JICHO LA MWEWE: Umbea unaopatikana katika sinema ya Tshishimbi

Monday August 3 2020

 

SINEMA huwa haziishi katika mpira wetu. Wiki iliyopita tulikuwa na sinema ya Papy Tshishimbi. Kiungo mkabaji wa Yanga. Inachekesha sana kwa kile kilichotokea, lakini ndio hali halisi ya soka letu.

Naweza kuandika hisia zangu, lakini pia nina habari za kuokotaokota kutoka kwa watu wa Yanga. Katika hisia zangu inaniambia wakati fulani Tshishimbi alionekana kuwa mchezaji muhimu pale Jangwani. Ndani ya msimu huu huu.

Wakati huo mkataba wake ulikuwa unaelekea ukingoni mwishoni mwa msimu huu ulioisha majuzi. Wakati ule Tshishimbi alikuwa ameikamata Yanga pabaya. Inaonekana alikuwa anatingisha hapa na pale. Kauli kama ile kwamba angetamani kucheza na wachezaji mafundi wa Simba iliivuruga Yanga.

Wakati ule Yanga walipambana kutaka kumbakisha Tshishimbi. Wakamuahidi pesa ndefu. Baada ya kuvutana hapa na pale, Yanga wakamkubalia alichotaka.

Ni wakati huu ambapo Yanga walitangaza kwamba, wamefikia makubaliano na Tshishimbi. Baadhi ya wanachama na mashabiki wakajipa tafsiri tofauti kuwa Tshishimbi amesaini mkataba mpya. Hata hivyo, naambiwa baadaye Papy alikuja kubadilika na kutaka apewe gari juu ya kile alichoahidiwa.

Lakini hapo hapo ulitokea mvutano kuwa kwa alichoahidiwa basi asaini mkataba wa miaka miwili huku yeye akitaka kusaini mkataba wa mwaka mmoja. Mvutano uliendelea mpaka mwishoni mwa msimu ulioisha.

Advertisement

Yanga wakapata habari za kuaminika kutoka katika hospitali moja ambayo Tshishimbi alikuwa anatibiwa. Kwamba goti lake ambalo lilimfanya acheze mechi moja tu dhidi ya Simba baada ya soka kurejea kutokana na kusimama kwa corona, lisingeweza kupona vyema.

Wakati wakiambiwa hivyo dirisha la usajili lilikuwa linakaribia na Yanga walianza kuzungumza na viungo wakali wenye afya njema. Mmoja ni huyu Gift Mauya waliyemsajili kutoka Kagera Sugar. Mwingine ni kiungo mkali kutoka DR Congo.

Kuanzia hapo Yanga wakaanza kumringia Tshishimbi. Wakaanza kumpiga mkwara kuwa, asaini mkataba wa miaka miwili au arudishe pesa zao. Tshishimbi hakugundua mtego ambao alikuwa amewekewa na viungo.

Wakati huo huo kasi ya Simba kumnyemelea Tshishimbi ikaanza kutoweka. Viungo wao wa nafasi ya chini, Mbrazil Fraga pamoja na Jonas Mkude wapo moto kweli kweli. Na hapa ndipo Tshishimbi akataka kuanza kuhaha tena katika vyombo vya habari.

Kwa sasa inaonekana kama vile Yanga wameshika mpini na yeye ameshika makali. Yanga inawafikiria viungo wapya zaidi kuliko Tshishimbi, ambaye amekosekana uwanjani kwa muda mrefu.

Nadhani Tshishimbi ameanza kuelewa hilo. Wiki iliyopita ilinishangaza kidogo kumsikia Tshishimbi akishindwa kuaga Yanga. Anaondoka nchini kwenda likizo huku akishindwa kujua hatima yake Yanga.

Jambo hili linanishangaza kidogo. Mchezaji ambaye mkataba wake unamalizika kwanini asijue hatima yake?

Wachezaji wengi ambao mikataba yao inamalizika huwa mioyo yao inafanya sherehe hasa kama wanafahamu ubora wao.

Kifupi ni kuwa wanakwenda kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata mkataba mkubwa katika klabu nyingine ambayo haitalazimika kumnunua kutoka katika klabu yake iliyopita.

Nilidhani Tshishimbi angefurahi kuwa free agent kama ambavyo Bernard Morisson analazimisha kwamba yeye ni free agent.

Ghafla maisha yamebadilika kwa Tshishimbi na anaonekana anaitaka Yanga ingawa hii ilikuwa fursa nzuri kwake kupata mkataba mkubwa kwingineko.

Kitu kibaya kwa Tshishimbi ni namna ambavyo hapo katikati alianza kuvunja madaraja na watu wa Yanga kwa kusema anapenda kuichezea Simba kutokana na eneo la katikati kuwa na wachezaji mafundi.

Kwa siasa za mpira wetu, hata kama alikuwa ana haki ya kusema mtazamo wake, lakini upepo wa mahusiano na klabu huwa unatoweka ghafla kwa siku za karibuni.

Kwa upande wa Yanga ni vema na wao wakajitafakari. Sawa, ofa yao kwa Tshishimbi iko mezani lakini kama wanataka kubadili gia angani kwa sababu wana uhakika wa kupata viungo wapya, au wamegundua kwamba goti la Tshishimbi lina matatizo walipaswa kujua haya mapema.

Mchezaji anapokwenda katika mwaka wake wa mwisho wa mkataba ni bora klabu kuamua mapema kwamba inamhitaji mchezaji au hapana. Ukizungumza na viongozi wa Yanga wakati wanataka kumbakisha Tshishimbi, na ukizungumza nao sasa hivi unagundua kwamba, ni binadamu tofauti kabisa.

Wakati ule walikuwa wakizungumza lugha ya ‘Tshishimbi lazima asaini mkataba mpya’.

Kwa sasa hivi wanazungumza lugha ya ‘aende kokote anakotaka’. Kuna karata wanazo mkononi na inaonekana wamezichanga vema. Lakini walipaswa kuzichanga karata hizo mapema zaidi ya sasa.

Klabu zetu zinapaswa kuwa taasisi kubwa na wasifanye mambo kwa kubadili upepo kwa wepesi sana. Wakati mwingine inawachanganya hata mashabiki ambao mpaka siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho huwa hawaelewi wachezaji gani wanaondoka klabuni.

Kitu cha msingi katika haya ni mabadiliko ambayo yatawafanya wawe taasisi imara.

Taasisi ambayo itaweka mfumo wa uwajibikaji kwa kila mtu klabuni. Hiki ndicho kitaondoa ubabaishaji.

Advertisement