Inter Milan yamtaka Lukaku kwa pauni 30milioni

Muktasari:

Lukaku ameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha Manchester United chini ya kocha Ole na kutoa uwezekano wa kuuzwa msimu huu

Milan, Italia. Inter Milan imesema ipo tayari kutoa pauni 30milioni pamoja na winga Ivan Perisic ili kuipata saini ya mshambuliaji wa Manchester United, Romelu Lukaku.

Winga huyo wa Croatia, Perisic amekuwa akihusishwa muda mrefu kutakiwa na Manchester United, huku Lukaku akishindwa kuonyesha ubora wake chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Kwa mujibu wa Gazzetta dello Sport la Italia, ambalo limesema kuwa Inter inamtaka Edin Dzeko kutoka AS Roma. 

Lukaku amecheza mechi 45 za mashindano yote ndani ya Manchester United msimu huu na kufanikiwa kufunga mabao 15, huku klabu hiyo ikimaliza nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England.

Inter nayo ipo katika vita ya kuwania kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa kupitia Serie A.

Inter ipo nafasi ya nne ikiwa mbele kwa pointi moja kwa watani zao wa jadi AC Milan na mbili zaidi ya Roma huku kila timu ikiwa na mchezo moja mkononi.