, watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, JKT Queens ni kama imeshindikana baada ya jioni hii kupata ushindi wake wa 16 mfululizo katika mechi za ligi hiyo na kujiweka katika nafasi nzuri ya kulieteta kwa mara ya pili.
JKT ikiwa nyumba kwenye Uwanja wa Isamuhyo ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Alliance Girls na kuzidi kujikita kileleni ikifikisha alama 48 kutokana na michezo 16 iliyocheza mpaka sasa.
JKT ndio timu pekee ambayo haijapoteza wala kutoka droo katika ligi ya msimu huu na inaziburuza timu zote 11 zinazoshiriki ligi hiyo iliyo msimu wa tatu tangu kuasisiwa kwake enzi za utawala wa Jamal Malinzi akiwa kama Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Timu hiyo imefunika kwa kila kitu katika ligi ya msimu huu ambao imesaliwa na mechi za raundi tano tu kabla ya kufikia tamati, kwani imefunga mabao 96 na kuruhusu wavu wao kuguswa mara nne tu mpaka sasa.
JKT wamesaliwa na mchezo mmoja tu kama itashinda kutazwa kuwa mabingwa tena, kwani watafikisha alama 51 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote ya ligi hiyo, kwani Mlandizi Queens ambayo ipo nafasi ya pili baada ya nao leo kushinda 2-0 dhidi ya Boabab Queens ina alama 35 tu.
Alama hizo za Mlandizi Queens waliopokwa taji na JKT msimu uliopita baada ya kulitwa katika msimu wa kwanza tu, ina maana kama itashinda mechi zake zote zilizosalia itafikisha alama 50.
Katika mechi nyingine za jioni ya leo, Marsh Queens wakiwa nyumbani jijini Mwanza wamelazimishwa sare ya 1-1 na Kigoma Sisterz, huku vibonde Mapinduzi Queens na Evergreen zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu na kuzifanya ziendelee kuwa mkiani zikiwa na alama sita kila moja.

Msimamo Ligi Kuu ya Wanawake
                                           P    W    D    L    F    A    PTS
1. JKT Queens                  16    16    0    0    96    4    48
2. Mlandizi Queens         16    11    2    3    37    8    35
3. Simba Queens             16    11    1    4    47    12    34
4. Alliance Girls               16    10    2    4    41    16    32
5. Panama FC                  15    9    2    4    35    23    29
6. Sisterz FC                      16    7    4    5    26    22    25
7. Yanga Princess             16    6    1    9    23    41    19
8. Tanzanite                      15    4    1    10    10    31    13
9. Baobab Queens            16    3    4    9    17    49    13
10.Marsh Queens              16    2    5    9    14    36    11
11. EverGreen                    16    1    3    12    8    56    6
12.Mapinduzi                    16    1    3    12    4    62    6