JAMVI LA KIPOTI : Safari Cameroon imeanza, nawasubiri wanasiasa

Muktasari:

Wabunge mbalimbali walionyeshana umahiri wa kukosoa sana bila kujiangalia kosa liliania wapi katika anguko hilo la Stars.

Ratiba kamili ya mechi za kuwania kufuzu Fainali zijazo za Mataifa Afrika imeshatoka na timu yetu kama kawaida ipo safarini kuwania tiketi hiyo.

Tanzania kupitia Taifa Stars imepangwa kundi moja pamoja na mataifa ya Tunisia, Guinea ya Ikweta na Libya na katika kundi hilo zikihitajika timu mbili kufuzu.

Safari hiyo inakuja wakati Taifa Stars inatoka kushiriki fainali zilizopita nchini Misri ikiangukia pua baada ya kupoteza mechi tatu zote katika kundi lao. Baada ya kupoteza mechi moja tu ugeni wa mashindano ukaibuka na kila mmoja kuzungumza lake juu ya timu hiyo wakikosoa na kupongeza.

Ikumbukwe ushiriki wa Stars katika fainali hizo ilikuwa ni mara ya pili baada ya kupita miaka 39 tangu tulipofuzu fainali za kwanza.

Kufanya vibaya kwa Taifa Stars kundi moja lilizua gumzo katika kukosoa kwake kutoka kwa wanasiasa wetu hasa wabunge ambao walitoa kauli nyingi.

Wabunge mbalimbali walionyeshana umahiri wa kukosoa sana bila kujiangalia kosa liliania wapi katika anguko hilo la Stars.

Hakuna nchi ambayo ilipiga hatua na inapiga hatua mpaka sasa kwa timu yao ya taifa bila nguvu ya serikali ya nchi husika.

Inawezekana ikawa ni nchi yetu tu tunataka kupata mafanikio katika soka bila serikali kuweka nguvu ya kweli na sio siasa. Hapa kwetu mpango kamili wa ustawi wa timu za taifa ulitakiwa kuanzia bungeni ambako ndiko mipango mingi ya kimaendeleo hupangwa.

Stars na anguko lake haikuwa na fungu lolote kutoka serikalini na mambo mengi yaliachiwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hata nchi hizo zinazofanya vizuri inajulikana kwamba mashirikisho yao yanapokea fedha nyingi ambazo kimsingi nyingi hutoka mara baada ya mashindano kumalizika.

Nchi yetu tu ndiyo wanasiasa walijiandaa kuona Stars inafanya vizuri bila ya kuwa na maandalizi.

CAF tayari imeshatangaza ratiba kamili ambayo sasa ni wakati wa kuona yale yaliyozungumzwa na wanasiasa walikuwa wanamaanisha ama walikuwa wakipimana ubavu na wale wanaosigana nao kisiasa.

Safari ya Stars kwenda Cameroon ipo mikononi mwao na sasa wanatakiwa kuhakikisha wanaibana serikali ili nayo kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo nayo iweke nguvu kubwa kuhakikisha Stars inafanya vyema.

Stars haiwezi kufanya vyema huku ikiishi kwa nguvu ya harambee ya kuchangisha fedha kutoka kwa wadau.

Ni wazi kwamba itafanya vizuri kwa mipango mizuri ya kuweka nguvu kubwa na si kutegemea mipango ya TFF pekee ambao mpaka sasa hawatoshi kutupa mafanikio yanayohitajika.

Hivi sasa tunategemea serikali na hata TFF watakaa pamoja kutengeneza muundo sahihi wa safari ya kwenda Cameroon ili wizara nao waipeleke mbele kuiombea baraka kwa Serikali kuu. Faida za Stars kufuzu kwa mara ya pili ni kubwa ikiwa pia kuona kupitia uzoefu walioupata wachezaji katika fainali zilizopita unatumika vyema katika fainali zijazo.

Huu sasa ni uwanja wa wanasiasa kuonyesha tathmini yao juu ya ubora mdogo wa lishe ya wachezaji, makocha madalali sasa zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili tuweze kufuzu fainali zijazo.

Wakati huohuo tutakuwa tukipambana na hilo pia mipamgo hiyo ya serikali inatakiwa kwenda sambamba na uzalishaji bora wa wachjezaji wa baadaye.

Inawezekana ni Tanzania tu ndiyo tumebaki na siasa wakati majiran zetu wakituacha kwa haraka katika kuwa na mipango thabiti ya maendeleo.

Kinachotukwamisha mipango yetu mingi ipo katika makaratasi na sio utendaji na hapo ndipo aguko letuy linapoanzia na kupotea. Changamoto hii ipo serikalini na mpaka TFF, na baadaye anguko la michezo kwa ujumla linakuja kutukumba na kuanza kulaumiana.

Tunataraji sasa kuona kwenye michezo nako kunaingizwa nguvu kubwa ya kuhakikisha nchi inapiga hatua kwa uhalisia.

Kutofanyika kwa lolote katika katika hili hakutakuwa na maana na zile kelele ambazo zilipigwa pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya kutofanya vyema kwa Stars.

Soka sasa ni ajira rasmi tena ambayo inaweza kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanaweza kuiletea nchi heshima kiama ambavyo sasa inafanyika kwa mshambuliaji wa Stars, Mbwana Samata ambaye amelithibitisha hilo.

Hatuwezi kuwa tunafurahia uwepo wa Sammata wakati hatufanyi juhudi za makusudi katika kuibua vipaji vipya ambavyo vitakuwa ndiyo Stars ya kesho.

Hili litafanikiwa tu kama pale bungeni wataamka na kuwa wapanga sera na mipango sahihi kwa kuangalia hata bajeti ya michezo.