JICHO LA MWEWE : Kwanini tuna hofu na kina Mane, Mahrez?

Muktasari:

  • Katika makundi kama ya Afcon hauwezi kupata kundi lenye Tanzania, Malawi, Somalia na Kenya. Utapata kundi kama hili. Ukihepuka kundi hili unaweza kupangwa na Nigeria na Misri. Au unaweza kupangwa na Ivory Coast na Tunisia. Kuna mengi ya kufikirika katika kundi hili la Algeria na Senegal.

KWAHIYO tumepangwa na Sadio Mane, Riyad Mahrez na Victor Wanyama sio? Ndivyo walivyopanga wakubwa pale Misri Ijumaa iliyopita. Taifa Stars itakwenda kucheza na Senegal, Algeria na majirani zetu Kenya.

Tulitegemea nini zaidi wakati tunashangilia Cape Verde kutoka sare na Lesotho pale Praia halafu Stars kuifunga Uganda mabao matatu uwanja wa Taifa? Tulitegemea tunafuzu kwenda Afcon na kisha kucheza na wakubwa kama hawa.

Kundi lolote kwa Taifa Stars lingekuwa gumu. Sio kwa bahati mbaya kwamba tumekaa miaka 39 bila ya kushiriki michuano hii. Ilitokana na kiwango chetu kuwa kibovu kila kukicha. Tukaenda chini zaidi katika viwango vya Fifa.

Katika makundi kama ya Afcon hauwezi kupata kundi lenye Tanzania, Malawi, Somalia na Kenya. Utapata kundi kama hili. Ukihepuka kundi hili unaweza kupangwa na Nigeria na Misri. Au unaweza kupangwa na Ivory Coast na Tunisia. Kuna mengi ya kufikirika katika kundi hili la Algeria na Senegal. Kwanza kabisa wachezaji wetu watavaa suti na kwenda Cairo kufurahia kuwepo tu katika michuano hii. Jambo la kwanza kabisa ni wachezaji kufurahia kuwepo. Kitu cha msingi zaidi ni kuhakikisha tunarudi mara nyingi katika michuano hii.

Tuna nafasi finyu ya kusonga mbele lakini tusijali sana. tulitaka kuwepo kwanza pale Misri na kushiriki. Inarudisha kujiamini kwa wachezaji wetu wa sasa na wale ambao wapo nje ya Taifa Stars wakiwa kama vijana kwa sasa na wanaamini siku moja watakuja kuchezea Stars.

Lakini hapo hapo hakuna haja ya kuogopa sana. kwanini tunaogopa? Kwa sababu kuna majina makubwa pale Senegal na Algeria. Lakini tuna sababu za kujifariji. Senegal imeshiriki michuano hii mara 15 na haijawahi kuchukua.

Algeria wamewahi kuchukua mara moja tu. mwaka 1990. Walikuwa wapi hawa wakubwa kutawala michuano hii na mara zote wanashiriki? Ni swali la kujiuliza. Sawa wana mastaa wengi wakubwa wanaocheza nje, lakini mbona rekodi zao katika michuano hii ni mbovu?

Kuna jibu moja rahisi. Wachezaji wa Afrika ni wazuri pindi wanapochanganyika na wazungu katika timu zao za Ulaya. Wanapokusanyika wenyewe wanakuwa na walakini. Wanakosa nidhamu na uwezo wao binafsi unapungua pia.

Sadio Mane wa Liverpool ni tofauti na Sadio Mane wa Senegal. Haishangazi kuona kila siku mashabiki wa Senegal wanamzoea. Wanaamini kwamba hajitumi sana. lakini inawezekana kwamba anacheza na watu tofauti pale Anfield.

Mashabiki wengine wana hofu kutokana na kichapo cha mabao 7-0 ambacho Stars walipokea kutoka kwa Algeria miaka ya karibuni. Mpaka leo naamini kichapo kile hakikutokana na ubovu wa Stars. Kilitokana na mbinu za kocha wa wakati ule, Charles Boniface Mkwasa. Alikwenda Algeria bila ya kuwaheshimu Algeria.

Katika mechi ile aliwapanga kwa pamoja, Mbwana Samatta, Elius Maguri, Simon Msuva na Thomas Ulimwengu. Aliwapanga viungo wawili tu, Mudathir Mudathir na Himid Mao. Ugenini dhidi ya Algeria unawaanzisha washambuliaji wanne unategemea nini?

Kama kocha, Emmanuel Amunike akizicheza mechi hizi kwa nidhamu kama alivyofanya katika pambano dhidi ya Uganda pale Kampala Taifa Stars inaweza kupata kitu. Sio lazima kushinda, lakini inaweza kuhepuka vipigo vya aibu na inaweza pia kuambulia sare dhidi ya wakubwa hawa.

Ni suala la kujitambua katika nguvu zako na kutambua nguvu za adui. Tulichomlaumu Amunike katika mechi dhidi ya Lesotho ni pale alipoamua kuwaheshimu Lesotho kama vile anacheza dhidi ya Algeria au Senegal. Alikosea. Hizi ndio mechi hasa ambazo Amunike inabidi acheze kwa kujihami na kwa nidhamu kubwa. Zama za kufungwa 8-0 zimepita miaka mingi iliyopita.

Labda Amunike aamue mwenyewe tu. mpira wa kisasa upo katika karatasi na tunaweza kusumbua vigogo.

Pamoja na hawa wawili ambao tunaweza kuwazungumzia sana lakini tusiwasahau ndugu zetu Kenya. Rafiki yetu Victor Wanyama amekuwa akija hapa nchini katika likizo zake lakini yeye na wenzake hawatakuwa na urafiki na sisi.

Na wao wanatuona sisi kama sehemu ya kuchukulia pointi zao muhimu. Wana wachezaji wengi ambao wanacheza nje na wana uwezo mkubwa. Kitu cha ajabu katika soka ni kwamba tunaweza kuwabania wakubwa halafu tukaja kufungwa kiurahisi na Kenya.

Mwisho wa siku twendeni Misri tukafurahie soka. Tukafurahie kuona wachezaji wetu wanapewa hadhi ya kukaa hoteli nzuri, kiwanja kizuri cha mazoezi, kupigiwa wimbo wa Taifa kabla ya mechi kuanza na mengineyo.

Wachezaji wetu wa ndani pia wanaweza kujiuza vema katika michuano hii. Ni wakati wa akina Fey Toto kukaa sokoni. Hatuna jambo ya kuhofia. Mwaka 1933 Rais wa zamani wa Marekani, Franklin D. Roosevelt aliwahi kusema ‘Kama kuna kitu kikubwa cha kuhofia basi ni kuihofia hofu yenyewe’. Kwanini tuna hofu na Mane na Mahrez?