Ilanfya, mashine KMC iliyomtoa jasho Ninja

Muktasari:

  •  Ilanfya ana sifa ya kutosha ya kuitwa mshambuliaji kwa kuwa ana maarifa, kasi na mbinu ya kufunga mabao anapokuwa ndani ya eneo la hatari la wapinzani

Dar es Salaam.Unaikumbuka timu ya Sigara iliyowahi kushiriki mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu) katika miaka ya 1980.

Ndio. Sigara ilikuwa moja ya timu tishio katika ligi hiyo na hasa kwa vigogo vya soka Simba na Yanga

Haikuwa kazi rahisi kwa miamba hiyo kupata ushindi mbele ya timu hiyo iliyokuwa ikimilikiwa na kiwanda cha kutengeneza sigara jijini, Dar es Salaam.

Umaarufu wa Sigara haukuja tu kutokana na jina lake, hapana. Mbinu na nidhamu ya mchezo ilikuwa silaha tosha kwa timu hiyo kutoa upinzani kwa wapinzani wao.

Ingawa Sigara haikuwahi kutwaa ubingwa wowote katika ligi hiyo hadi inashuka daraja na hatimaye kupotea katika ramani ya soka, lakini iliundwa na wachezaji nyota.

Ulikuwa huwezi kuitaja Sigara bila nyota waliokuwa wakitamba enzi hizo akina Gebo Peter, Aziz Nyoni, Selemani Pembe, Abunu Issa, Julius Mwakatika, Idd Cheche,  Obi Mwambungu, Kasongo Athumani, Martin Ilanfya na wengine wengi tu.

Ilanfya, alinogesha kikosi cha Sigara katika safu ya kiungo akiwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa timu hiyo ambayo ilikuwa mwiba katika mashindano hayo.

Kuna usemi unasema ‘mtoto wa nyoka ni nyoka’. Msemo huu umethibitika kwa Charles Martin Ilanfya aliyefuata nyayo za baba yake katika soka.

Jina la Ilanfya si geni kwa mashabiki wa soka hasa wanaofuatilia mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezaji huyo ndiye mpachika mabao wa KMC yenye maskani Kinondoni, Dar es Salaam akiwa mmoja wa washambuliaji chipukizi wanaoinukia vyema.

Ilanfya ana sifa ya kutosha ya kuitwa mshambuliaji kwa kuwa ana maarifa, kasi na mbinu ya kufunga mabao anapokuwa ndani ya eneo la hatari la wapinzani.

Bila shaka beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anafahamu vyema shughuli ya Ilanfya anapokuwa uwanjani.

Ninja anakumbuka namna mshambuliaji huyo alivyomtesa katika mechi yao iliyopita ambayo Yanga ilishinda mabao 2-1 kwa mbinde.

Ilanfya ndiye alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kucheza kwa kiwango bora ingawa hakufunga bao. Bao la KMC lilifungwa na Mohammed Rashid.

Ilanfya na Rashid walikuwa mwiba kwa mabeki wa Yanga na kama si beki Ally Ally kujifunga bao la pili katika harakati za kuokoa krosi ya Ibrahim Ajibu, matokeo yangekuwa sare.

Katika mazungumzo na gazeti hili, Ilanfya anamtaja baba yake ndiye aliyemuingiza katika ulimwengu wa soka kwa kuwa alipenda afuate nyayo zake.

“Baba alipoona ninaupenda mpira aliamua kuniwekea mkazo kwa kuniamsha asubuhi kwenda kukimbia naye milimani, hali ile ilikuwa ikinitengenezea kujiamini,” anasema mchezaji huyo.

Anasema baada ya kucheza mchangani hatimaye ndoto yake ya kucheza soka ya ushindani ilizaa matunda mwaka 2015 baada ya kujiunga na African Sports ya Tanga.

Ilanfya anasema baada ya kucheza kwa kiwango bora ndani ya msimu mmoja alitimkia KMC wakati huo ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Ilanfya hakutaka kubweteka katika mashindano hayo, mwakani mwaka 2018 alijiunga na Mwadui Shinyanga ya Ligi Kuu akiwa na malengo ya kukuza kipaji chake. “Nilicheza msimu mmoja Mwadui, katika usajili wa dirisha dogo nilimua kurejea KMC lengo ni kukuza na kuendeleza kipaji changu cha soka,”anasema Ilanfya.

Mchezaji huyo aliyefunga mabao mawili katika ligi hiyo anamtaja beki wa Simba Pascal Wawa ni mtu katili anapokuwa uwanjani.

Mshambuliaji ameziita Simba au  Yanga kwenda kumsajili kwasana hana woga wa kukosa namba katika kikosi cha kwanza kama baadhi ya nyota ambao wamekuwa wakihofia kuporomosha viwango vyao. Ilanfya anatoa wito kwa TFF kuboresha ligi kwa kupata udhamini  ili kuongeza kasi ya mashindano.