Ilikuwa ni shoo ya kibabe ya Mmakonde Luis katika uwanja mbovu

Muktasari:

Simba ina mafundi. Namungo ina wataalamu lakini mpira ambao tumeuziwa ni wa bei ya chini. Tungeweza kuuziwa mpira wa bei ghali zaidi kama wachezaji wangecheza Chamazi au Uwanja mkubwa wa Mkapa au Nyamagana pale Mwanza.

NILISAFIRI kilomita zaidi ya 1,200 kutoka Dar es Salaam kwenda Sumbawanga kuitazama fainali ya FA. Simba walikuwa wanacheza na Namungo. Kuna lugha nyingi zaidi ya hapo. Unaweza kusema pia kuwa Luis Miquissone alikuwa anacheza na Namungo. Jamaa anajua. Ni Mmakonde mwenzangu huyu. Anajua hasa. Anajua namna ya kukokota mpira, kupiga chenga, kufunga, kuudhi mabeki na kila kitu. Anajua sana. Kilichokera ni jinsi ambavyo fainali yenyewe ilichezwa katika uwanja ambao haukumstahili.

Sio yeye tu. Uwanja wenyewe haukustahili fainali. Haukustahili kwa wachezaji wa pande zote. Sio suala la chuki. Uwanja wa Nelson Mandela sio wa kwanza kuwa mbovu hapa nchini. Vipo vingi tu ambavyo vinaufanya uwanja wa juzi kuwa afadhali. Tena ni viwanja vinavyochezewa Ligi Juu. Jana yake watu waliotutawala walikuwa na mechi yao ya fainali kama hii pale Wembley. Sawa, wao ni matajiri. Sawa pambano la Arsenal na Chelsea lilichezwa katika kiwango cha juu. Hatuwezi kufikia ubora wao lakini basi tufikie walau ubora wa uwanja wao katika sehemu ya kuchezea.

Sina shida na Uwanja wa Nelson Mandela lilipofika suala la kuchukua mashabiki. Uwanja wote una majukwaa na mashabiki walikaa. Tatizo sio sisi mashabiki kukaa. Afadhali tusimame lakini uwanjani tuone soka maridadi huku wachezaji wakishindana kwa ubora wao zaidi kuliko kushindana na uwanja.

Simba ina mafundi. Namungo ina wataalamu lakini mpira ambao tumeuziwa ni wa bei ya chini. Tungeweza kuuziwa mpira wa bei ghali zaidi kama wachezaji wangecheza Chamazi au Uwanja mkubwa wa Mkapa au Nyamagana pale Mwanza.

Tatizo hili limeanza kuwa la kudumu nchini. Na nahisi litaendelea tena na tena. Jaribu kufikiria. Kwa sasa Ligi zimesimama na timu zimekijita katika kununua mastaa. Mchezaji aliyezungumzwa zaidi miongoni mwa wachezaji wa ndani, Bakari Mwamnyeto amenunuliwa na Yanga.

Siku mashabiki wa soka wa uwanja wa Nelson Mandela wakipelekewa Mwamunyeto hawataamini sana. Watamuona anabutua tu. Na ndio maana naamini kwamba hata hao Chama na Mmkonde Luis hawakuonyesha ubora wao mpaka kiwango cha mwisho kabisa.

Kuonyesha kwamba tatizo hili la viwanja litaendelea subiri uone sasa wakati huu Ligi imemalizika. TFF, bodi ya Ligi na Chama cha Mapinduzi ambacho kinamiliki viwanja vingi vya Ligi Kuu vilipaswa kuwa bize kuona namna gani ya kurekebisha hali hii. Hata hivyo msimu ujao tutacheza tena katika hali hii hii na maisha yatasonga mbele. Hapa ndipo tatizo linapoanzia. Kwanini tusitumie muda huu katika kufumua viwanja vyetu ambavyo tunajua vitachezewa Ligi Kuu msimu ujao.

Turudi katika mechi ya juzi. Ilikuwa ni mechi ambayo Simba ilidhihirisha kwamba bado imetengeneza pengo kubwa kati yao na washindani wao ambao wanajidhani ni washindani wa karibu kwao. Yanga, Azam na Namungo.

Mechi kati ya Simba na watatu hawa zimedhihirisha pengo na hali halisi. Juzi Namungo walisukumwa na kulazimishwa kufanya makosa mengi kutokana na ubora wa Simba. Clotiuos Choma, Francis Kahata na Mmakonde Luis wanapoanza kwa pamoja kunakuwa na tabu nyingi kwa wapinzani wao wa ndani. Simba haianzi na wale mawinga asilia. Pembeni huwa inaanza na viungo asilia ambao wanapisha njia kwa Shomari Kapombe na Mohamed Hussein Tshabalala kushambulia kuanzia pembeni. Eneo la mbele la SImba limejaza wachezaji wenye akili na maono katika kutengeneza nafasi.

Yanga na Azam zinajitutumua kununua mastaa kwa sasa ingawa inaacha maswali kama wataweza kushindana na Simba kwa msimu ujao. Nadhani itachukua muda kidogo kama ambavyo Simba ilivyoundwa. Iliundwa taratibu kidogo.

Hata hivyo kuna maswali mawili ambayo najiuliza. La kwanza ni hilo hapo. ni lini hawa wengineo wataiweka Simba kando katika ubora wa soka nchini. Nadhani inahitaji muda kidogo. Acha tuone watamaliza vipi usajili wao na watarekebisha vipi mabenchi yao ya ufundi.

Lakini kuna swali jingine ambalo nimekuwa nikijiuliza mara kwa kwa mara kuhusu Simba. Hawa akina Chama ni bora sana lakini wana ubavu wa kuipeleka wapi Simba katika michuano ya kimataifa. Ndani ya nchi hawakamatiki lakini nje ya nchi nimeshuhudia wakipigwa tano tano mara kadhaa katika michuano ya kimataifa msimu uliopita. Ligi yetu inadumaza? Sijui. Ninachojua ni kwamba kama ambavyo Simba inajiona imeacha pengo kubwa kati yao na wengineo hapa nchini basi ndivyo ambavyo nayo imeachwa pengo kubwa na wengineo katika soka la kimataifa.

Katika mechi za ugenini siwaoni akina Chama katika ubora huu huu wa kuwasukuma wapinzani wao kama wanavyofanya mechi za ndani. Sijui Simba wafanye nini kuziba pengo hili. Inawezekana hawa akina Chama ni Chui wa karatasi wanaotisha zaidi wapinzani wao wa ndani.

Ukisikia timu za nje zinavyowezekana kwa kununua wachezaji wa bei mbaya na kuajiri makocha wa bei mbaya, huku ukifikiria timu ya mwisho nchi hii kufika walau nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa ya Afrika ilikuwa mwaka 1974, unapata shaka kama tunaweza kurudi tena huko. Nadhani kuna jambo lazima ifanyike na Simba ibadilishe sera zake. Ifanye uwekezaji wa kweli na isijidanganye kuwa wana watimu bora zaidi inayoweza kupambana na akina Al Ahly ndani na nje ya uwanja. Wafanye kitu.