Ishu ya Manji, Simba na vita ya TFF zimebamba 2018

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuleta baadhi ya mambo yaliyotokea ndani ya mwaka huu ambayo yatakumbukwa kutokana na kusisimua mashabiki wengi.

MWAKA 2018 umebakia na siku chache tu kabla ya kumalizika na kuupisha mwaka mpya wa 2019. Ndani ya mwaka 2018 kuna mambo mengi ya kukumbukwa yaliyojiri kuanzia Januari hadi sasa, hususan kwenye michezo hasa soka.

Mwanaspoti linakuleta baadhi ya mambo yaliyotokea ndani ya mwaka huu ambayo yatakumbukwa kutokana na kusisimua mashabiki wengi.

YANGA YAANDIKA REKODI

Waliokuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara tatu mfululizo, Yanga iliandikisha rekodi ndani ya 2018, baada ya kukubali kulitema taji mapema katika ligi ya nyumbani, Vijana wa Jangwani walifanya kweli michuano ya Afrika.

Yanga ilitinga kwa mara ya pili katika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutemwa kutoka Ligi ya Mabingwa Afrika na Rolling Township ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1. Awali iliitoa Welayta Dicha ya Ethiopia.

Wababe hao soka walitinga hatua hiyo Aprili, ikiwa ni mara yao ya pili kucheza makundi ya shirikisho, ya kwanza ikiwa 2016, pia ilikuwa ni mara ya tatu kufika hatua hiyo kwani 1998 iliandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

SIMBA YAOSHA NYOTA NA MFARANSA

Mwezi mmoja baada ya Yanga kulitema taji la ubingwa wa Ligi Kuu, Simba iliosha nyota Mei na kubaki mwezi wa kukumbukwa kwa klabu hiyo na mashabiki wake.

Timu hiyo, ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu iliousotea kwa miaka mitano kwani mara ya mwisho kutwaa taji hilo ilikuwa kwenye msimu wa 2011- 2012.

Simba ilitwaa ubingwa huo ikiwa chini ya Kocha Mfaransa Pierre Lechantre aliyepewa mkataba wa miezi sita tu ambao aliusaini March akichukua mikoba ya Joseph Omog.

Lechantre kwenye benchi alisaidiana na Mrundi, Masoud Djuma na baada ya kumalizika mkataba wake, hakuongeza mkataba mwingine kwani hakufikia makubaliano na uongozi.

Kwa ubingwa huo Simba ilipata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo sasa imefuzu kucheza mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Nkana FC ya Zambia itakayocheza nayo Jumamosi ya wiki hii kule Zambia.
MABAO 100 YA BOCCO

Straika na nahodha wa Simba, John Bocco msimu huu ukiwa wa 10 kwake tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara alifikisha mabao 100 na kuandika rekodi ya aina yake.

straika huyo alifikisha mabao hayo baada ya kufunga mara mbili wakati Simba ikiizamisha Mwadui mjini Shinyanga na kufunika kwani hakuna mchezaji aliyefikia idadi ya mabao ya Bocco hadi sasa, akiwa amezichezea timu mbili tu za Ligi Kuu, Azam na sasa Simba anayotamba nayo akiwa nahodha wake.

Mbali na mabao hayo lakini mwaka 2018 ulikuwa wa neema kwa straika huyo mrefu kwani alinyakua tuzo kadhaa kuanzia zile za Mchezaji Bora wa Mwezi, Mchezaji Bora wa msimu na kinara wa Msimbazi kupitua tuzo za Mo Dewji Award.

EDO ATIBUA REKODI MSIMBAZI

Kama lisingekuwa bao la straika wa Kagera Sugar, Edward ‘Eddo’ Christopher lililofungwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Magufuli, Simba ingetwaa taji la Ligi Kuu bila kupoteza mechi yoyote.

Eddo ndiye aliyetibua rekodi ya Simba kwa kufunga bao hilo lililoipa timu yake ushindi wa pointi tatu, japo siku hiyo ndio Simba ilikabidhiwa Kombe la ubingwa na Rais Magufuli huku ikikamilisha ratiba ya msimu dhidi ya Majimaji iliyoshuka daraja.

OKWI NA KIATU CHA DHAHABU

Kwa mara ya kwanza, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kucheza katika ardhi ya Tanzania ilikuwa msimu wa 2010/13 aliposajiliwa Simba akitokea SC Villa ya Uganda.

Tangu acheze Ligi ya Tanzania kwa misimu tofauti hakuwahi kutwaa Kiatu cha Dhahabu hadi msimu uliopita ambapo alifikisha mabao 20 na kuwazidi wachezaji wengine aliokuwa anakimbizana nao.

Okwi ambaye kwenye Ligi ya Tanzania amefunga mabao 70 hadi sasa, amecheza timu mbalimbali ikiwemo Yanga, Etoile du Sahel ya Tunisia, Sonderjyske ya Dernmak ambako kote huko hakudumu na kuvunja mkataba. Timu pekee ambayo huichezea kwa muda mrefu ni Simba ingawa sasa kuna habari za kutakiwa na Kaizer Chief ya Afrika Kusini.

