Ishu ya Dembele imefikia hapa

BARCELONA, HISPANIA. BARCELONA imeripotiwa kuitaka Manchester United kulipa mshahara wote wa Ousmane Dembele ili waruhusu uhamisho wa mkopo ufanyike kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Staa huyo Mfaransa analipwa Pauni 215,000 kwa wiki kwa huduma yake anayoitoa huko Barcelona na kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua Man United baada ya kukwama kwenye jitihada za kumsajili Jadon Sancho. Barca wapo tayari kumwaachia Ousmane Dembele, lakini kama tu Man United itamlipa mshahara wake wote.

Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer anataka suala la usajili wa staa mpya lifanyike haraka kabla ya dirisha la usajili kufungwa Jumatatu.

Barcelona wao wanataka pesa ili kuweka sawa mipango yao ya kiuchumi baada ya janga la corona, huku wakiwa na mpango wa kumnasa beki wa Manchester City, Eric Garcia.

Barca wao wapo tayari kumwaachia Dembele kwa dili la jumla, lakini Man United hawapo tayari kufanya hivyo, wakihitaji huduma ya mchezaji huyo kwa mkopo.

Hata kwenye hilo la mkopo, Barcelona wapo tayari kumpeleka Dembele akakipige Old Trafford, lakini kama tu wababe hao wa England watakubali kumlipa mshahara wake wote. Man United inahitaji kuongeza nguvu zaidi kwenye safu yake ya ushambuliaji, huku kiungo Paul Pogba akiripotiwa kumpigia simu Dembele akimwambia akakipige Old Trafford. Solskjaer anatarajia kupata pesa wikiendi hii kupitia kwa Chris Smalling na Andreas Pereira ambao watatimkia Italia.

Ishu ya Sancho, Man United imetanguliza Pauni 70 milioni - ambayo baadaye watalipa kidogokidogo na kufikia Pauni 100 milioni, lakini Borussia Dortmund wanataka walipwe mzigo wote.