JIPANGE: Viungo hawa ukitaka saini zao utavunja benki

Thursday December 6 2018

 

LONDON, ENGLAND.THAMANI za wanasoka kila mwaka zimekuwa zikipanda na wengine zimekuwa zikishuka. Mwaka huu umeshuhudia thamani za wachezaji wengi sana zikipanda na hivyo kufanya huduma zao unapozihitaji basi ni lazima utoboe mfuko.

Hawa hapa ndio viungo ambao hakika katika kipindi cha mwaka mmoja wamepandisha thamani zao na sasa ukitaka kuwasajili basi ujipange, utavunja benki.

5.Saul Niguez – Atletico, Euro 90 milioni

Saul amefanikiwa kuliweka juu jina lake kwenye ulimwengu wa soka akitambulika kama mmoja wa viungo matata kabisa unaowahitaji kuwapo kwenye kikosi chake.

Kimo chake ni futi sita na hakika Mhispaniola huyo ana kasi na uwezo mkubwa sana wa kuuchezea mpira anavyotaka na ndio maana anaonekana kama kizazi adimu sana katika zama hizo za soka la Wahispaniola.

Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone amewatengeneza na kuwaibua wachezaji wengi sana katika klabu hiyo na Saul ni mmoja wa wachezaji hao ambao hakika ubora wao wa uwanjani umefanya thamani zao kwenda juu na ukitaka kumsajili pochi yako isikose Euro 90 milioni.

4.Sergej Milinkovic-Savic – Lazio, Euro 90 milioni

Kiungo huyo wa Kiserbia amekuwa na ofa nyingi sana mezani kwake. Manchester United na vigogo wengine kibao walisumbuka sana kwenye dirisha lililopita wakijaribu kuisaka huduma yake.

Hakika ni moja ya vipaji adimu sana vinavyopatikana kwenye timu za kawaida na si vigogo na ndipo maana timu kama Man United, Real Madrid na Barcelona zinahangaika sana kuitaka huduma yake.

Staa huyo anaweza kucheza kama kiungo wa kati au kiungo wa kushambulia. Wakati kipindi cha usajili wa dirisha la Januari kikitarajia kuanza hivi karibuni tu, hakuna mashaka timu kibao zitakwenda kutaka saini ya Milinkovic-Savic. Staa huyo hapatikani kwa mkwanja unaopungua Euro 90 milioni.

3.Dele Alli – Tottenham, Euro 100 milioni

Akikaribia kufunga mabao 40 katika mechi zaidi ya 100 alizochezea Tottenham Hotspur, Dele Alli ni mmoja wa wachezaji muhimu sana wa kocha Mauricio Pochettino kwenye kikosi hicho.

Ni kiungo anayeweza kuwa kiunganisha vyema kwa wachezaji wenzake na wakati mwingine anaweza kucheza kwenye nafasi ya ushambuliaji na nafasi nyingine kulingana na anavyotumika kwa siku husika.

Akiwa bado hajashinda taji lolote kubwa kwenye maisha yake ya soka, Dele amepandisha kiwango chake na kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa kabisa na ukitaka saini yake kwa sasa basi jipange na mkwanja usiopungua, Euro 100 milioni.

2.Philippe Coutinho – Barcelona, Euro 150 milioni

Fundi wa mpira wa Kibrazili, Philippe Coutinho amekuwa kwenye ubora mkubwa kabisa huko Barcelona akiwasaidia katika harakati zao za kubeba mataji matatu msimu huu. Fundi wa kufunga mabao ya mashuti ya mbali.

Huko Barcelona, kocha Valverde amemchezesha eneo la chini kidogo, akimpa uhuru wa kuvuruga sehemu ya katikati ya uwanja.

Barca ilimnasa Januari kwa ada ya Euro 130 milioni, lakini sasa thamani yake imepanda na ukitaka saini yake ni Euro 150 milioni.

1.Kevin De Bruyne – Man City, Euro 150 milioni

Shughuli yake anayofanya huko Manchester City akiwa chini ya Mhispaniola Pep Guardiola ni matata kweli kweli kiasi cha kuzivutia timu kibao zinazohitaji huduma yake.

De Bruyne amekuwa mchezaji anayeogopwa zaidi na timu pinzani huku pacha yake na David Silva imekuwa yenye matata uwanjani.

Chelsea wao walimuuza KDB kwa Euro 22 milioni tu, lakini kwa sasa ukitaka huduma yake, yakupasa uwe na mkwanja unaoanzia Euro 150 milioni.

Advertisement