Imetiki! Barca kiroho safi Messi kutua City

BARCELONA, HISPANIA. KIROHO safi. Barcelona imekubali yaishe kwa Lionel Messi na imebariki uhamisho wake kujiunga na Manchester City katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Messi, 33, alikuwa anataka kuondoka katika dirisha lililopita, lakini dili lilifeli kwenye dakika za mwisho baada ya Barcelona kushilikilia msimamo kwamba kipengele kinachomruhusu mchezaji kuondoka bure kilifikia tamati kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa, hivyo Man City ilitakiwa kutoa Pauni 630 milioni ili kuvunja mkataba wa nyota huyo.

Lakini, taarifa zilizotolewa na tovuti ya The Mirror zinadai kwamba kwa sasa Barca imebariki mchakato wa mchezaji huyo kujiunga na Man City mwisho wa msimu huu kwa kuwa hawana uwezo wa kumbakisha tena licha ya kufanya jitihada za nguvu.

Messi ameonekana kutohitaji kuendelea kusalia Barcelona baada ya kufichuka kwa ripoti zinazodai kwamba kocha Ronald Koeman alimshawishi sana aongeze mkataba mpya walau wa mwaka mmoja zaidi kuendelea kusalia, lakini anaonekana kukataa akisisitiza anahitaji kuungana na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola.

Man City iko kwenye nafasi nzuri ya kuinasa saini ya Messi katika dirisha lijalo kwa kuwa mchezaji mwenyewe ameonekana kuhitaji zaidi kujiunga nao, lakini pia hakuna klabu nyingine ambayo imeonyesha nia ya kutaka kumsainisha mkataba katika dirisha kubwa lijalo.

Mtendaji Mkuu wa Man City, Omar Berrarda aliwahi kukaririwa akisema baada ya kufeli kumsainisha mkataba katika dirisha lililopita wanajipanga hadi mwisho wa msimu huu ambapo mkataba wake utakuwa unafikia tamati.

“Ni miongoni mwa wachezaji wachache wa kizazi hiki ambao wana vipaji, kikubwa hakuna timu ambayo itakataa kuwa naye inapopata nafasi hiyo, ni kweli tulikuwa tunamhitaji, lakini kwa sasa tunajaribu kupambana na hawa ambao tupo nao kwenye timu na tutajaribu kumsainisha mwisho wa msimu,” alisema Berrarda.

Msimu uliopita Barcelona ilidaiwa kukamilisha hadi mazungumzo na wawakilishi wa Messi na shida ilikuwa ni kukubaliana na Barca ambayo ndio ilikuwa kikwazo kikubwa kukamilisha dili hilo lililokuwa kwenye asilimia chache za kutimia, lakini kwa sasa mambo yako vizuri na Messi kutua Etihad ni suala la muda.

Rais wa Barca, Josep Bartomeu ni miongoni mwa watu wanaotajwa kuchangia kuondoka kwa Messi katika viunga hivyo kwa sababu ya uhusiano wao kuyumba. Inaaminika Barcelona hawana uwezo wa kumzuia tena staa huyo, ingawa kuondoka kwa Messi kunaweza kuwa mwisho wa Bartomeu kwa sababu mashabiki wanaamini ndiye aliyeifanya klabu kuwa katika hali mbaya.

Vilevile ikiwa Messi ataondoka kuna uwezekano yakazuka maandamano makubwa ya kumtaka bosi huyo wa Barcelona aachie kiti. Barca inayoshika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa La Liga imekuwa na kiwango kibovu tangu ligi ianze msimu huu ambapo imeshinda mechi mbili, sare moja na kupoteza mchezo wa mwisho dhidi ya Getafe ambapo ilipigwa bao 1-0.