JICHO LA MWEWE: Kwa Samatta tulikuwa tunatembelea uzi mwembamba

FIKIRIA kama dirisha dogo la usajili la Januari wakati Mbwana Samatta angekuwa anakwenda Aston Villa, labda Ibrahim Ajibu angekuwa anatua Real Betis ya Hispania.

Aidha wakati wawili hao wakisaini kule pengine naye Shomari Kapombe angekuwa anasaini Marseille ya Ufaransa, huku John Bocco naye angekuwa ametua Cagliari ya Italia.

Kifupi labda tungekuwa na mastaa wengi ambao wametua katika soka la Ulaya katika zile ligi kubwa tano maarufu ambazo ni England, Italia, Ufaransa, Ujerumani na Hispania.

Maumivu ya Samatta kuachwa na Aston Villa yasingetupa maumivu na wala tusingetupia matusi katika mitandao yao ya jamii. Ukweli ni kwamba tumeumia Samatta kuondoka England. Tulitamani abakie pale ili tumtazame kila wikiendi.

Kuna mambo yameendelea ndani ya Villa. Kuna siasa zimeendelea. Amekuja Mkurugenzi Mpya wa Ufundi na akataka kuleta watu wake. Samatta alitolewa mhanga. Angeweza kucheza msimu huu na hatima yake kuamuliwa baadaye lakini wameona bora waachane naye kwa sasa bila ya sababu za kisoka.

Kisoka Villa ilibidi wamvumilie Samatta ili aendelee kuzoea soka la Kiingereza na huu ndio msimu ambao wangeweza kuamua kitu kuhusu uwezo wa Samatta. Ikumbukwe kuna wachezaji kibao ambao walichelewa kuzoea soka la Kiingereza, lakini walipozoea walikuwa moto. Mmoja wapo ni Thierry Henry ambaye alicheza mechi 10 za mwanzo pale Arsenal bila ya kufunga bao lolote.

Hata hivyo, wao wameamua kuachana naye sasa hivi bila ya kumpa muda. Maamuzi haya yamewaumiza Watanzania kwa kiasi kikubwa lakini tatizo kubwa lipo upande wetu.

Kama tungekuwa na wachezaji wengi wanaocheza Ulaya nadhani tusingesikia maumivu haya. Tatizo kubwa hapa ni kwamba Watanzania milioni 56 wanamtegemea mchezaji mmoja tu anayecheza Ulaya katika ngazi kubwa, Mbwana Samatta. Hatuna wafariji wengine.

Kama tungekuwa na wachezaji wengi tusingesikia maumivu haya. Kwa Samatta tulikuwa tunatembelea katika uzi mwembamba ambao ungeweza kukatika muda wowote ule kama ilivyotokea kwa Samatta pale Aston Villa.

Mungu alimfikisha Samatta England, lakini tujaribu tu kufikiri, kama Samagol angepata majeraha akiwa TP Mazembe si ajabu mpaka leo tusingekuwa na mchezaji yeyote aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya Ubelgiji au ya England.

Haya ndio madhara ya wachezaji wetu kugoma kutoka nje na kuwa wavumilivu pindi wanapokwenda kucheza nje. Haya ndio madhara ya timu zetu, hasa kubwa kutokuwa na sera ya kutengeneza makinda na kuwauza. Taifa limebakia kumtegemea mchezaji mmoja tu. Tunampa mzigo mkubwa Samatta.

Watanzania na hata majirani zetu Wakenya tumekuwa tunatembelea katika uzi mwembamba kwa muda mrefu na matokeo yake pengo kati ya Samatta na wengine ni kubwa kama ilivyokuwa kwa Victor Wanyama dhidi ya wengine pale Kenya.

Wanyama alipoondoka England kwenda Canada hakuna Mkenya mwingine ambaye Wakenya wanaweza kujivunia pale England au kwingineko barani Ulaya. Ni kama hiki ambacho kimetokea kwa Samatta. Hakuna Mtanzania mwingine ambaye tunaweza kumtazama katika Ligi tano kubwa za Ulaya.

Kwa wenzetu Ivory Coast, Nigeria, Senegal, Mali na kwingineko hawana Samatta mmoja. Wamegawanyika wakiwafuatilia wachezaji wao mbalimbali. Kama Yaya Toure ameondoka pale England basi kuna staa mwingine wa Ivory Coast atatamba pale au kwingineko.

Kwa sasa Watanzania tumeelekeza masikio yetu kwa Kelvin John. Mwakani ataenda kujiunga rasmi na Genk na huenda tukaanza safari naye kama tulivyosafiri na Samatta kuanzia TP Mazembe, kisha Genk, halafu Aston Villa na sasa Fenerbahce. Kwanini wasitokee kina Kelvin John 20 waliotawanyika katika timu mbalimbali Ulaya?

Huyu Kelvin naye tutaanza kumtwisha mzigo kama tuliomtwisha Samatta. Naye kama mambo yakienda kombo mbele ya safari tunaweza kujikuta hatuna mtu mwingine wa kujivunia ukizingatia kuwa, Samatta ameshaanza kutupwa mkono na umri.

Inabidi tujifunge kamba kuzalisha wachezaji wengi wanaokwenda nje ya nchi kila kukicha. Wachezaji wetu wajifunze uvumilivu, mawakala wapewe ushirikiano na vilabu vyetu. Tujikite pia katika kuwaondoa wachezaji wetu katika umri mwafaka kama ilivyokuwa kwa Kelvin.

Shukrani kwa sasa tuna makinda kama Ali Ng’anzi anayecheza Marekani na Ally Msengi ambaye anatamba katika soka la Afrika Kusini kwa sasa. Tukiwa na vijana hawa wengi nje katika umri mdogo kuna uwezekano wakatupunguzia maumivu kama haya ambayo Samatta ametuletea.

Kumtegemea mchezaji mmoja ni kosa ambalo tumeendelea kulifanya kwa muda mrefu tangu Samatta akiwa TP Mazembe. Ni hili ndilo ambalo limetugharimu kwa sasa na limetutia hasira.

Vipi kama Ajibu na wengine wangekuwa wametimba Ligi Kuu ya Ufaransa kwa sasa. Tungekuwa na hasira hizi?

Wazee wa zamani, wakati fulani walikuwa watu wa masihara, ila walikuwa wanasema kweli pale walipotetea maamuzi yao ya kuzaa watoto wengi.

Walikuwa wanasema kuzaa mtoto mmoja kulikuwa ni kujihatarisha katika siku za usoni. Vipi kama Mungu akimtwaa?