JK, Makonda wanaporudisha utani wa jadi Simba, Yanga

Muktasari:

Alichokifanya Kikwete Mkuu wa Dar es Salaam Paul Makonda akakifanya ukumbini hapohapo kwa kuipa eneo Yanga kule Kigamboni ili nao wajenge uwanja.

Jambo moja nililoondoka nalo katika ukumbi uliofanyika harambee ya Yanga iliyopewa jina la Kubwa Kuliko ni juu ya maisha halisi ya klabu kongwe hapa nchini Simba na Yanga.

Hotuba ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ilikuwa fupi na tamua ambayo ilikuwa na elimu kubwa maisha halisi ya sasa ya klabu hizi kongwe.

Kikwete ni mmoja kati ya marais waliokuwa wadau wakubwa wa michezo na katika utawala wake wa miaka 10 alifanya makubwa ingawa viongozi mbalimbali hawakutumia nafasi hiyo vyema kuhakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo.

Hotuba yake ilikuwa na elimu kubwa akianzia kuwakumbusha viongozi wenzake jinsi gani wanatakiwa kufanya maamuzi kwa usawa wakiwa madarakani.

Alikumbusha ukiwa kiongozi wote waliokuzunguza ni wa upande wako na wanatakiwa kutumikiwa na wewe tena kwa usawa bila upendeleo wa kile unachokipenda.

Hakuishia hapo kilichonifurahisha mimi ni pale alipokuwa akisimulia jinsi alivyokuwa na mchango katika klabu ya watani wake Simba tena wa kimaendeleo.

Kubwa ni ile ya kusaidia fedha kiasio cha Sh30 milioni ili klabu hiyo ipate eneo la kujenga uwanja wao kule Bunju na harakati hizo za ujenzi zinaendelea sasa ingawa kwa kusuasua.

Akili au msukumo wa Kikwete kuisaidia fedha zile Simba licha ya kutaka kuona klabu hiyo inapiga hatua kimaendeleo lakini pia alidumisha desturi ya klabu hizo mbili kuwa na tofauti uwanjani tu na baada ya dakika 90 watu wote wanakuwa familia moja kwa kushirikiana.

Alichokifanya Kikwete Mkuu wa Dar es Salaam Paul Makonda akakifanya ukumbini hapohapo kwa kuipa eneo Yanga kule Kigamboni ili nao wajenge uwanja.

Makonda tayari ameshawaonyesha eneo hilo viongozi wa Yanga na huenda kesho ikawa ni siku ya makabidhiano rasmi kama ratiba itaenda kama ilivyopangwa.

Huu ndio utani wa jadi wa klabu hizi kongwe na sio mambo yanayoendelea sasa kwa klabu hizi kuwa mahasimu na utofauti mkubwa.

Kikwete na Makonda wanapita katika njia ambayo ilikuwa miaka mingi huko nyuma kwa klabu hizi kuwa ndiyo chanzo cha ushirikiano na hata kuzikana panapotokea matatizo.

Baadhi ya viongozi waliopita hapa kati na hata sasa baadhi wamezifanya klabu hizi kuwa maadui kwa kushafiana mambo mbalimbali na kuondoa dhana ya awali ya kushirikiana.

Watu wa sasa hawako tena katika utani wa jadi wao wamekwenda nje na kuanzidha uadui wa jadi kwa kufikia uwanjani hata kupigana,kuvuana nguo na hata kutoleana lugha kali.

Msukumo mkubwa wa uharibifu wa dhana ya umoja wa Simba na Yanga unatoka kwa viongozi baadhi wa klabu hizi ambao katika kutafuta umaarufu wao wamekuwa wakiendelea kutengeneza tabaka kubwa la utofauti.

Pale Afrika Kusini katika nchi ambayo ina baadhi ya raia wakorofi zaidi klabu zao kubwa ni Orlando Pirates na Keizer Chiefs.

Unaweza kushangaa utakapoona timu hizo zikicheza mechi baina yao,utulivu mkubwa, amani na nidhamu ya ushangiliaji hutawala muda wote wa mchezo.

Shabiki wa Pirates anakaa karibu kabisa na yule wa Chiefs na wote wanashangilia timu zao bila kugombana tena kila mmoja akiwa na jezi ya klabu zao lakini hilo haliwezi kutokea katika mechi za Simba na Yanga.

Ushabiki wa Simba na Yanga sasa uko mbali kiasi cha kuweza hata kudhuliana mwilini kitu ambacho ni tofauti na huko nyuma.

Ni wakati sasa watu katika klabu hizi mbili wakajitathimini na kuanza kubadilika kupitia elimu hii ya kutoka kwa Kikwete na hata Makonda.