Ishu ya Cheka na ajali ya moto iko hivi

Wednesday August 14 2019

 

By Imani Makongoro

WAKATI Taifa likiwa kwenye msiba mzito wa ajali ya moto ulioua zaidi ya watu 70 mkoani Morogoro, ghafla zikazuka taarifa kuwa bondia Francis Cheka naye amepoteza maisha kwenye ajali hiyo.

Cheka, ambaye ameitangaza Tanzania kwa muda mrefu katika anga za masumbwi, ilidaiwa kuwa alionekana kwenye eneo la tukio siku ya ajali na kwamba, baadaye hakuonekana wala taarifa zake kusikika na kuibua hofu kubwa kwa wakazi mjini humo.

Lakini, Mwanaspoti ambalo hivi karibuni lilifanya mahojiano maalumu na Cheka, linafahamu kuwa kwa sasa amehamishia makazi yake nchini Msumbiji na mengine mkoani Mtwara.

Hata hivyo, lilifanya jitihada za kumsaka bila mafanikio na kupiga hodi kwa mkewe, Toshi Azenga ambaye alionyesha kushangazwa na taarifa hizo kisha akasema kuwa, mumewe ni mzima wa afya na kuomba habari hizo zipuuzwe.

Alisema kuwa ni kweli Cheka ana makazi eneo la Kilimahewa ambako ajali imetokea, lakini akasema kila kitu kiko salama.

Taarifa za awali zilidai kwamba, Cheka alikuwa kwenye harakati za kuwazuia watu wasiibe mafuta wala kusogelea eneo hilo kwa kuwa ni hatari kwa usalama wao.

Advertisement

“Sio kweli kabisa, mume wangu ni mzima wa afya na sasa yuko Msumbiji anaendelea na shughuli zake,” alisema Toshi. “Huo ni uvumi na sijui umetokea wapi, hata familia tumeusikia na kushangazwa na jambo hili limesababisha usumbufu kwa baadhi ya watu.”

Toshi, ambaye ni mama wa watoto wawili kwa Cheka, History na Azenga alisema amewasiliana na mumewe na kumueleza jambo hilo.

“Hii mitandao kiboko, hivi tunaongea Cheka ni mzima wa afya na anafanya majukumu yake kama kawaida, hajarudi Morogoro, yuko Msumbiji kwa mama mkwe,” alisistiza Toshi huku akicheka.

Advertisement