Ishu ya straika Mkongo Simba ipo hivi…

MPAKA jana ubao wa usajili ulikuwa unasomeka hivi, mastraika Chris Mugalu na Jesse Were ni Simba na Farid Mussa ni Yanga.

Usajili wa timu mbalimbali za Ligi Kuu umepamba moto huku Yanga na Azam zikionekana kufumua vikosi vyao zaidi ya Simba ambayo bilionea wao, Mohammed Dewji Mo akisisitiza jana; “Timu nzuri hazihitaji kusajili sana.”

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni Simba wamefufua mazungumzo na Mugalu, ambaye ni raia wa DR Congo anayekipiga Lusaka Dynamos ya Zambia na ana nafasi kubwa ya kutua na jana jioni jijini Dar es Salaam walikuwa na kikao ambao jina lake lilikuwa linajadiliwa pamoja na Mkenya, Were anayeichezea Zesco ambaye nafasi yake hata hivyo ni finyu sana na huenda akaibukia Yanga.

Kuhusu dili la Were Simba licha ya yeye kukataa kufafanua lakini Kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo alifichua; “Niliona taarifa hizo zikisambaa nikasema Jesse (Were) ni rafiki yangu nikampigia kujua kama zina ukweli au vinginevyo ameniambia anakuja Simba.”

“Wako katika mazungumzo na viongozi wa Simba na anasema yamefikia pazuri wakati wowote wanaweza kuja kufikia mwafaka na wakamalizana.”

Mbali na hao, Mwanaspoti limejiridhisha Yanga jana ilifanya mazungumzo na Meneja wa Sureboy wa Azam, Herry Mzozo na tayari walipeleka barua jana mchana Chamazi kuhusu nia yao ya kumtaka mchezaji huyo ambaye baba yake ni Yanga damu.

Mzozo alipoulizwa jana alidai kuna watu wa Yanga walimfuata lakini akawaelekeza wazungumze na Azam kwa vile bado mteja wake ana mkataba nao.

Habari zinasema Farid naye tayari yupo Dar es Salaam baada ya klabu ya Tennerife ya Hispania kupitia kikosi cha vijana, kutangaza kumtema rasmi na kumtakia kila la kheri yeye na wenzie sita.

Habari zinasema dili lake na Yanga liko kwenye hatua nzuri ingawa Azam nao wameonyesha tamaa ya kutaka kumrudisha na anawapa pia nafasi. Vigogo wa Yanga jana walikuwa bize na ishu ya Farid na Sureboy na walitarajia kupata hatma usiku wa kuamkia leo kumaliza ishu.

Mpaka sasa usajili uliokamilika Simba ni beki wa kulia David Kameta ‘Duchu’ kutoka Lipuli FC ingawa mabosi hao bado hawajamtangaza rasmi.

Duchu anakwenda kupigania namba na Shomary Kapombe na Haruna Shamte inatajwa huenda akatolewa kwa mkopo ama kama wataafikiana kuvunja mkataba basi itakuwa hivyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alipozungumzia usajili mpya alisema; “Kikosi chetu kina wachezaji ambao wana uwezo, kinachotakiwa ni kuongezewa nguvu ili kocha asipate kazi ya kuanza kufundisha upya, tunahitaji wachezaji ambao wataitoa Simba pale ilipoishia Ligi ya Mabingwa Afrika.”