LIGI BILA MDHAMINI MKUU

Ligi Kuu Bara msimu wa 2018-2019 ulianza ukiwa na ongezeko la timu 20, lakini bila ya mdhamini mkuu baada ya Kampuni ya Mtandao wa Simu za Mkononi, Vodacom kumaliza mkataba wake bila kuongeza tena.

Kukosekana kwa mdhamini wa ligi kumeifanya ligi kupoteza msisimko na huku klabu nyingi kulia njaa kutokana na hali ya ukata.

JPM AMWAGA PESA STARS

Baada ya Timu ya Taifa Stars kucheza mechi na Uganda ambayo ilikuwa ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika mwakani na kutoka suluhu ugenini, matokeo yaliyochangia kumshawishi Rais John Magufuli kuwaalika Ikulu na kupata naye chakula cha mchana.

Wakati JPM akiOalika Stars iliypkuwa inajiandaa kwa mechi nyingine ya kufuzu ambayo ilikuwa ya marudiano dhidi ya Lesotho, Novemba

18 ambapo ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0. Matokeo ambayo yaliwanyong’onyesha mashabiki wengi nchini japo nafasi bado ipo.

JPM iliipa Stars Sh 50 milioni ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na timu hiyo tangu aingie madarakani miaka mitatu iliyopita.

Rais aliitaka Stars kushinda mechi hiyo ili njia yake ya kufuzu kwnda kwenye fainali za Afcon ziwe rahisi kabla ya kucheza mchezo wa mwisho na Uganda utakaochezwa Machi, 2019.

DJUMA AFUNGASHIWA VIRAGO

Wakati Yanga ikikimbiwa na kocha wake mkuu, George Lwandamina kutokana na njaa iliypo Jangwani, wenzao Simba Oktoba 8, walimfungashia virago Kocha Msaidizi, Masoud Djuma aliyevunjiwa mkataba na klabu hiyo, kwasasa Djuma anaifundia AS Kigali.

Lwandamina alitimka Yanga ikisaliwa na mechi moja tu kabla ya kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho kwa sababu ya kutolipwa stahiki zake na kutoa nafasi kwa Mwinyi Zahera kutoka DR Congo kutua.

Lakini Djuma aliyesaini mkataba wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja raia wa Uganda alifurishwa kwa kushindwa kwenda sawa na bosi wake Patrick Aussems ambaye aliwaambia viongozi wake kuwa hayupo tayari kuendelea kufanyakazi na msaidizi wake kwani anawapotosha wachezaji wake.

Mengi yalizungumza na kujadiliwa, huku mashabiki wa Simba waliowengi wakipinga kuondolewa kwa Djuma aliyetokea kuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki. Lakini ukweli ulibaki pale pale lazima aondoke na muda ulipofika mkaba wake ukavunjwa.

Kabla ya kuonyeshwa mlango wa kutokea, Djuma aliachwa kwenda safari za mikoani kwa madi ya kupewa kazi ya kuwasimamia wachezaji waliokuwa na majeraha.

MAGORI, MKWABI WAULA SIMBA

Novemba 4, klabu ya Simba itakumbuka kwa kufanya uchaguzi mkuu kupata wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza tangu klabu hiyo iamue kubadilisha mfumo wa uendeshaji kutoka klabu ya wanachama na kuwa kampuni.

Simba ilipata wajumbe saba wakiongozwa na Mwenyekiti wao Swedy Mkwabi.

Pia, Crescentius Magori aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, huku Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye alikaimu nafasi ya Rais naye akiongezwa kwenye wajumbe wa bodi.

MANJI APIGWA CHINI

Baada ya kujiuzulu mwenyewe Mei mwaka jana na baadaye TFF kujichanganya na kumtambua kupitia barua ya Julai 11, Yusuf Manji kuwa Mwenyekiti wa Yanga, TFF hiyohiyo ilikuja kumpiga chini bilionea huyo wa Yanga.

TFF kupitia agizo la Baraza la Michezo (BMT) iliitisha Uchaguzi wa Yanga ambao mpaka sasa umejaa sintofahamu kibao ili kusaka viongozi wapya wa juu ikiwamo nafasi ya Mwenyekiti Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga aliyejiuzulu katikati ya mwaka huu na wajumbe wengine wanne wa Kamati ya Utendaji.

VITA YA WAMBURA NA TFF

Ni mwaka mbaya kwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na wanachama wa shirikisho hilo waliofungiwa maisha kujihusisha na soka.

Kati ya hao alikuwamo Michael Wambura ambaye alifungiwa Aprili na kufungua shauri Mahakama Kuu Tanzania Mei na kushinda shauri hilo Novemba 30, hivyo kurejea katika nafasi yake ya Makamu wa Rais wa TFF.

Wengine waliofungiwa chini ya utawala wa Rais Wallace Karia kupitia kamati ya Maadili ya shirikisho hilo ni Mbasha Matutu, Dustan Mkundi, Joseph Kanakamfumu na Robert Richard aliyefungiwa mwaka mmoja.

Kurejea kwa Wambura kumeibua ‘vita’ vya kibabe baina ya viongozi hao wa juu wa TFF, lakini pia imeshuhudia ukifanyika Uchaguzi Mdogo wa Bodi ya Ligi (TPLB) ulimuingiza Steven Mnguto kuchukua nafasi ya Clemant Sanga aliyepigwa chini Julai mwaka huu kwa kukosa sifa.