Ishu ya Ibrahim Class ipo hivi

Muktasari:

  • Awali Class alipewa kibali na Kamisheni ya kusimamia ngumi za kulipwa nchini cha kwenda kucheza nchini Marekani pambano la Desemba 15.

BONDIA Ibrahim Class na aliyekuwa msaidizi wake, Chaurembo Palasa wamefunguka kilichotokea kwenye pambano lao nchini Afrika Kusini huku kukiwa na tetesi bondia huyo alifanyiwa hujuma ili apoteze pambano hilo.

Tangu juzi Jumanne kumekuwepo na taarifa za Ibrahim Class (King Class Mawe) kupigwa na bondia wa Afrika Kusini katika mazingira tatanishi kwenye pambano lililopigwa Jumapili iliyopita kwenye Mji wa Johanesburg.

Katika pambano hilo, Class alidai hamwoni mpinzani wake na anaona giza ilipofika raundi ya tano akihisi kwenye maji aliyokuwa akipewa ulingoni yalikuwa na namna.

Wakizungumza na gazeti hili jana Jumatano, Class na Palasa kwa nyakati tofauti walielezea mazingira ya pambano hilo lilivyokuwa hadi Class kupoteza ambalo pia anadai alidhulumiwa fedha zake za pambano.

“Ulingoni pale tuliokuwa tunamhudumia Class (seconds) tulikuwa mimi na Jay Msangi, sijui nini kilitokea, lakini kuanzia raundi ya tatu Class alianza kulalamika anasikia kizunguzungu, nikamwambia, basi kama huwezi kuendelea acha pambano,” alisema Palasa.

Awali Class alipewa kibali na Kamisheni ya kusimamia ngumi za kulipwa nchini cha kwenda kucheza nchini Marekani pambano la Desemba 15.

“Tukiwa Marekani, promota alisema pambano hilo halitakuwepo, hivyo Class akawa anaendelea na mazoezi chini ya kocha Roy Fernandes,” alisema Palasa.

Alisema wakati huo Class alikuwa akiwasiliana na Jay Msangi ambaye alimwambia kuna pambano Afrika Kusini, hivyo ajiandae akapigane huko kwa kuwa lile la Marekani halipo tena,” alisema Palasa.

Akizungumzia pambano hilo, Class alisema ‘figisu’ zilianza tangu walipofika Johannesburg ambako hawakumkuta mwenyeji wao, lakini Palasa alifanya jitihada na kuwasiliana na waandaaji wa mchezo huo ambaye aliwapa maelekezo ya wapi wafikie.

“Kilichokuja kutokea kwenye mkataba wa pambano malipo yalikuwa dola 12,000 (zaidi ya Sh 22 Milioni), na ndiyo mwakilishi wa IBF Afrika (Onesmo Ngowi) wakati anatusainisha alisema na Dola 2,000 ikatolewa kwa ajili ya gharama nyingine na mimi nilipaswa kulipwa dola 10,000.

“Kilichotokea baada ya pambano, mtu aliyekabidhiwa hizo fedha alidai yeye kapewa dola 7,000 pekee na hapo hapo alitaka nimpe dola 800 za malipo ya kutafuta pambano,” alisema Class. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Emmanuel Salehe alisema hajui pambano hilo kibari chake kilitolewa vipi, hivyo atalifanyia kazi ili kujua undani wake kabla ya kuchukua hatua.

Awali kabla ya tukio hilo, Makamu Mwenyekiti wa TPBRC, Joe Anea alisema walimpa kibali Class cha kwenda kucheza Marekani pambano la Desemba 15 ambalo hata hivyo walijulishwa na wakala wa pambano hilo (Chaurembo Palasa) mpinzani wa Class amepangiwa bondia mwingine.