Ile vita ya FA ndio leo mjue

Friday January 24 2020

By Yohana Chale

KIPUTE cha Mashindano ya Kombe la FA kinaendelea wikiendi hii na leo Ijumaa kutakuwa na michezo miwili kwa timu kusaka nafasi ya kusonga hatua ya 16 bora.

KMC yenye kocha mpya, Haruna Harerimana ambaye alianza kwa kishindo ilipoilaza Mtibwa Sugar 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, leo Itavaana na Pan African ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Harerimana alisema hajapata muda wa kuzichunguza timu za FDL, hivyo hawajui vizuri wapinzani wake na anaingia uwanjani kutokana na uzoefu wa michezo mingine aliyoongoza timu.

“Kikubwa ninachokifanya sasa ni kuweka ‘combination’ kwa timu maana sijafanikiwa kupata kikosi cha kwanza ndio maana kila mchezo najaribu kubadilisha wachezaji niliokuwa nao ili kujua yupi anafaa wapi.

“Nitakapofanikiwa kupata wachezaji wa kikosi cha kwanza ndio naweza kusema mchezaji gani akicheza ni mpange na mwenzake ambaye wanaelewana vyema, ila kwa sasa wote wanafanya kazi vyema na ninaendelea kuwachunguza,” alisema Harerimana.

Panama FC kutoka Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) nayo itavaana na Mtwivila ya Ligi Daraja la Pili (SDL) ambayo huko haina matokeo mazuri kwani, katika michezo sita iliyocheza imevuna alama tano na inakamata nafasi ya sita kati ya saba kwenye msimamo wa Kundi C.

Advertisement

Kocha wa Mtwivila, Lissa Mwalupimbi alisema wanaingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa kutokana na umuhimu wa mchezo huo kwa timu yao katika kuhakikisha inasonga mbele kwenye FA.

“Kutokana na mazingira ya ligi yetu imekuwa ngumu kuwasoma wachezaji wa timu pinzani na tunaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na timu zote kushindwa kujuana vyema hasa uwepo wa madaraja ya ligi tunazotoka,” alisema Mwalupimbi.

Kesho Jumamosi kipute hicho kitaendelea kwa michezo nane kupigwa viwanja tofauti huku

Simba itaikaribisha Mwadui FC kwenye Uwanja wa Uhuru huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 kwenye Ligi Kuu mchezo uliofanyika Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga lililofungwa na Mathias Mdamu.

Nayo Gwambina FC atakipiga na Ruvu Shooting, African Sports itaikaribisha Mkwakwani Alliance FC, Ihefu FC itavaana na Gipco wakati Ndanda FC ikikipiga na Dodoma FC.

Michezo mingine ya kesho, bingwa wa kombe la Mapinduzi Mtibwa Sugar atakipiga na Sahare All Stars, JKT Tanzania itakuwa nyumbani kucheza na Tukuyu Stars.

Advertisement