JICHO LA MWEWE: Kwa Zlatko Krmpotic ilikuwa suala la muda tu

Muktasari:

Tatizo kubwa kwa Zlatko sio tu timu yake ilikuwa haichezi vizuri, pia kulikuwa hakuna dalili ya mabadiliko kwamba itacheza vizuri siku za usoni, kila mechi ilikuwa hadithi

KOCHA Mserbia, Zlatko Krmpotic alikuja nchini kwa haraka na ameondoka kwa haraka pia. Alikuja nchini ndani ya saa 24 tangu atakiwe kibaruani na ameondoka ndani ya saa 24 tangu kibarua chake kikomeshwe.

Safari ya kuondoka kwake ilitabirika mapema. Binafsi niliitabiri mapema. Ilikuwa ni katika pambano kati ya Yanga dhidi ya Mbeya City. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuiona Yanga ikicheza chini ya kocha huyu.

Sikujali sana matokeo kama ambavyo Yanga hawajajali sana lilipokuja suala la kumtimua kocha. Walitazama jinsi gani timu yao ilivyokuwa inacheza. Siku hizi Watanzania wameelimika katika masuala mawili. Suala la kwanza ni kutaka timu yao iende kwa tajiri. Zamani ilikuwa vita kweli kweli kufikirika mtu mmoja angeweza kuimiliki Yanga au Simba. Siku hizi wanachama na mashabiki wamechoka kukaa na njaa. Wapo tayari kwa hilo.

Jambo jingine ni siku hizi wanachama na mashabiki wanataka kuona timu yao ikicheza mpira. Wanachama wanafuatilia soka la Ulaya kwa umakini mkubwa. Wanaijua timu inayocheza vizuri na wanaijua timu inayocheza ovyo. Wanajua timu inayokaba vizuri na wanaijua timu inayoshambulia vizuri. Haijalishi wanapata matokeo ya aina gani.

Pambano dhidi ya Mbeya City, Yanga ilicheza pambano lote kama vile wanacheza katika dakika tano za mwisho, huku timu yao ikiwa imefungwa. Yaani kama vile ilikuwa inalazimisha kuchomoa bao kwa hali na mali.

Kuna mpira wa namna hiyo duniani kote. Unapiga mpira mmoja mrefu kwenda mbele huku wote mkiwa mmekusanyika mbele. Bahati mbaya ni Yanga ilikuwa inafanya hivyo kumsaka mshambuliaji wao, Michael Sarpong pekee. Mashabiki na viongozi wa Yanga hawakuwahi kuelewa aina hii ya mpira. Majuzi tu Yanga ilikuwa imetoka katika aina ya mpira wa ‘Kampa kampa tena’ ulilokuwa unaongozwa na fundi kutoka Zimbabwe, Thaban Kamusoko. Inawezekana hawakutarajia sana kupata mpira huo katika vikosi vyao kadhaa vilivyokuja lakini baada ya usajili wa pesa nyingi katika dirisha hili lililopita walitazamia kuupata tena mpira ule.

Kilichowakera mashabiki wa Yanga ni kwamba mpira ule wa kina Kamusoko umehamia kwa watani zao Simba. Mastaa wa Simba wanautandaza hasa. Wanaweka chini mpira kuanzia nyuma mpaka katika lango la adui.

Matokeo ya mwisho ya pasi za Simba ni kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Haishangazi kuona John Bocco anafunga, Chris Mugalu anafunga, Meddie Kagere anafunga na hata Charles Ilamfya naye anafunga.

Haishangazi kuona viungo wao wanafunga pia. Lakini zaidi ya kila kitu, Simba imeweza kujipambanua nani ni nani katika timu. Kwa mfano, kila mtu anajua kazi ya Clatous Chama katika kikosi cha Simba. Lakini mpaka sasa Yanga hawajui nani anafanya kazi ya Chama katika kikosi chao.

Ilitangazwa na watu wa Yanga kwamba Carlinhos angekuwa ‘Chama mpya’ katika kikosi cha Yanga, lakini mwishowe Zlatko alikuwa anampanga akitokea pembeni. Mchango wake mkubwa ulikuwa ni kutumia kipaji chake binafsi cha kupiga mipira ya adhabu na kona. Ndani ya mfumo hatukujua Carlinhos alipaswa kukaa wapi, lakini pia hatukujua viungo wengine walikuwa na kazi ya kufanya nini uwanjani. Kwa mfano pale Morogoro kiungo mkabaji, Tanombe Mukoko alipangwa kucheza namba kumi. Haya yalikuwa maajabu ya Zlatko. Labda kwa sababu alifunga bao katika pambano dhidi ya Kagera Sugar pale Kaitaba.

Katika mechi hiyo dhidi ya Kagera ndipo tulipoona maajabu mengine ya Zlatko. Aliwapanga kwa pamoja viungo watatu wa ulinzi. Mukoko, Feisal na Gift Mauya. Timu ilikuja inajibaka yenyewe zaidi. Ni sawa na kuwapanga Jonas Mkude, Fraga na Mzamiru Yassin ndani ya mechi moja.

Achilia mbali hilo, mashabiki wa Yanga kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu walikuwa wakitazamia timu yao sasa icheze kama Simba, icheze kwa kumtawala adui kwa pasi nyingi na ubora mwingi. Matokeo yalikuwa muhimu kwao, lakini yalipaswa kuja na mpira mwingi uwanjani sio kutegemea tu mabao ya ushindi ya beki wa kati, Lamine Moro. Timu yake ilikuwa haichezi vizuri, pia kulikuwa hakuna dalili ya mabadiliko kama itacheza vizuri katika siku za usoni.