JICHO LA MWEWE : Taifa Stars inazidi kuwa mwili wa baunsa

Muktasari:

  • Mbele unaweza kuanza na Samatta, Msuva na Ulimwengu. Hapo katikati lazima wajae kina Jonas Mkude, Himid Mao na Feisal Salum. Viungo asilia. Hapo katika ushambuliaji ina maana nje watakuwepo Kichuya, Zayd, Farid, Chilunda na Mandawa. Kama kuna mabadiliko basi wanaweza kuingia wawili. Wengine watakuwa jukwaani.

NILIKUWA nakiangalia kikosi chetu cha timu ya taifa kitakachoivaa Uganda Machi 22. Kocha Emmanuel Amunike amewaita mastaa wake wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi. Amejivunia kwelikweli mastaa hao. Dalili za kukua kwa soka letu.

Nina wasiwasi na mambo machache. Kuna tatizo ambalo sio la Amunike na kuna tatizo la Amunike. Wachezaji wengi wanaocheza nje ambao wameitwa wanacheza nafasi ya ushambuliaji. Timu imekosa uwiano. Kuna wachezaji kati yao nadhani Amunike amelazimisha kuwaita. Inawezekana sio yeye, bali watu waliomzunguka

Eneo la ushambuliaji timu ina Mbwana Samatta, Farid Mussa, Shaaban Chilunda, Shiza Kichuya, Rashid Mandawa, Simon Msuva, Yahaya Zayd, na Thomas Ulimwengu. Hapa sijamtaja John Bocco ambaye ameitwa lakini anacheza nyumbani.

Baadhi yao wameandikwa kama viungo. Ni kweli, katika dunia ya soka la kisasa mawinga nao ni viungo. Hata hivyo, kwa soka la kisasa zaidi unahitaji viungo watimilifu watatu eneo la katikati na mbele unaweza kuchezesha washambuliaji watatu katika mfumo wa 4-3-3.

Mbele unaweza kuanza na Samatta, Msuva na Ulimwengu. Hapo katikati lazima wajae kina Jonas Mkude, Himid Mao na Feisal Salum. Viungo asilia. Hapo katika ushambuliaji ina maana nje watakuwepo Kichuya, Zayd, Farid, Chilunda na Mandawa. Kama kuna mabadiliko basi wanaweza kuingia wawili. Wengine watakuwa jukwaani.

Viungo asilia kwa hapo wapo wanne tu. Himid Mao, Mudathir, Feisal Salum na Mkude. Ina maana timu ina viungo asilia wanne halafu ina washambuliaji tisa. Mmoja ndio anacheza nyumbani. Nadhani wachezaji wengi wa nafasi ya ushambuliaji watakuja kufanya mazoezi tu kikosini.

Wakati mwingine sio mbaya kwa sababu inawakatisha tamaa wachezaji wetu wa ndani ambao akili zao zimelala. Inabidi waamke na kugundua kwa sasa ni vigumu kuitwa Stars kama unacheza soka nyumbani. Haijalishi unafunga kwa kiasi gani.

Hata hivyo, wakati umefika kwa Kocha Amunike kuanza kuwazungukia wachezaji wake wanaocheza nje kwa ajili ya kujua fomu zao. ndivyo wanavyofanya wenzetu. Tunakaribia kukipita kigezo cha kwamba ukicheza nje inabidi uitwe. Inabidi tufike mahala tujue huko unakocheza upo katika hali gani.

Hivi ndivyo ambavyo makocha mbalimbali wa timu za taifa wanavyofanya. Hata katika taifa ambalo Amunike ametoka huwa wanafanya hivyo kwa sababu kuna mastaa wengi wa Nigeria wanaocheza nje ambao wanatamba na hauwezi kuwaita wote 100.

Tukiachana na suala hilo ni wazi kwa sasa inabidi tuwaamshe wachezaji wa nafasi nyingine nao wakacheze nje. Katika nafasi muhimu kama ya ulinzi kuna mchezaji mmoja tu wa anayecheza nje, Hassan Kessy. Upande wa kushoto Abdi Banda ameachwa.

Uzoefu mkubwa wa soka la kulipwa nje ya mipaka yetu unahitajika kwa wachezaji wa nafasi ya ulinzi. Kuanzia kwa kipa, Aishi Manula na mabeki wake kulikuwa na umuhimu mkubwa wa kupata wachezaji wanaocheza nje katika maeneo hayo. Ni maeneo nyeti.

Wakati fulani nilizungumza na Samatta ambaye alionyesha tamaa ya kumuona Aishi akidaka katika klabu kubwa zaidi barani Afrika kwa sababu uwezo anao, lakini pia atajifunza mambo mengi kwa kucheza ligi ngumu zaidi.

Timu yetu kwa sasa imekuwa kama mwili wa baunsa. Mara nyingi mabaunsa juu wanakuwa na maumbili makubwa lakini miguu yao inakuwa midogo. Taifa Stars ina watu wanaotisha pale mbele kama Samatta na Msuva lakini hakuna wachezaji wa aina hiyo katika safu ya ulinzi. Wachezaji wanaotisha nje ya mipaka.

Tunawategemea baadhi ya mabeki wazoefu katika soka la ndani lakini ukweli ni kwamba wenzetu wetu wanaotuzunguka katika ukanda huu wana mabeki wanaocheza katika soka la kulipwa nje ya mipaka yao wakitamba katika klabu mbalimbali zinazoshindana kimataifa.

Mabeki wetu katika miaka ya karibuni wamekuwa wakipata nafuu kucheza na washambuliaji wa ndani ambao hawawapi mikikimikiki. Zinapokuja mechi za kimataifa tunajikuta tunaathirika.

Hili sio tatizo la Kocha Amunike. Ni tatizo letu wenyewe. Tatizo la wachezaji wetu huku pia likiwa ni tatizo la soka duniani kote.

Washambuliaji wanatazamwa kwa haraka zaidi kuliko mabeki. Timu nyingi zina matatizo ya ufungaji au utengenezwaji nafasi kuliko ilivyo kwa tatizo la safu za ulinzi. Ndio maana kina Kichuya wote wanaondoka.

Sijui tutakabiliana vipi na hili tatizo lakini nadhani ingekuwa vizuri kama warithi wa kina Agrey Morris na Kevin Yondani wangekuwa wanatoka nje.

Tangu Taifa Stars ilipoanza kuundwa kwa mtazamo mpya katika utawala wa Marcio Maximo mabeki wote wa kati huwa wanatoka katika ligi ya ndani.

Hilo eneo muhimu kwa kutoa viongozi uwanjani. Hao watu wa eneo hilo ndio ambao huwa wanakabiliana na kina Sadio Mane au Mohamed Salah wakija nchini.

Kunahitaji uzoefu mkubwa katika eneo hilo. Sijui tutaweza kutatua vipi.