JB ataja ugomvi wake mkubwa na Wema

Muktasari:

Wema Sepetu ametimiza miaka 30 jana Ijumaa na sherehe yake imehudhuriwa na wasanii mbalimbali huku  sherehe hiyo ikiambatana na uzinduzi wa filamu yake mpya.

Msanii wa filamu, Jacob Steve ‘JB’ amesema ugomvi wake mkubwa na msanii mwenzake Wema Sepetu ni kutowahi kuamka asubuhi.

Jb ambaye hivi karibuni alitangaza kustaafu kuigiza, aliyafungikia hayo katika sherehe ya kuzaliwa Wema Sepetu iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Amesema tabia hiyo humfanya Wema kupata tabu ya kucheza ‘scene’ za asubuhi pale anapohitajika kufanya hivyo.

Amesema kwake Wema ni msanii mzuri, kwani mbali na kuweza kuuvaa uhusika ni mwepesi katika kushika script kichwani tofauti na watu wengine.

“Miaka 20 niliyokaa kwenye tasnia nimekutana na wasanii mbalimbali, ambao wengine unalazimika kuwamezesha script hata mara kumi lakini sio Wema. Halafu ukija kwenye kuuvaa uhusika ndio usiseme na hili hulimudu kila uhusika anaoangiwa,”amesema JB.

Hata hivyo amebainisha kuwa kwa kuwa yeye humchukulia kama mtoto wake huwa hachoki kila mara kumkumbusha umuhimu wa kuamka asubuhi hususani pale anaohitajika kufanya kazi.

Filamu alizowahi kucheza JB na Wema ni pamoja na ‘Chungu cha tatu’, Senia Bachelour na 14 Days.