JICHO LA MWEWE: Viungo wetu wana hofu na akili zao au miili yao

Monday September 14 2020

 

By EDO KUMWEMBE

RAFIKI yangu mmoja aliniuliza tofauti kati ya viungo wawili wapya wa Yanga, Tanombe Mukoko na Zawadi Mauya. Huyu Tanombe ametoka nje ya nchi, Mauya tunaye hapa nchini. Msimu uliopita alikuwa na msimu bora zaidi nchini hatimaye akanunuliwa na Yanga.

Mechi iliyopita ya Yanga kabla ya hii ya jana, walicheza na Tanzania Prisons na mmoja kati ya wachezaji wapya ambaye aliwakosha mashabiki alikuwa Mauya. Mimi mwenyewe alinikosha. Alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Alionekana kuwa na utulivu mkubwa.

Baadaye aliingia mchezaji aliyeitwa Mukoko. Akacheza mpira tofauti na ule aliokuwa anacheza Mauya. Rafiki yangu akaniuliza tofauti yao. Wote hawa wanaonekana wamefika katika timu kwa ajili ya kuziba pengo la Papy Tshishimbi.

Nilichomwambia rafiki yangu ni kwamba Mukoko aliingia uwanjani akicheza soka la kutafuta matokeo zaidi. Mpaka wakati huo pambano lilikuwa sare na aliingia uwanjani kwa ajili ya kuona timu yake inapata bao la pili kwa haraka.

Kazi yake kubwa ilikuwa kukokota mpira kwa hatua sita mbele na kuisukuma timu mbele. Mauya alikuwa anapiga pasi pale pale alipokuwepo na alikuwa anawapasia watu wa karibu. Mukoko alikuwa anajaribu kuisukuma timu mbele kwa staili mbili. Kwanza ilikuwa ni yeye mwenyewe kusogea na mpira kwa hatua nyingi.

Pili alikuwa anapiga pasi ndefu kwenda mbele pembeni hasa upande wa kushoto ambapo walikuwepo Yassin Mustapha, beki wa kushoto na rafiki yake wa karibu, Tuisila Kisinda. Yanga walifurahia soka lake ingawa kabla ya hapo waliguna kwanini Mauya alitolewa uwanjani.

Advertisement

Kinachotokea hapa ni kwamba viungo wetu wengi hawaamini utimamu wa miili yao lakini pia utimamu wa akili zao. tunapokea malalamiko mengi kwamba hawa kina Jonas Mkude, Fey Toto na wengineo wanapiga sana pasi za karibu au zinazokwenda magharibi na mashariki. Hawapigi pasi za madhara.

Linapokuja suala la kutembea na mpira kwa hatua saba au nane kama Mukoko alivyokuwa anafanya hii inatokana na kuamini nguvu za mwili wako. Kwamba unajua adui yeyote utakayekutana naye utafanikiwa kumshinda katika matumizi ya nguvu.

Viungo wetu wengi wanapiga pasi za nyuma au za pembeni kwa sababu ni maeneo salama zaidi. Hawataki rabsha za kwenda mbele kwa sababu wana hofu na matumizi yao ya miili. Wanahisi wakijaribu kutembea na mpira watapokonywa kiurahisi.

Kuna aina mbili za wachezaji wanaopenda kutembea na mpira. Wale wenye kasi kama kina Saimon Msuva ambao wanategemea zaidi kasi zao, lakini pia wale wenyewe nguvu wanaojivunia nguvu zao. Ndio hawa kina Mukoko.

Kuna viungo wachache ambao hawahofii kwenda mbele huku wakiamini zaidi akili zao za soka kuliko nguvu na mengineyo. Mmojawao ni huyu Clatous Chama. Hana nguvu nyingi na wala hana matumizi ya nguvu, lakini anaamini kwamba mpira utakuwa salama kwa sababu ana akili kuliko wachezaji wa timu pinzani. Haishangazi kuona Chama ni mchezaji hatari zaidi kwa sasa nchini.

Lakini katika suala hili hili la kupiga pasi ndefu kuna viungo wetu wengi wanahofia akili zao. Mukoko alikuwa anapiga pasi ndefu kwenda kwa watu wa mbele pembeni. Alikuwa ananikumbusha Athuman Idd ‘Chuji’. Alikuwa na uhakika na akili yake. Wachezaji wetu wana hofu kwamba huenda kila atakapopiga pasi zake zikawa fyongo au zikatoka nje. Ni uoga tu wa kushindwa kuiamini akili yako.

Matokeo yake tuna viungo ambao wanajaribu kucheza mpira salama zaidi wakihofia akili zao na utimamu wao wa miili. Anachukua pasi hapa karibu anapiga hapa karibu. Anapofungua chumba akiwa peke yake anapokea mpira na anapiga tena pasi ya karibu hapo hapo. Timu inajikuta haiendi mbele kwa kasi.

Mauya anapaswa kujifunza zaidi kwa Mukoko wakati mchezaji kama Fey Toto anapaswa kujifunza zaidi kwa Chama hasa anapopangwa katika eneo la mbele. Msimu huu naona atakuwa akipangwa mbele zaidi huku Mauya na Mukoko wakicheza nyuma yake. Lazima ajiamini na mpira na atembee na mpira.

Vinginevyo viungo wetu wataendelea kucheza ‘soka salama’ kwa muda mrefu. Soka ambalo halizisaidii sana timu, ingawa pia halina madhara kwa timu.

Advertisement