JICHO LA MWEWE: La Morrison linaturudisha nyuma mwaka 1947

UKIKUTANA na mzungu ameshika gazeti la Kiingereza pale Posta likiwa na habari hizi za sasa za Bernard Morrison halafu akauuliza inawezekana vipi, usimfiche. Mwambie ukweli. Anachokiona ndio hali halisi.

Mwambie inawezekana sana hapa Tanzania. Mchezaji mmoja kusaini mikataba miwili au mchezaji mmoja kusaini mkataba mmoja lakini wengine wakadai bado ana mkataba nao. Inawezekana sana Tanzania na sio mara ya kwanza. Nahofia inaweza isiwe mara ya mwisho.

Majuzi tu mchezaji anayeitwa Pius Buswita aliitwa na wakubwa wa Dar es salaam, Simba na Yanga na akasaini mikataba miwili tofauti ya klabu hizi. Mwishowe Yanga walishinda kesi na wakarudisha pesa za Simba. Sijui Buswita yuko wapi na nadhani waliomgombania wanajuta.

Kabla ya hapo alikuwepo Mbuyu Twite. Naye alisaini mikataba miwili. Akaishia kucheza Yanga. Walau yeye aliifanyia Yanga mambo makubwa kuliko Buswita. Hata hivyo, haiondoi kumbukumbu kwamba naye aliwahi kufanya ujinga huo.

Na sasa mkononi tuna kesi ya Mghana anayeitwa Bernard Morrison. Simba wana mkataba wake wa miaka miwili na walimtangaza juzi. Yanga wamebakiza jina lake katika orodha ya wachezaji ambao wataitumikia klabu yao msimu ujao wakidai kwamba ana mkataba wa miaka miwili.

Ni mambo ya kizamani, lakini bado yapo. Sina majibu. Na mimi najiuliza maswali yale yale ambayo mashabiki wanajiuliza. Inawezekana vipi Yanga kufoji saini yake katika dunia hii ya kisasa? Inawezekana vipi? Kwanini wafanye hivyo?

Na mtu mwingine atajiuliza swali jingine. Mbuyu na Buswita hawakuwahi kukana kusaini mikataba pande zote mbili. Lakini Morrison anakana kabisa kwamba hakusaini mkataba wa Yanga. Zamani ilizoeleka kwamba mchezaji angeanza kuwa mkimya baada ya kuhisi ameyakoroga na mwishowe kuacha timu zimalizane zenyewe, lakini Morrison ameendelea kusisitiza hana mkataba na Yanga.

Tangu sakata hili lilipoanza na Yanga kuhisi kwamba Morrison amesaini Simba nadhani walikuwa na nafasi ya kujitafakari na kuachana naye kama kweli walikuwa wamefoji saini yake. Kufoji saini ni kosa la jinai. Kwanini bado wamebakiza jina lake klabuni? Kwanini baada ya picha kusambaa mitandaoni wakatoa taarifa kwa mashabiki wao kwamba Morrison ni mchezaji wao na ana mkataba nao wa miaka miwili?

Ina maana viongozi wa Yanga hawajui rungu la mamlaka za dola? Ina maana viongozi wa Yanga hawajui watakachokutana nacho mbele ya safari? Kwanini bado wameendelea kujiamini na mchezaji mwenyewe ameendelea kusisitiza kwamba hakuwa na mkataba na Yanga?

Tukiachana na hilo tunageuka upande wa pili. Simba wanajiamini nini na mchezaji mwenyewe? Wana uhakika kwamba Yanga wana mkataba feki? Mkataba wa pili wa Morrison upo TFF, wana uhakika kwamba haujaingizwa katika mifumo ya usajili ya mchezaji?

Mwisho wa siku tunaulizana, yuko wapi wakala wa Morrison? Hajawahi kuonekana sura hapa nchini. Hajulikani hayupo. Mchezaji anayewezaje kufanya mambo haya kienyeji bila ya wakala? Hasa mchezaji ambaye anatoka katika taifa la Afrika Magharibi ambalo tunaamini kwamba lina wachezaji wanaojitambua.

Mwisho wa siku nadhani kesi ya Morrison inapaswa kuwa mfano wa mwisho mbaya katika masuala ya uhamisho ya wachezaji ndani ya soka letu. Wenzetu waliondoka huku miaka mingi iliyopita. Mchezaji wa mwisho ninayemkumbuka aliyezitia klabu mbili kubwa za Ulaya vitani ni Obi Mikel.

Alisaini mkataba wa awali na Manchester United na kisha akasaini mkataba kamili na Chelsea. Baadaye Chelsea walifanikiwa kumpata mchezaji, lakini ilitokana na umri wake kuwa mdogo huku pia United wakishutumiwa kumpata bila ya kumhusisha wakala wake.

Mwisho wa kila kitu ni kwamba suala la Morrison linaonekana kuwakera mashabiki waelewa wa pande zote mbili. Mashabiki wajinga watakuwa na furaha kwamba ama Morrison amehama timu yao au amehamia timu yao.

Mashabiki waelewa na wasomi na wachambuzi wa mambo watakerwa zaidi na kitendo hiki kwa sababu kinarudisha nyuma soka letu. Tunaishi zama za zamani katika nyakati ambazo wenzetu walishasahau ujinga huu wa ama mchezaji kusaini mikataba miwili au kutojulikana uhalali wake.

Hawa mashabiki wanaokerwa sana ni wale ambao tunadai sio wazalendo pindi wanapouponda mpira wetu na kukimbilia kushangilia timu za Ulaya. Tutawaambia nini wakati tunapojikuta katika hali kama hii.

Ligi Kuu imebeba viwanja vibovu, timu dhaifu ambazo haziwezi hata kulipa mishahara kwa wachezaji wake, leo tunawaongezea ujinga kama huu wa Morrison. Tutawaambia nini watoto wetu ambao wameanza kujikita kupenda soka la Ulaya kwamba mpira wetu ni mzuri?

Ifike mahala watendaji wa klabu zetu na maofisa wanaoongoza mpira wetu wamalize hivi vioja. Vinatia aibu. Dunia inaenda kasi na wenzetu wapo katika hatua za VAR na Goal Line Technology. Mambo ya Morrison yamebakia kuwa historia kwao. Wanakimbizana na mambo ya kisasa zaidi na walishamaliza zamani mambo ya kizamani kama haya.