JAMVI LA KISPOTI : Hata Ndayiragije,Matola watafelishwa tu

Friday August 2 2019

 

By Khatimu Naheka

Tanzania tunahitaji maendeleo ya soka na kiu hii ipo kwa wananchi wengi ambao wanatamani siku moja kuona tunaishi katika maisha ya watu wa Cameroon, Nigeria, Algeria na hata Misri.

Kiu hii inatutesa wengi, lakini wakati tukiwa na shauku hiyo, bahati mbaya sana hatujajua tunakosea wapi katika kuondoka sehemu tulipo na tufike tunapotaka kufika.

Bahati mbaya zaidi kila mmoja amekuwa mjuaji wa safari tunayotaka kuianza na karibu kila mwenye kiu hiyo amekuwa dereva wa gari tunalotaka kutumia katika safari hiyo.

Wengi wamekuwa wajuaji kuliko dereva ambaye tunamchagua ili atuendeshe kuelekea sehemu ambayo zipo Misri na wengine. Na kuna wakati tunafikia hata kuwatusi madereva sahihi kwa kutojua kwetu tukidhani tunajua.

Sasa kikosi cha Taifa Stars kipo chini ya makocha wa muda, Ettiene Ndayiragije na mzawa Suleiman Matola ambao dhamana yetu ipo mikononi mwao kutupeleka tunapotaka.

Ndayiragije na Matola wanakuja kusaidia na kuendeleza walipoishia Mnigeria Emmanuel Amunike na msaidizi wake Hemed Morocco ambao baada ya Fainali za Mataifa Afrika (Afco) ajira zao ziliishia hapo kwa kuondolewa.

Advertisement

Bahati mbaya inawezekana hata Ndayiragije na Matola hawajajua tunakwama wapi, lakini kama wanajua itakuwa ni fursa nzuri kwetu kubadilika. Tanzania licha ya kukosa mipango sahihi katika soka, shida nyingine inayotusumbua ni kupenda zaidi klabu zetu badala ya maendeleo ya taifa.

Kikubwa kitakachowakwamisha kina Ndayiragije ni maisha ya klabu za Simba na Yanga ambazo mashabiki wao juu ya wachezaji wa timu hizo ndiyo tatizo kubwa.

Amunike alichokosea ni kuwa mkali kwa wachezaji kutoka timu hizo alipoona upungufu wao na kuamua kuwaambia ukweli.

Ukweli huo ndio ulikuwa mwiba kwake na maisha yakageuka na kuambiwa amewatukana wachezaji - tena matusi makubwa na hafai kuendelea kufundisha timu yetu.

Shida katika soka letu, licha ya Amunike kudiriki hata kuomba vyombo vya habari kwamba tuwaambie ukweli wachezaji, lakini maisha yetu hayataki ukweli hata kidogo.

Ukishauzungumza ukweli tambua kwamba kesho maisha yako yatapunguza siku kama mgonjwa wa kansa na kuanza kuandamwa na matatizo ya hapa na pale. Tayari shida ya wachezaji wa Simba na Yanga imeanza kujitokeza katika utawala wa Ndayiragije ingawa hataki kusema.

Wachezaji wetu hawana nidhamu, inamlazimu kocha kuchagua kusuka au kunyoa - kwa maana akiwa mkali kwao maisha yake yako hatarini kikazi.

Akishawaambia ukweli wachezaji husika watanuna na kwenda kumsema vibaya, na kansa mbaya zaidi kwetu hatuna viongozi wenye weledi nao huanza kuchukia na kuwachukia makocha kutokana na mambo ya namna hii.

Kunyamaza kimya hakuwezi kutufanya kufika katika safari tunayotaka kwenda kwa kuwa ni idadi ndogo sana ya wachezaji wenye nidhamu wamewahi kupenya kwenda katika kundi la mafanikio.

Wengi hukwama kama tunavyokama sisi na kupiga hatua mbili mbele na kurudi tatu nyuma, na haya ndio yamekuwa maisha yetu ya kila siku.

Shida yetu hapa sio kocha, bali ni mfumo wa maisha tuliyoyachagua kwa kupenda zaidi klabu zetu.

Hapa tunaweza kumfukuza kocha hata kwa kosa la kuwaita wachezaji wengi wa Azam badala ya Simba au Yanga. Tunaweza kumtimua kocha kwa kosa la kuwaita wachezaji wengi wa Simba, akamchukua mmoja wa Yanga kwa kuwa kila shabiki anajua mpira kuliko makocha na kusahahu huchagua wachezaji kulingana na mifumo wanayotaka kutumia.

Safari hii imekuwa ngumu kwetu kutokana na mahaba hayo - tena wakati mwingine yanaweza hata kuanza kutokea kwa viongozi wa soka.

Inatokea hata kocha kueleza utovu wa nidhamu wa mchezaji husika na watu wakaona kabisa hoja yake, lakini baadaye ikageuzwa kuwa mchezaji husika anachukiwa badala ya kuandamwa.

Hili ndilo linalotumaliza katika soka letu na bahati mbaya naona hata Ndayiragije na Matola nao watakwama kutokana na na shida hiyo ya wachezaji wetu ambao wengi hawana hadhi ya kulisaidia taifa.

Kwa sasa timu yetu imekwishaanza michuano ya kuwania kufuzu kwa michuani ya Chan itakayopigwa huko Cameroon mwakani, lakini tayari zinasikika chokochoko za maneno maneno ya ajabu ajabu mitaani kuhusu kikosi chake.

Tumeshindwa kuuona uzalendo katika suala la timu yetu ya taifa kwa kuipa moyo, badala yake tunapambana kutana kuifelisha kila mara ili hoja zetu dhaifu zionekane kuwa na nguvu dhidi ya makocha. Kwa mtindo huu hatutafika.

Advertisement