Imeisha! Bifu la Ronald, Ramos lamalizwa rasmi

Madrid, Hispania. CRISTIANO Ronaldo ndio alikuwa mfalme pale Real Madrid akishinda mataji kibao kabla ya kuamua kusepa na kutua Juventus ambako nako anakiwasha kwelikweli.

Hata hivyo, Ronaldo ufalme wake ulikuwa ndani ya uwanja tu kwani, huko nje kuna mtu anaitwa Sergio Ramos, ambaye ndio alama ya wababe hao wa Santiago Bernabeu.

Ramos ndiye nahodha wa Real Madrid mwenye rekodi kibao za kuvutia akiifanya vyema kazi yake ya kukaba na kufunga pale anapotaka. Ameshinda mataji kibao akiwa sambamba na Ronaldo, lakini wawili hawa walikuwa na jambo lao kwa muda mrefu tu.

Ndio! Ronaldo na Ramos licha ya uwanjani kushirikiana kwa kila hali kusaka matokeo kwa ajili ya chama lao, lakini walikuwa maadui wakubwa wanapotoka nje ya uwanja.

Imefichuka kwa muda wa miaka miwili, Ronaldo na Ramos walikuwa kwenye bifu kali na hawakuwa wakizungumza hadi juzi usiku walipoamua kuweka pembeni tofauti zao na kurejesha maisha yao ya ushkaji kama ilivyokuwa zamani.

Ronaldo na Ramos walianza kwa kuwa marafiki wakubwa kabla ya kuwa maadui na sasa wamekuwa washkaji tena kama zamani. Mchezo wa kirafiki ulioisha suluhu dhidi ya Hispania na Ureno ndio umemaliza tofauti za mastaa hawa waliodumu pamoja kwa miaka minane.

Chanzo cha bifu la Ronaldo na Ramos ni tuzo ya Ballon d’Or aliyoshinda kiungo fundi wa mpira wa Real Madrid, Luka Modric mwaka 2018, ambapo Ronaldo hakuonekana kufurahia.

Imeelezwa, Ronaldo alikuwa na matarajio makubwa ya kushinda tuzo hiyo kwa mara ya sita ili kwenda jino kwa jino na hasimu wake, Lionel Messi lakini katika hali asiyotarajia mzigo ukaenda kwa Modric ambapo, alionyesha hadharani kutoridishwa na uamuzi huo.

Kitendo cha Ronaldo kuonyesha hali hiyo kilimkera, Ramos na hapo wawili hawa waliokuwa na nguvu na ushawishi ndani ya Madrid, wakaingia kwenye bifu ambalo hakuna aliyefanikiwa kulizima.

Juzi, baada ya mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki, Ronaldo na Ramos wakakutana na kuzungumza huku wakitangaza kumaliza tofauti zao mbele ya aliyekuwa beki kisiki wa Madrid, Pepe akiwa pembeni yao.

“Tuko pamoja, nimefurahi sana kukutana nawe rafiki yangu na mambo mazuri yanakuja,” Ramos aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii huku akiweka picha akiwa na Ronaldo na Pepe.

Katika picha hiyo, Ramos alikuwa ameshika jezi ya nahodha huyo wa Ureno yenye namba saba mgongoni ambayo ilikuwa imesainiwa na Ronaldo huku wamepeana mikono.

Ronaldo na Ramos wamekutana kwa mara ya kwanza juzi tangu alipoachana na miamba hiyo na kutimkia Juventus.