Iwobi mzigoni kusaka rekodi ya miaka 100

Muktasari:

Iwobi, aliyejiunga na Everton akitokea Arsenal anatarajia kuanzishwa kwenye mechi hiyo, huku matumaini mengine kutoka kwa timu hiyo wasifungwe bao ipo kwa kipa wao, Jordan Pickford na safu ya ulinzi ya mabeki Michael Keane, Lucas Digne, Yerry Mina na Seamus Coleman.

ABUJA, NIGERIA. STAA wa Kinigeria, Alex Iwobi huenda akaingia kwenye historia ya Everton wakati leo Ijumaa watakapokipiga na Aston Villa kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England huko uwanjani Villa Park.

Kwenye mechi hiyo kama chama la Iwobi, Everton litafanikiwa kuzuia wavu wake usiguswe basi atakuwa wamefikia rekodi muhimu kwenye timu hiyo iliyodumu kwa miaka 107.

Baada ya kushuka uwanjani mara mbili kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Everton ndio timu pekee ambayo haikuruhusu bao hadi sasa, wakitoka sare ya bila kufungana kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Crystal Palace kabla ya kuwachapa Watford 1-0 kwenye mechi ya pili.

Wakicheza mechi yao ya tatu leo, chama hilo linalonolewa na Marco Silva, kama litafanikiwa kuzuia wasifungwe, basi watakuwa wamefikia rekodi ambayo waliifanya msimu wa 1912-13, ambapo walicheza mechi zao tatu za mwanzo wa msimu bila ya kuruhusu bao kwenye wavu wao.

Iwobi, aliyejiunga na Everton akitokea Arsenal anatarajia kuanzishwa kwenye mechi hiyo, huku matumaini mengine kutoka kwa timu hiyo wasifungwe bao ipo kwa kipa wao, Jordan Pickford na safu ya ulinzi ya mabeki Michael Keane, Lucas Digne, Yerry Mina na Seamus Coleman.

Kwenye mechi iliyopita, Iwobi, alikaa benchi mwanzo mwisho, lakini leo anatarajia kuanza mechi yake ya kwanza ya kiushindani tangu alipotua kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Goodison Park.