JICHO LA MWEWE : Uchebe hajui kilichompiga, amejikuta kazimia

Muktasari:

Kuna mengi yamemuondoa ambayo hayafahamu. Kwanza nasikia alijifanya ni rafiki wa bosi wa timu kuliko viongozi wengine. Kwa sababu aliletwa na bosi, basi hakutaka urafiki na watu wengine. Alikuwa ana namba za bosi wake tu. Wengine ‘aliwadeliti’. Watanzania hauwezi kuishi nao hivi.

MZUNGU anayeitwa Uchebe anatapatapa kwa sasa mitandaoni. Jina lake kamili ni Patrick Aussems. Juzi katika akaunti yake ya Instagram nimemuona akiwa ameposti ngao yake ya hisani aliyotwaa na kikosi cha Simba mwanzoni mwa msimu huu. Uchebe bwana!

Ulikuwa ni ujumbe wake kwa mabosi wa Simba waliomtimua kazi asubuhi yake, kwamba alikuwa anawaonyesha kuwa wamemfukuza katika msimu ambao alitwaa kitu, kwamba wamemfukuza huku timu yake ikiwa inaongoza ligi.

Uchebe bwana! Nadhani anatafakari na hajui kitu kilichompiga usoni. Alikuwa halijui vyema soka la Tanzania. Mpira wa Tanzania haupo kama anavyofikiri. Kuna mambo mengi yamemuondoa nyuma ya pazia. Anaweza kuposti chochote anachojisikia lakini Simba usemi wao ni ule ule wa majirani zao Yanga. Daima mbele nyuma mwiko. Wakati Yanga wakilisema hili midomoni, Simba huwa wanalisema mioyoni.

Kuna mengi yamemuondoa ambayo hayafahamu. Kwanza nasikia alijifanya ni rafiki wa bosi wa timu kuliko viongozi wengine. Kwa sababu aliletwa na bosi, basi hakutaka urafiki na watu wengine. Alikuwa ana namba za bosi wake tu. Wengine ‘aliwadeliti’. Watanzania hauwezi kuishi nao hivi.

Lakini pia Uchebe hakujua kwamba zile bao tano ambazo Simba ilifungwa mara mbili Kinshasa na Cairo hazijawahi kuwatoka akilini Wanasimba. Zile tatu za Algeria zipo katika akili zao lakini zile tano mara mbili zilimuondoa kibaruani siku nyingi tu.

Baada ya usajili wa ‘mabilioni’ ambao ulisababisha Simba wawatambie sana watani zao wa pale Jangwani, zile tano ziliwakosesha raha kwa kiasi kikubwa. Wengine waliumia bila ya hoja, lakini wengine waliumia kwa hoja. Niliafiki mawazo ya baadhi ya mabosi kuhusu kocha kukosa mbinu katika mechi za ugenini.

Simba ilicheza na Vita pale Kinshasa kama vile ipo nyumbani. Ilicheza na Al Ahly pale Cairo kama vile ipo nyumbani. Hata walipofungwa Algeria walikuwa wanacheza kama wapo nyumbani. Walikuwa wanacheza kama timu kubwa badala ya kukubali nafasi yao kwamba wao ni timu ndogo na walipaswa kucheza katika nidhamu ya ulinzi. Hawakufanya hivyo.

Wakati huo Bwana Aussems alikuwa ‘anajimwambafai’ kwamba ameifikisha Simba hatua ya makundi. Hata hivyo, mabosi wake katika vikao vya baa walikuwa wanatuambia ‘wanajua jinsi walivyoifikisha Simba hatua hiyo’. Unapofika katika mjadala huu Bwana Uchebe alikuwa anawekwa kando.

Uchebe alikuwa hajui kwamba kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwafanya wachezaji wawe fiti. Masuala ya ushindi yana mambo mengi nje ya uwanja. Kujigamba kwake kulikuwa hakuna maana yoyote mbele ya mabosi wa Simba.

Na hata mkataba wake ulipofika mwisho mabosi wengi waliafiki asiongezewe mkataba. Ni bwana mkubwa mwenye pesa zake, na anayemlipa, ndiye ambaye alimkingia kifua vyema. Akamuongezea mkataba.

Kwa sasa Simba inaongoza ligi, lakini Aussems anapaswa kujua kwamba Simba iliacha kuhesabu ligi ya Tanzania kuwa mafanikio misimu miwili iliyopita. Ninachojiuliza ni mambo mawili. Nani aliingilia uhusiano wake na tajiri? Nasikia siku za mwisho tajiri alikuwa hapokei simu zake. Badala yake alikuwa anamwambia aongee na bosi mtendaji kutoka Sauz.

Huyu bosi mtendaji kutoka Sauz hana mapenzi makubwa na Wazungu. Historia ya nchi yake dhidi ya Wazungu wote tunaifahamu. Kwahiyo huu ulikuwa mwanzo wa mwisho wa Bwana Uchebe. Lakini swali jingine ninalojiuliza, Simba walichelewa wapi kuacha naye tangu walipotolewa na wale Wamakonde wa Msumbiji? Kilitokea nini wakaendelea kuwa naye?

Na sasa mashabiki wamesahau kutolewa kwao na Wamakonde na wamerudi katika ligi na ndio maana kila wakitazama msimamo wa ligi hawaoni sababu ya kumuondoa. Ndio maana anapata nguvu ya mashabiki. Usiwashangae sana mashabiki wa Tanzania. Ni hawahawa ambao walikuwa wanataka Uchebe aondoke na nafasi yake apewe Masoud Djuma. Mpira wetu bwana! Leo hawataki aondoke.

Hii ‘timing’ mbovu ndio ambayo imewatesa viongozi kuachana na Uchebe. Unaongozaje ligi halafu unafukuza kocha?

Haukuwa wakati sahihi lakini nasikia kuna maudhi yalikuwa yanaendelea katika kambi ya Simba ambayo yaliamsha hasira zao za muda mrefu. Haya mambo kama vile kocha kutotaka kambi, kuwa mshkaji wa wachezaji na mengineyo yamemaliza muda wa Aussems Tanzania lakini ukweli kwamba mwanzo wa mwisho wake ulianza zamani tu. Zamani sana kabla hajasaini mkataba mpya.

Kitu kingine ambacho Bwana Uchebe hakufahamu ni kwamba hajalishi unafanya mambo mazuri kiasi gani katika klabu zetu lakini huwa tuna tabia tu ya kuchoka sura za makocha, na hata wachezaji.

Basi tu tunaamua kwamba mwisho wako umefika. Tunataka sura mpya. Hata sisi watu wa magazeti huwa tunafurahi kocha akifukuzwa kwa sababu stori ya ujio wa kocha mpya huwa inauza zaidi magazeti kuliko za kocha aliyepo.

Kama anabisha katika suala hili akamuulize rafiki yake Mwinyi Zahera. Alikuwa anadhani Yanga ni ‘watu kwelikweli’. Walimsapoti hata kwa kuvaa vipensi wakati alipoingia matatizoni na TFF. Leo yuko wapi?