Ishu ya Niyonzima na Okwi

Saturday January 13 2018

 

SIMBA ambayo jana Ijumaa imeanza mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari, Dar es Salaam, ilikuwa na matumaini makubwa na nyota wao ghali, Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi. Wekundu hao wa Msimbazi ambao, wanajiandaa na mechi ngumu dhidi ya Singida United, sasa imeamua kukimbilia nje ya jiji ili kujiweka sawa na mchezo huo wa Alhamisi.

Hata hivyo, tayari Wanasimba wanaamini ni kama vile wameliwa fedha zao katika usajili wa wachezaji hao kwa namna wanavyotumia muda mwingi nje ya uwanja.

Nyota hao ndio waliosajiliwa kwa dau nene la zaidi ya Sh 100 milioni katika dirisha la mwishoni mwa msimu na mashabiki wa klabu hiyo walitarajia wangeifanyia makubwa, hasa baada ya Okwi kuanza kutupia mabao manne katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting. Okwi amefunga mabao manane hadi sasa katika Ligi Kuu na ndiye kinara.

Lakini, mambo yamebadilika baada ya Okwi na Niyonzima kuumia kwa nyakati tofauti na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, wakati huu timu ikipambana kurejesha heshima katika mechi zake za Ligi Kuu Bara ambayo wapo kilele mwa msimamo kwa sasa.

Ishu ya nyota hao kukosekana kwenye kikosi cha timu hiyo inalipasua kichwa kwa benchi la ufundi chini ya Kocha, Masudi Djuma kutokana na ukweli kwamba, huduma zao zinahitajika sana kwa sasa katika Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.

Mwaka huu Simba itaiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa tangu walipocheza Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa raundi ya awali mwaka 2013.

Simba imepangwa kuanza mechi za raundi ya awali na timu ya Jeshi ya Gendemarie National ya Djibout kati ya Februari 7-18, huku mashabiki wakiwa na kiu ya kuona timu yao ikivuka hapo na kutinga raundi ya kwanza na kucheza ama na Green Buffaloes ya Zambia ama Al Masry ya Misri.

Ni hivi. Awali Simba, ilipanga kuwapa mapumziko nyota wake wote baada ya kutolewa katika Kombe la Mapinduzi, lakini ghafla jana asubuhi walianza tizi, baada ya Djuma kutaka kuweka mambo sawa kabla ya kuivaa Singida.

Hata hivyo, Djuma na wasaidizi wake wa benchi la ufundi wanaumizwa na Niyomzima na Okwi kushindwa kuhudhuria mazoezi hayo kutokana na kusumbuliwa na majeraha kwa muda mrefu.

Niyonzima hajapona na ameliambia Mwanaspoti kuwa, anaendelea mazoezi mapesi huku akiwa chini ya uangalizi wa daktari wake, ambaye ndiye atakayeampa ruksa ya kurejea uwanjani, huku Okwi akiwa hajarejea kutoka kwao Uganda.

“Bado nafanya mazoezi mwenyewe na sijaweza kurudi uwanjani. Sijawa fiti kiasi na ndio sababu nafanya mazoezi mepesi chini ya uangalizi,” alisema.

Kuhusu Okwi mpaka sasa viongozi wamekuwa wakikwepa kufafanua kwa nini raia huyo wa Uganda ameshindwa kurejea nchini wakati Djuma alishaagiza mapema arejee ili awe na wenzake hata kama hachezi kwa kuwa ni majeruhi.

“Sijajua kwanini Okwi hajarejea mpaka sasa, kwa kweli haipendezi. Nilitaka awe huku ili tumuangalie kwa ukaribu wakati akijiuguza,” alikaririwa Djuma ambaye anakaimu nafasi ya Kocha Mkuu akichukua mikoba ya Joseph Omog aliyetimuliwa hivi karibuni.

Hata hivyo, Mratibu wa Simba, Abbas Ali, alipotafutwa ili kueleza ni vipi wachezaji hao hawapo mazoezini kama wenzao, alisema wamekosekana kikosini kutokana na majeruhi na hakuna kitu kingine kinachowakwaza, japo ni kukosekana kwao ni pengo kwa timu yao.

“Ninachofahamu kuhusu Niyonzima na Okwi hawapo kwa sababu ni majeruhi, Niyonzima anaweza kuwa sawa siku yoyote kuanzia sasa, ila sijui ni lini atarudi uwanjani. Daktari ndiye anayejua zaidi. Ni kama suala la Okwi,” alisema.

Daktari Yassin Gembe, hakupatikana ili kufafanua kuhusiana na suala la wachezaji hao kwani, katika mazoezi ya jana asubuhi mabosi wa Msimbazi walikataa waandishi kwa kile kilichoelezwa ni maelekezo toka kwa viongozi wa juu.

Lakini, mmoja ya watu wa karibu na Simba, alilidokeza Mwanaspoti kuwa, ishu ya Niyonzima na Okwi kuwa nje, inawaumia WanaSimba na kuamini ni kama wameliwa fedha zao tu na hasa kwa Niyonzima aliyesajiliwa kwa mbwembwe kutoka Yanga.

“Ukiangalia Ibrahim Ajib anavyofanya vizuri Yanga, kisha ukalinganisha na kazi aliyoifanya Niyonzima mpaka sasa, unaweza kubaini ni kama tumeliwa, ila wakuu wameamua kukauka. Na suala la Okwi limewagawa, ila inafichwa,” kilidokea chanzo hicho.

Manula freshi

Katika hatua nyingine, kipa Aishi Manula aliyefunga ndoa hivi karibuni amesharejea kikosini kujiunga na wenzake katika mazoezi ya jana yaliyofanyika chini ya ulinzi mkali.

Katika mazoezi hayo alikuwa karibu na mchezaji mwenzake wa zamani wa Azam, Shomari Kapombe, ambaye amerejea kutoka kwenye majeraha, wakipiga stori mbili tatu huku wakionyesha sura za bashasha muda mwingi.

Manula aliyekosa mechi zote za Kombe la Mapinduzi, alifunga ndoa wikiendi iliyopita na mchumba wake wa muda mrefu, Aisha katika harusi ya kukata na shoka iliyofanyika mjini Morogoro.