JKT Queens ilivyoliwa ngumu na Alliance

Muktasari:

  • Naye kocha wa Alliance Ezekiel Chobanka, alisema lengo lao lilikuwa ni kuvunja rekodi kwa JKT Queens ambao hawajapoteza tangu waanze ligi

TANGU ligi kuu ya wanawake Tanzania Bara (SWPL) ianze kwa msimu huu mabingwa watetezi JKT Queens walikuwa wanashinda mechi zao si chini ya mabao matatu, lakini wamekumbana na muziki wa Alliance Girls.

Katika mechi yao ya juzi JKT Queens imejikuta ikipata wakati mgumu na kushinda mechi kwa mabao 2-1 baada ya Alliance Girls kuonyesha kiwango cha hali ya juu.

Kocha wa timu hiyo, Ali Ali alikiri kwamba ilikuwa mechi ngumu kwao na kwamba zilizobakia mzunguko wa pili wanahitaji kuongeza nguvu zaidi.

“Alliance Girls ni timu yenye ushindani wa hali ya juu na ushindi ambao tumeupata wa mabao 2-1 ni kwa sababu ya uzoefu wa wachezaji nilionao”alisema.

Naye kocha wa Alliance Ezekiel Chobanka, alisema lengo lao lilikuwa ni kuvunja rekodi kwa JKT Queens ambao hawajapoteza tangu waanze ligi

“Kwa sasa tunaangalia ni namna gani tunamaliza msimu tunajipanga kwa mwakani ipo siku tutawafunga tena mabao mengi tu,” maneno ya Chobanka.