JKT hiyoo fainali RBA

Muktasari:

Matokeo hayo yanaifanya JKT kutinga fainali bila kufungwa katika mechi 20  ilizocheza mpaka sasa, ikiwamo 15 za awali, mbili na robo fainali na tatu za nusu fainali.

 

JKT imefuzu kucheza fainali ya Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA),  baada ya kuichapa Oilers pointi 84-63  katika mchezo mkali uliofanyika jana usiku kwenye uwanja wa Bandari Kurasini jijini Dar es Salaam.

 JKT sasa itasubiri mshindi wa mechi kati ya ABC au Kurasini Heat ambazo matokeo yao yataamuliwa na mechi  ya tatu itakayoanza saa  2:00  usiku

 Timu hizo kila moja imeshinda mechi moja, ABC ikitangulia kupata ushindi wa pointi 72-65, kabla ya Kurasini kulipa kisasi kwenye mchezo wa marudiano juzi kwa ushindi wa pointi 75-72.

 Kwa matokeo hayo, timu hizo zitacheza mechi nyingine tatu na mshindi wa mechi 3-2 ndiye atacheza fainali na JKT ambayo imefuzu baada ya kuichapa Oilers katika mechi tatu mfululizo.

 JKT ilianza na ushindi wa pointi 59-46, kisha ikashinda pointi 65-54 kabla ya jana usiku kushinda kwa pointi 84-63, matokeo ambayo yameipa tiketi ya fainali mapema huku Oilers ikiondoshwa mashindanoni bila kuonja ladha ya ushindi kwenye nusu fainali hiyo.